Bukobawadau

DOZI YA LEO JUMATANO DEC 17,HIVI WEWE VIPI?!

Labda niongee na wanaume leo, najua labda uko karibu sana na mama yako mzazi, najua unampenda sana, najua labda wewe ndio wa kiume peke yako kwenu, najua jinsi mama yako alivyoteseka sana kwa ajili ya maendeleo yako hadi hapo ulipo leo na hauna budi kumheshimu na kumpenda, najua vyote hivyo na nina viheshimu sana, hata mimi pia nina mpenda mama yangu na kumheshimu, kama wengine wengi pia walivyo, ila nafasi ya mama inabaki kuwa ya mama na nafasi ya mke wangu inabaki kuwa ya mke wangu. 
Iweje leo mama yako ndio mwamuzi mkuu wa masuala ya maisha yako na familia yako?? mjenge wapi? nyumba ya aina gani? mzae watoto wangapi? mkaishi wapi na muishi vipi? muda wa kumtembelea anaamua yeye, muda wakuwaona wajukuu anaamua yeye, maisha ya mke wako mama yako pia ndio atoe maamuzi, kila unachopanga na mkeo lazima kwanza umshirikishe mama yako akipitishe au kukipinga,labda hata yeye ndio bado anakulazimisha uendelee kuishi kwa wazazi hadi leo, mama yako ndio kashika "remote control" ya familia yako na maisha yenu kwa jumla. 
 Wewe vipi??? Hivi unafahamu maana halisi ya uamuzi wa kuoa?? Kama ulikua bado hujapevuka vyakutosha siungeendelea kuishi na mama yako?? Hivi unadhani mkeo anafurahi hata kama hakwambii? Hata wewe ungekuwa mwanamke leo, ukaolewa, ukweli ni kwamba usingeweza kuvumilia hiyo hali, sasa jiulize yeye anapata wapi kifua cha kukuvumilia wewe na huyo mama yako hadi leo. Tafakari, chukua hatua, amua kubadilika - Dr. Chris Mauki
Next Post Previous Post
Bukobawadau