POLISI NA VURUGU
Kwa nini Polisi iwe chanzo cha
vurugu?
NA PRUDENCE KARUGENDO
UCHAGUZI wa serikali za mitaa umemalizika, katika
uchaguzi huo yamejionyesha mabadiliko makubwa katika maamuzi ya wananchi. Kwa
asilimia kubwa wananchi wameonyesha jinsi wanavyouamini upinzani kuliko utawala
uliopo. Hiyo inatokana na matokeo ya uchaguzi huo ambayo yameishusha CCM kutoka
kileleni ilikokuwa na kuileta katikati ikiwa ni ishara ya kuibwaga chini muda
mfupi ujao.
Lengo la
makala haya sio kujadili mwenendo wa uchaguzi huo kwa sasa, isipokuwa kuangalia
namna vyombo vya dola vinavyoyachukulia
maamuzi ya wananchi vikiwa havionyeshi kuyaheshimu wala kuyafurahia.
Kwa ujumla
uchaguzi huo umeendeshwa kwa amani na utulivu ukiondoa maeneo kadhaa ambako
vyombo vya dola, hasa Jeshi la Polisi, lililoamua kuingilia kati na kuanzisha
vurugu ikiwa ni ishara ya kutoyafurahia maamuzi ya wananchi. Kwa ufupi ni
kwamba wananchi, kama kawaida ya Watanzania ilivyo, waliamua kufanya uchaguzi
huo kwa amani na utulivu lakini polisi kwa kukosa kazi ya kufanya baada ya
kuona hakuna vurugu jeshi hilo wakaamua kufanya vurugu wenyewe ili waonekane
wanatimiza wajibu wao.
Jambo la
kusikitisha ni kwamba makamanda wa Polisi wanaamua kufanya kazi ya
kuwafurahisha wakubwa wao, hasa viongozi wa kisiasa wa chama tawala, kwa kufanya
mambo ya upendeleo wa wazi kwa chama tawala huku wakiwaumiza wananchi ambao
ndio waajiri wao katika kutafuta sifa na baadaye kupandishwa vyeo.
Inabidi
polisi waelewe kwamba wananchi wote bila aina yoyote ya ubaguzi ndio
wanaochangia mishahara yao kupitia kwenye kodi zinazotolewa na kila mwananchi
bila kuuliza anatoka chama gani cha siasa. Wananchi wanafanya hivyo ili
kujihakikishia usalama wao. Sasa inapokuja wakatenganishwa na kuonekana wengine
wanapendelewa dhidi ya wengine hilo ni jambo linaloweza kuamsha hisia za kwamba
wanaporwa pesa zao ili zikatumike kuwakandamiza.
Nitoe mfano
wa kitu nilichokishuhudia Mjini Bukoba. Katika uchaguzi wa serikali za mitaa
uliofanyika nchi nzima siku ya Jumapili iliyopita, wananchi wa manispaa ya
Bukoba walidhamiria kufanya mabadiliko makubwa ya kisiasa tofauti na ilivyo kawaida yao ya miaka nenda
rudi.
Kabla ya
uchaguzi huo CCM ilikuwa na mitaa 55 kwenye manispaa ya Bukoba, Chadema ilikuwa
na mitaa 9 na CUF mitaa 2. Lakini baada ya uchaguzi wa mwaka huu CCM imeshuka
chini mpaka kufikia mitaa 35 wakati Chadema ikipanda juu mpaka mitaa 29 na
kuiacha CUF kwenye mitaa ileile 2. Hiyo inaonyesha kwamba wananchi wa manispaa
ya Bukoba wamedhamiria kufanya
mabadiliko kwa kuuamini zaidi upinzani.
Jambo lingine
ni kwamba, pamoja na wananchi kufanya maamuzi hayo katika mazingira magumu ya
kusakamwa na vyombo vya dola, wananchi wa manispaa ya Bukoba wameonyesha imani
yao kwa upinzani kwa kuhakikisha wanawaweka wajumbe wote wa upinzani katika
baadhi ya mitaa ambayo waliamua kuwabakisha wenyeviti wa chama tawala. Mfano
mmojawapo ni mtaa wa Pepsi, kata ya miembeni, katika eneo la Nyamkazi ambako
mwenyekiti kachaguliwa wa CCM lakini wajumbe wake wote 5 wametoka Chadema.
Kinachosikitisha
na kuonekana kinalandana na vitendo vya vyombo vya dola ninavyovielezea hapa ni
kitendo cha mwenyekiti aliyechaguliwa katika mtaa wa Mtoni, kata ya Bakoba,
manispaa ya Bukoba, anayejulikana kwa
jina la Felician Bigambo. Katika mtaa huo wananchi wameamua kumchagua yeye kuwa
mwenyekiti kupitia CUF, lakini wajumbe wote 5 wamechaguliwa kutoka Chadema.
Mwenyekiti
huyo ameapa waziwazi kwamba kamwe hawezi
kufanya kazi na wajumbe hao wa Chadema, ambao sio wa chama chake. Hiyo maana
yake ni kwamba anapingana na maamuzi ya wananchi wa mtaa wake walioamua kuchagua
kwa mtindo huo. Lakini badala ya kujiuzulu kwa vile hakubaliani na maamuzi hayo
yeye anadai kwamba hataweza kujichanganya na wajumbe hao kuwatumikia watu wa
mtaa wake!
Pamoja na
wananchi wa mtaa wake kumuamini na kumuona anafaa kuwatumikia yeye hawaamini na
ni kama anaona wananchi hao wa mtaa wake hawafai kwa lolote!
Kwa upande mwingine mtu mmoja aliyechaguliwa
kuwa mjumbe kupitia Chadema katika mtaa wa Pepsi, kata ya Miembeni iliyopo eneo
la Nyamkazi hapa Bukona Mjini, Delifinus Lwabigene, anasema kwamba watu wa mtaa
wake wameonyesha imani kwa Chadema kwa kuwachagua wajumbe wote toka chama
hicho, isipokuwa mwenyekiti ndiye wamemtoa CCM kwa kuziamini juhudi zake
binafsi za kuwatumikia watu wa mtaa huo wakiwa hawana imani kabisa na chama
chake.
CCM imepata
mitaa 35 katika manispaa ya Bukoba, ila mitaa hiyo iko katika maeneo ambayo
wakazi wake wakijumlishwa pamoja bado idadi yao haifikii idadi ya wakazi wa
mitaa 2 ya eneo linalojulikana kama Kashai. Eneo hilo la Kashai lina mitaa 9
ambayo yote imekombwa na Chadema.
Baada ya
kutangazwa matokeo ya mtaa wa mwisho katika eneo hilo la Kashai wananchi kwa
furaha waliamua kushangilia wakielekea kwenye ofisi ya Chadema ya manispaa ya
Bukoba. Walikuwa kwenye magari, pikipiki, baiskeli na wengine kwa miguu.
Walikuwa wameshika matawi ya miti kuonyesha kuwa wanachokifanya ni cha amani.
Lakini kwa
kukasirishwa na matokeo hayo makamanda wa polisi wa manispaa ya Bukoba
waliamuru polisi kuwafuatilia wana Chadema hao na baadaye kuwazunguka kwa mbele
ili kuweka kizuizi kabla wana Chadema hao hawajafika ofisini kwao na kuwaamuru
watawanyike kwa madai kwamba wamefanya maandamano bila kibali!
Wanachadema
bila ubishi wakaamua kutawanyika, hata hivyo kutokana na wingi wao, bado polisi wakatumia kigezo hicho kudai
kwamba watu hao walikuwa bado wanaandamana. Kwahiyo wakaanza kupiga mabomu ya
kutoa machozi!
Jambo
linaloonyesha kwamba makamanda wa polisi hawakufurahishwa na matokeo ya Chadema
kuibuka kidedea, ni kwamba hata katika maeneo yaliyochukuliwa na CCM wanachama
wake walishangilia na kuandamana vilevile, lakini hatukuona polisi wakiwazuia
wala kuwaingilia kwa namna yoyote ile. Isipokuwa kuwalinda na kuhakikisha
furaha yao haiingiliwi na yeyote. Ni katika hali hiyo ambapo polisi wanakuwa
tayari kufunga hata barabara ili wana CCM waonyeshe furaha yao!
Mimi
nathubutu kusema kwamba matendo hayo yanayofanywa na chombo ambacho kipo
kulinda usalama wa raia bila kujali itikadi zao, dini wala rangi zao, ni
haramu. Ni kitendo cha kuanzisha vurugu, kitendo cha kuvunja amani ya wananchi
na kuhatarisha usalama wao.
Wana
Chadema, kama walivyo wana CCM na wafuasi wa vyama vingine, ni raia kama
walivyo raia wengine wote. Vilevile ni wanadamu kama walivyo wengine wote.
Wanaweza kufikia wakati wakakataa kuona haki zao zinapindishwa na watu walioajiriwa
kuzilinda. Na hali inapokuwa hivyo kinachofuatia ni mapambano yanayoweza
kuishia kwenye umwagikaji wa damu. Mapambano ya kujilindia haki.
Cha
kuangalia ni kwamba wanaopaswa kuhakikisha matukio hayo hayatokei, polisi, ndio wako msitari wa mbele kuhakikisha
wanaanzisha hali hiyo ya upotevu wa amani. Katika hali ya kawaida jambo hilo
linatakiwa kuangaliwa kwa umakini uliopitiliza kama kweli tunatamani kuendelea
kujivunia hali ya amani na utulivu.
Tusiwaachie
polisi wakawatumie wananchi na amani yao
kama ngazi za kupandia kuyafikia maslahi yao binafsi. Polisi wanapoviangalia tu
vyeo bila kujali vyeo hivyo wanavitumiaje na kwa manufaa ya nani, basi ieleweke kwamba hayo ni maslahi binafsi.
Wananchi hawawalipi polisi mishahara ili kuwaongezea nguvu za kuyasaka maslahi
binafsi, wanawalipa ili wakawatumikie kwa kuwahakikishia usalama wao.
Usalama
hauwezi kujitokeza kwa kuchokonoa hasira za wananchi, kwa kufanya mambo ya
kuwakera wananchi ili polisi wakaonekane wazuri kwa wakubwa wao huku wananchi
wakikandamizwa. Kwa maneno mengine ni kwamba usalama wa wananchi hauwezi
kupatikana bila ya kutendeana haki.
Inawabaidi
polisi wajifunze kutenda haki wa raia, vinginevyo Polisi itajikuta ni idara ya
kuanzisha vurugu na kuipoteza amani ya nchi kinyume na inavyotarajiwa. Matokeo
yake Tanzania itageuka kuwa kama nchi tunazodhani zimekumbwa na rahana ya
Mwenyezi Mungu kumbe ni rahana ya kujitakia.
0784 989 512