RAIS KIKWETE ATOA ZAWADI ZA MWAKA MPYA KWA MAKUNDI MAALUM MKOANI KAGERA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete asherekea sikuu ya mwaka mpya na makundi maalum
mkoani Kagera kwa kutoa zawadi mbalimbali za sikukuu kwa wahitaji katika
makundi ili kusherekea pamoja naye sikukuu ya mwaka mpya.
Zawadi hizo zilitolewa na Mkuu wa
Mkoa wa Kagera John Mongella kwa makundi maalum ambayo ni vituo vya kulelea
watoto yatima Ntoma na Kabirizi, kituo cha kulelea watoto wenye utindio wa
ubongo Kemondo na kituo cha kutunza wazee Kiilima vyote vipo katika
Halamashauri ya Wilaya ya Bukoba.
Kwa niaba ya
Rais Kikwete Mkuu wa Mkoa wa Kagera alitoa mafuta lita 20, kilo 100 za mchele,
na mbuzi mmoja kila kituo isipokuwa
kituo cha wazee Kiilima kilipatiwa mbuzi wawili. Akitoa zawadi hizo John
Mongella alisema kuwa Rais Kikwete amemwagiza kuzifikisha kwa walengwa
washerehekee naye sikukuu za kufunga mwaka.
Akitoa shukrani kwa niaba ya
wazee wenzake Mzee Evalister
Kayogera alisema Rais Kikwete amekuwa
akiwakumbuka kila mara na wanamshukuru na kumwombea dua kwa Mwenyezi Mungu ili
aendelee kumjalia afya njema na kumpa nguvu zaidi kutimiza majukumu yake
kwa ufasaha zaidi.
Mzee Evalister Kayogera alisema
wao (wazee) ni kama watoto wa ndege
ambao wanawategemea mama zao kuwaletea chakula, kwahiyo wazee wanaitegemea serikali ambayo ndiyo mama mlezi wao na imekuwa ikiwakumbuka
kwa kutoa huduma mbalimbali muhimu kwao.
Kituo cha Wazee Kiilima
kilianzishwa mwaka 1978, hadi sasa katika kituo hicho kuna jumla ya wazee 12
wanawake 4 na wanaume 8, aidha kituo hicho kinawalea watoto yatima 10 ambapo
wasichana ni wawili na wavulana wanane na kuwa jumla ya wahitaji 22.