Bukobawadau

IKULU:JK hatawaadhibu vigogo wa escrow bila ya uchunguzi

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
 Dar es Salaam. Ikulu imesema pamoja na kuwa Rais Jakaya Kikwete amekwishapokea maazimio ya Bunge kuhusu wanaotuhumiwa kuchota Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow, hawezi kuwachukulia hatua mpaka hapo uchunguzi kuhusu suala hilo utakapokamilika.
“Rais lazima aagize vyombo vya uchunguzi kufanya kazi yake na baada ya hapo ndipo atapata mahali pa kuanzia. Watu wengi walitaka Rais Kikwete achukue hatua baada ya kupewa maazimio ya Bunge. Jambo hilo haliwezekani,” Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema jana na kuongeza kuwa hatua zitachukuliwa kwa watakaobainika kuwa na makosa ya kimaadili au jinai baada ya uchunguzi.
Alisema uchunguzi kuhusu uchotwaji wa mabilioni hayo uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) pia utazingatiwa na Rais katika kutoa uamuzi.
“Maazimio ya Bunge ni mazuri ila inatakiwa muda kwanza ili Rais naye apate taarifa za uchunguzi zaidi. Maazimio hayo ni muhimu na si ya kupuuzwa hata kidogo,” alisema.
Alisema vyombo vinavyofanya uchunguzi kuhusu suala hilo ni vile ambavyo vilitajwa kufanya hivyo katika maazimio manane ya Bunge.
Bavicha wamtaka Kikwete achukue hatua
Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), limemtaka Rais Kikwete kuacha kuhamisha wakuu wa mikoa na badala yake atoe uamuzi wa kuwashughulisha watuhumiwa wote waliohusika na kashfa ya escrow.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu wa Bavicha, Mwita Julius alisema: “Wakati huu si mzuri wa kuanza kuhamisha wakuu wa mikoa kwa kuwa ni gharama, ni muda wa kuwachukulia hatua wahusika wote waliotajwa bungeni wakihusika na sakata la escrow.”
Alisema Rais anatakiwa kuwashughulikia wateule wake wote waliotajwa bungeni kwani wananchi wanasubiri kuona mabadiliko hayo kwa haraka.
Juzi, Rais Kikwete aliteua mkuu mmoja wa mkoa na kuwahamisha wengine sita.
Nyongeza na Hussein Issa na Hadija Salum.
MWANANCHI
Next Post Previous Post
Bukobawadau