Bukobawadau

KATIKA KUWAJIBIKA KUMBE LOWASSA JEMBE

NA PRUDENCE KARUGENDO

KUMBE  ni vigumu kupata uzuri au ubaya wa kitu kama kitu hicho hujakilinganisha na vitu vingine. Kukilinganisha ndiko kunaweza kutoa picha sahihi ya kipi kizuri kipi kibaya. Bila kuvilinganisha vitu na kupata picha sahihi ya jinsi vilivyo inaweza kutolewa hukumu ya ubaya au ya uzuri kwa kuoneana au kupendeleana.

Sakata la wizi wa pesa za umma kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow limeibua mengi, kama nilivyoonyesha kwenye makala yangu ya juma lililopita,  bado sakata hilo linaendelea kuibua mengine mengi. Lingine lililoibuliwa na kuwekwa peupe ni la ujasiri wa wasimamizi wa shughuli za serikali, mawaziri wakuu. Kwa hapa niwataje Edward Ngoyai Lowassa, aliyewajibika kwa kujiuzulu nafasi hiyo kufuatia Kashfa ya Richmond, na Mizengo Kayanza Pinda, anayegoma kuwajibika kwa kujiuzulu kufuatia kashfa mbaya kuliko zote kuwahi kutokea tangu nchi yetu ijitawale, kashfa ya “Tegeta Escrow Account”.

Tukijaribu kuzilinganisha kashfa hizi mbili, Richmond na Tegeta Escrow Account, tutaona kwamba Richmond, hata kama ilikuwa imelenga kwenye faida, lakini lengo lake kuu lilikuwa ni kuinusuru nchi isiingie kwenye janga la giza. Hiyo ni tofauti na akaunti ya Tegeta escrow ambayo ni ya pesa zilizokuwa na mashaka.

Tofauti inakuwa hivi, moja ni ya kushindwa kuwekeza na nyingine ni ya kukwapua pesa ya umma.

Akaunti hiyo ilifunguliwa kwa ajili ya kuzihifadhi pesa zilizokuwa zikitolewa na Tanesco kwa IPTL huku kampuni hiyo ya umma ikiwa inanung’unikia uhalali wake, kusudi ukweli ukipatikana wa kiasi gani halali kampuni hiyo ilipaswa kuilipa IPTL ndipo pesa hizo ziende kwa mwenyewe, kwa IPTL  au kurudi kwa aliyezitoa. Mpaka hapo pesa hizo zilikuwa bado ni umma.

Mmoja wa waliotoa ushahidi katika Mahakama ya Kimataifa ya Migogoro ya Kibiashara, London Uingereza, kuhusu pesa za akaunti ya Tegeta Escrow zilipaswa ziende kwa nani kati ya Tanesco na IPTL, Patrick Rutabanzibwa, anasema baada ya kutoa ushahidi wake katika mahakama hiyo dalili zote zilionyesha kuwa pesa hizo ni mali ya Tanesco kutokana na IPTL kuzidisha kwa makusudi ghalama za madai yake kwa Tanesco.

Rutabanzibwa anasema kwamba baada ya ukweli huo kujulikana ndipo ikaonekana kwamba pesa yote iliyokuwa kwenye akaunti ya Tegeta escrow ilipaswa iende Tanesco na bado Tanesco iendelee kuidai IPTL kiasi kingine kilichobaki.

Kilichotakiwa kufanywa kabla ya hapo ni serikali kupitia shirika lake la Tanesco kufanya mahesabu ili kujua kwa uhakika ghalama halisi waliyopaswa kuidai IPTL mbali na pesa iliyokuwa kwenye akaunti ya escrow. Lakini hicho hakikufanyika, kilichozuia mahesabu hayo kufanyika hakiko wazi. Ila inahisiwa kwamba ni kwa vile pesa hiyo ilishaanza kudokolewa kwenye akaunti ya escrow.

Na kwa vile hesabu hiyo ya ni kiasi gani cha pesa ambayo Tanesco ilipaswa kuidai IPTL haikufanyika kwa kuzishirikisha pande zote mbili, ndiyo maana CAG akasema kwamba pesa ya kwenye akaunti ya escrow ingeweza kuwa ya umma au isiwe ya umma. Hiyo ni kwa vile mahesabu ambayo yangetegua kitendawili hicho hayakufanyika.

Kwa ufupi ni kwamba lengo la IPTL halikuwa kuinusuru Tanzania isiingie gizani kama ilivyokuwa kwa Richmond,  bali kuifanyaTanzania kichaka kilichonona ambacho kila mtu angeweza kujifunzia uwindaji na kutoka ndani na mnyama, awe swala, digidigi na hata tembo! Yaani mahali pa kujizolea pesa.

Sio lengo la makala haya kutoa historia ya pesa hiyo chafu, isipokuwa tunataka kuonyesha kwa uhakika kuwa pesa hiyo ilikuwa mali ya umma  ambayo waziri mkuu, akiwa msimamizi wa shughuli zote za serikali ikiwemo pesa hiyo, alitakiwa kuwa na habari ya nini kinaendelea.
 Lowassa, tofauti na Pinda, baada ya mkakati wake kugeuka kashfa hakuwa na kigugumizi cha sikujua, kibusara aliona kuwa huo ni mzigo ulio kichwani kwake, akakubali kuutua kutokana na picha iliyoonyesha kwamba umemuelemea, akakubali kuwajibika mwenyewe ili kuilindia heshima nafasi hiyo ya waziri mkuu.
Kwa kuona hivyo wote walioguswa na kashfa hiyo hawakuwa na lingine la kufanya zaidi ya kuachia ngazi wenyewe bila kusubiri kupigiwa “nduru”, neno la Kihaya linaloashiria tukio la hatari.

Uamuzi huo wa Lowassa uliokoa mambo mengi ukiwemo muda wa Bunge, ghalama za kuliendesha Bunge mpaka usiku wa manane na hata siku ambazo si za vikao vya Bunge nakadhalika. Uamuzi huo wa Lowassa tusipouita ujasiri unaotokana na mtu kujituma akijua anautumikia umma tuuiteje?

Hata kama Spika Makinda hakutamka majina bilashaka alimaanisha tukio hilo la Lowassa pale aliposema kwamba waliowahi kuguswa na tukio la aina hiyo hawakupoteza muda kwa vile walikubali kuwajibika wenyewe, lakini hawa wamegoma. Ni wazi  alimaanisha ujasiri wa Lowassa.

Hata hivyo sote tunaelewa kwamba waziri mkuu, Mizengo Pinda, au mtoto wa mkulima,  kama yeye anavyopendelea kujulikakana, sio mtu mwenye dalili za ufisadi. Ila pale unapotokea ufisadi,  hasa ulio chini yake kama huu,  anatakiwa atuhakikishie bila kuacha chembe yoyote ya mashaka kuwa hahusiki nao.

Lakini kitendo cha kung’ang’ania kiti kwa madai ya kwamba hakujua kama kuna ufisadi unaotendeka chini yake kinatulazimisha tumuangalie vibaya, kinatufanya tumuangalie kama mtu aliyeuatamia ufisadi makusudi na kuufanya uimarike akiwa ametuficha tusiuone ila tuje kuambulia tu madhara yake.

Waziri mkuu kama alivyo Pinda anatakiwa afanye mambo kwa kusukumwa na mguso alionao kwa wananchi na kwa nchi yake, hapaswi kuongoza kwa kutumia hisia na dhana, anatakiwa atumie utashi ulio kwenye maamuzi yake mwenyewe. Sababu mara nyingi Pinda anapendelea kutumia maneno ya “mimi nadhani, mimi nahisi, mimi nafikiri (bila uhakika) nakadhalika, maneno yanayomuondoa kwenye utashi wake wa maamuzi.

Yeye akiwa waziri mkuu akifanya mambo kwa kuhisi na kudhani anategemea ni nani afanye mabo kwa uhakika uliokamilika?

Jambo zuri na jepesi ambalo angelifanya Pinda na kuendelea kuvuta imani za wananchi ni kujitenga kabisa na ufisadi huo alioutamia kwa kuondoka hapo alipo ili rais akamjaribu mtu mwingine.

Kuwajibika sio mwisho wa kuwatumikia wananchi. Mzee Ali Hassan Mwinyi aliwahi kuwajibika katika miaka ya 1970, kuwajibika huko kulibaki katika kumbukumbu za wananchi na baadaye kukachangia kumpa Mwinyi urais kwa kishindo mwishoni mwa mwaka 1985. Tayari wananchi walikuwa na imani naye kuwa yuko makini kuwalinda kutokana na kuguswa na yanayowapata. Lakini asiyekuwa tayari kuwajibika utampimaje kuwa yuko tayari kukulinda?

Sababu hata kama haya yametokea bila Pinda kuelewa, kitendo cha yeye kuukalia uchafu ambao wananchi wameishauona na kumuonyesha bila yeye kushtuka ni uzembe usiomithilika. Ni imani yangu kuwa wananchi hawapendezwi kuwa na kiongozi mzembe, maana uzembe hauwezi kuwahakikishia usalama wao na mustakabali mwema wa nchi yao.

Sakata hili la Tegeta Escrow linanifanya nimalizie makala yangu haya kwa kumpongeza Edward Lowassa kwa ujasiri wake wa kukataa kujifunga pamoja na uzembe, hivyo akaamua bila kushurutishwa kuachia ngazi, pamoja na uhondo wa ngazi hizo ulivyo. Sababu hicho ni kitendo cha kijasiri kwelikweli, huu ni ushuhuda tosha kwamba wengine kinawashinda.


0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau