KCU(1990) Ltd:Yakumbuka shuka kumekucha
NA PRUDENCE KARUGENDO
HATIMAYE mamlaka ya juu yanayosimamia na kuyalinda
masuala ya ushirika nchini yamekifanyia kazi kilio cha siku nyingi cha
wanaushirika wa mkoani Kagera kuhusu chama chao kikuu cha ushirika cha KCU
(1990) Ltd.. Mamlaka hayo yameiondoa Bodi ya wakurugenzi ya ushirika huo na
kuagiza kwamba wahusika wasiruhusiwe kugombea nafasi yoyote ya uongozi katika
ushirika huo.
Nataja tu
mamlaka ya juu kutokana na kutokuwa na uhakika ni mamlaka yapi yaliyoagiza
uamuzi huo uchukuliwe. Hiyo ilifuatia wenye mamlaka ya kufanya hivyo, Waziri wa
Kilimo, Chakula na Ushirika, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mrajis Msaidizi
kushindwa kuyashughulikia kwa wakati malalamiko ya muda mrefu ya wanaushirika
wa KCU (1990) Ltd..
Kwa karibu
kipindi cha miaka minne wanaushirika wa KCU (1990) Ltd. wamekuwa wakitoa
malalamiko yaliyosheheni hoja nzito kuhusu mwenendo mbovu wa uongozi wa
ushirika wao. Lakini jambo la kushangaza mamlaka husika yalifumba macho na
kuziba masikio yakiuacha uharibifu, hujuma na ufisadi viendelee katika ushirika
huo kiasi cha kuufanya uonekane unasambaratika kama mali siyo na mwenyewe wala
mwangalizi.
Lakini
hatahivyo zipo nafasi zilizotengwa mahususi kwa ajili ya kuulinda ushirika,
kuuimarisha na kuuboresha. Nafasi hizo ni kama ile ya Mrajis wa Vyama vya
Ushirika na wasaidizi wake wakiwemo maafisa ushirika, lakini ni ajabu kwamba
nafasi hizo zimegeuka za kuukandamiza
ushirika na kuwaacha wanaushirika wakitaabika huku wakiuona ushirika wao
ukisambaratishwa na waliopaswa kuulinda.
Wanaushirika
wanasema kwamba Mrajis msaidizi ni mwajiriwa wa serikali, lakini kimuonekano ni kama mwajiriwa wa
ushirika kutokana na kuhudumiwa na chama cha ushirika katika mambo yaliyo mengi
kiutendaji! Na katika hilo muda wote Mrajis Msaidizi anakuwa upande wa uongozi wa
chama kikuu cha ushirika akifanya kila njia kuwazuia wanachama wa ushirika
wasiweze kuuwajibisha uongozi wa chama chama chao pale unapokuwa umezembea
katika masuala mbalimbali nyeti.
Mfano mzuri
ni katika sakata ninalojaribu kulionyesha hapa la KCU (1990) Ltd.. Baadhi ya
wanaushirika, tena wanaowawakilisha wenzao wa vyama vya msingi, walikuwa na
maswali muhimu kuhusu uendeshaji wa chama chao kikuu, KCU (1990) Ltd., lakini
badala ya maswali hayo kujibiwa na Bodi ya chama hicho walinyamazishwa kwa
nguvu na hata kufukuzwa kabisa kwenye mikutano ya chama hicho bila kujali kuwa
wao ni wajumbe waliotumwa na wanaushirika, na wahenga walisema kwamba mjumbe hauawi.
Na mara
nyingi aliyekuwa akiongoza usumbufu huo dhidi ya wawakilishi wa wanaushirika ni
Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoani Kagera, ambaye kimantiki ndiye
aliyepaswa kusimama imara kuhakikisha wanauhoji uongozi kuhusu uozo uliokuwa
kwenye chama chao.
Lakini
badala yake Mrajis huyo msaidizi alijionyesha wazi anavyoungana na Bodi ya KCU
(1990) Ltd. kuuficha uozo ndani ya chama hicho, na matokeo yake KCU (1990) Ltd.
ikaanza kusambaratika.
Mtu mwingine
ambaye wanaushirika wa KCU (1990) Ltd. wanamlaani sana ni Mrajis wa Vyama vya
Ushirika, Dk. Audax Rutabanzibwa, ambaye tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo hakuonyesha
juhudi zozote za kuunusuru ushirika wao, ambao kibaya zaidi ni ushirika wa
nyumbani kwao.
Inasemekana
kwamba badala ya kuushughulikia ushirika wa KCU (1990) Ltd. Mrajis wa Vyama vya
Ushirika amekuwa akiwachukulia wote wanaojaribu kuunusuru ushirika huo kama
watu wasioupenda ushirika. Ni jambo hilo lililowafanya wanaushirika wa KCU
(1990) Ltd. waanze kuhisi uhusiano haramu kati ya Bodi ya chama chao na Mrajis
wa Vyama vya Ushirika.
Wanahoji
kitendo cha Mrajis huyo kwenda kuifukuza Bodi ya KNCU ya Kilimanjaro na
kushindwa kufanikisha matakwa yake hayo baada ya wanaushirika wa Kilimanjaro
kupiga kura wakiugomea uamuzi wake huo.
Kule
Kilimanjaro wametamka wazi kuwa Mrajis wa Vyama vya Ushirika amegeuka kikwazo
kwa maendeleo ya ushirika nchini.
Swali
linalojiweka wazi ni la kwa nini Mrajis aone kasoro kwenye KNCU wakati hajapata
malalamiko toka kwa wanaushirika wanaounda chama hicho kuhusu Bodi ya chama
chao, lakini ashindwe kuona kasoro kwenye Bodi ya KCU (1990) Ltd. pamoja na malalamiko
yote aliyoyakuta na mengine yakizidi kupelekwa kwake na wanaushirika?
Katika hali
kama hiyo unawezaje kuzipuuza hisia za wanaushirika wa KCU za kwamba kuna namna
ambayo Mrajis wa Vyama vya Ushirika alikuwa akijinufaisha na ubadhirifu
uliokuwa ukifanywa na Bodi ya Wakurugenzi wa KCU (1990) Ltd. kutokana na
ukaribu na uswahiba aliokuwa akiuonyesha kwa Bodi hiyo?
Na kwa nini
isionekane kuwa pengine uamuzi wa Mrajis wa kutaka kuifukuza Bodi ya KNCU
ulitokana na Bodi hiyo kumnyima ushirikiano kama ule aliokuwa nao kwa KCU
(1990) Ltd. wa kuuminya ushirika kwa manufaa ya wachache?
Sababu mpaka
wanaushirika wa KNCU, kule Moshi, wanatamka kwamba Mrajis ni kisiki katika njia
ya maendeleo ya ushirika, ni lazima kuna jambo baya wameliona kwake.
Sasa inasemwa
kwamba Bodi ya KCU (1990) Ltd. imeondolewa, ni kweli imeondolewa au imemaliza
muda wake? Sababu Sheria ya Ushirika ya 2013 inayotajwa kuwa ndiyo iliyotumika
kuiondoa Bodi hiyo bilashaka ilitungwa kuunusuru ushirika, kwahiyo ingetumika
mapema lazima kuna mambo yangenusurika katika KCU (1990) Ltd. kuliko sasa
ambapo chama hicho ni kama kimefilisika kabisa kutokana na uongozi mbovu wa
Bodi hiyo iliyomaliza muda wake.
Ndiyo maana
mtu mmoja kasema kwa lugha ya Kihaya kwamba “ajuna akanyonyi akajuna kakyaharara”
maana yake ni kwamba anayetaka kumnusuru ndege hufanya hivyo ndege akiwa bado
ana uwezo wa kuruka, lakini akisubiri akafa kinachofuatia ni uozo na harufu
chafu. Hakuna lingine liwezalo kufanyika.
Aliyekuwa
mwakilishi wa chama cha msingi Kamachumu, Archard F. Muhandiki, anasema kwamba
Bodi iliyofukuzwa ilimfanyia njama za kila aina kusudi asiweze kutimiza
uwakilishi wake kiukamilifu, na hatimaye ikamfukuza kabisa kutoka kwenye
uwakilishi. Kwahiyo eti kwa sasa wote, yeye na Bodi, wako nje ya shughuli za KCU (1990) Ltd..
Kwahiyo anashauri wote, yeye na waliokuwa wakurugenzi wa Bodi hiyo iliyofukuzwa,
wafanyiwe uchunguzi wa kina kusudi watakaobainika walihujumu mali za ushirika
wakamatwe na kushitakiwa na ikibidi wafilisiwe ili kufidia mali za ushirika.
Nimalizie
kwa kusema kwamba, ni kweli Bodi ya KCU (1990) Ltd. imeondolewa na kuwekwa Bodi
mpya, lakini hiyo haina tofauti na kukumbuka shuka wakati kumekucha. Nani atoe
pongezi kwa hilo?
0784 989 512