Bukobawadau

MATOKEO YA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA MKOANI KAGERA MWAKA 2014

 Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika nchi nzima siku ya Jumapili tarehe 14/12/2014 ili kuwapata viongozi wa ngazi za Mitaa, Vijiji na Vitongoji, aidha mkoani Kagera uchaguzi ulifanyika katika hali ya utulivu na amani na uliendeshwa katika halmashauri nane za mkoa wa Kagera.
Mkoa wa Kagera una jumla ya Mitaa 66, Vijiji 668, na Vitongoji 3722 aidha,  katika mkoa huo wa Kagera idadi ya wapiga kura iliyotarajiwa kuandikishwa ni 982,905 ambapo idadi halisi ya wananchi waliojitokeza na  kujiandikisha ni  767,809 sawa na asilimia 78.1
Matoke ya Uchaguzi; Katika mkoa wa Kagera vyama vya siasa vilivyoshiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni vitano kama ifuatavyo, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Civic United Front (CUF), NCCR Mageuzi, na Tanzania Labor Party (TLP)
Wenyeviti wa Mitaa; Katika Manispaa ya Bukoba kuna jumla ya mitaa 66 na uchaguzi ulifanyika katika mitaa yote 66 ambapo CCM ilishinda mitaa 34 sawa na asilimia 51.52, CHADEMA ilishinda mitaa 30 sawa na asilimia 45.45 na Chama cha CUF kilipata mitaa miwili sawa na asilimia 3.03.

Wenyeviti wa Vijiji; Katika Halmashauri za Biharamulo, Bukoba, Karagwe, Kyerwa, Missenyi, Muleba na Ngara  kuna jumla ya vijiji 668 ambapo uchaguzi ulifanyika katika vijiji 620   na CCM ilijinyakulia vijiji 443 sawa na asilimia 71.45, CHADEMA ilipata vijiji 165 sawa na asilimia 26.61

Chama cha Civic United Front (CUF) ilijinyakulia vijiji 13 sawa na asilimia 2.1 pia chama cha Tanzania Labor Party (TLP) kilijishinda katika vijiji viwili sawa na asilimia 0.3. Kutokana na kasoro mbalimbali zilizojitokeza uchaguzi haukufanyika katika vijiji 48 kwenye maeneo mbalimbali katika mkoa.
 Wenyeviti wa Vitongoji; Katika Halmashauri saba za mkoa wa Kagera ukiondoa Manispaa ya Bukoba kuna jumla ya vitongoji 3722 na kati ya hivyo CCM ilijinyakulia vitongoji 3202 sawa na asilimia 71.02, CHADEMA ilishinda vitongoji 902 sawa na asilimia 27.32,
Chama cha CUF kilishinda vitongoji 52 sawa na asilimia 1.57, chama cha NCCR Mageuzi kilishinda vitongoji  vitatu sawa na asilimia 0.09 na TLP ilijishindia vitongoji  viwili sawa na asilimia 0.06. Jumla ya vitongoji 490 uchaguzi haukufanyika tarehe 14/12/2014 kutokana na sababu mbalimbali.
 Katika ngazi ya wenyeviti wa vijiji, uchaguzi haukufanyika katika vijiji 48, na ngazi ya wenyeviti wa vitongoji  uchaguzi haukufanyika katika vitongoji 490 lakini juhudi zimeendelea kufanyika na kuanzia tarehe 15/12/2014 uchaguzi umeendelea kufanyika.
 Hivyo mara  baada ya uchaguzi kukamilika katika vijiji na vitongoji vilivyobaki bila kufanya uchaguzi na  matokeo kutolewa na wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo hayo ambapo  takwimu zilizotolewa hapo juu zinaweza kubadilika kwa kiasi kikubwa.
Next Post Previous Post
Bukobawadau