SALMIN NA DEKO LA KISIASA ZANZIBAR
NA PRUDENCE KARUGENDO
INASHANGAZA kwamba mpaka sasa bado kuna watu wanaoendekeza
deko la kisiasa katika bara la Afrika wakati huu wa karne ya kistaarabu! Deko
linalotokana na mtu kuzitegemea nguvu za dola alizozishikilia na kuzichukulia
kama mhimili pekee wa kisiasa badala ya kuwategemea wananchi ambao ndio
wanaopaswa kutoa maamuzi ya mwisho kwa nchi yao kwa vile ndio wenye nchi, nchi
ni mali yao.
Deko la aina
hiyo limeshuhudiwa sana, hasa katika bara la Afrika, katika karne iliyopita,
ambapo watu walifikia kujipachika urais wa maisha kana kwamba wangeishi milele!
Hiyo yote ni kwa sababu ya deko la kisasa. Katika kuendeleza deko hilo
wamefanya mengi kama kutesa na hata kuua.
Lakini baada
ya mtikisiko wa kisiasa uliolikumba bara la Afrika katika karne hii tuliyomo,
mtikisiko ambao umedhihirisha kuwa wananchi ndio wenye nguvu za mwisho katika
nchi zao, nguvu ya umma, nilitegemea kwamba deko la baadhi ya wanasiasa
lingepungua na hata kuisha kabisa.
Mfano,
tumeyasikia yaliyotokea majuzi kule Burkina Faso. Rais Blaise Compaore
aliyedeka kwa karibu miaka 27 akiiona nchi hiyo kama mali yake binafsi,
alitimuliwa na wananchi kama mbwa koko baada ya kutaka kulifanya deko lake liwe
la kudumu maisha yake yote, wananchi
wakasema hapana inatosha.
Kwahiyo
nilidhani hilo la Compaore lingekuwa fundisho zuri kwa watawala wa Afrika walio
na vimelea kama vya kwake, nilikuwa na imani hiyo kutokana na tukio lenyewe
kuwa la hivi karibuni. Ila kulingana na ubaya wa deko la kisiasa ulivyo inaonekana
watawala wengi wa Afrika hawakulitilia maanani tukio hilo!
Niseme
kwamba deko ni mbaya kuliko hata ujambazi. Mtoto aliyedekezwa ni hatari kwa
familia yake kuliko mtoto mwenye tabia ya ujambazi. Madhara ya ujambazi mara
nyingi yanampata tu anayejihusisha na ujambazi, lakini madhara ya deko yanaweza
hata yakaiteketeza familia nzima, baba mama na watoto wenzake na mwenye deko.
Deko ni hatari sana.
Mfano kule
Zanzibar madhara ya deko la kisiasa yameanza kujionyesha baada ya Mnadhimu wa
Baraza la Wawakilishi, Salmin Awadhi Salmin, kutamka kwamba wananchi watapiga
kura hadi vidole vikatike lakini hawatabadilisha chochote katika Ikulu ya nchi hiyo! Deko la
ajabu. Kawaida mwenye deko haangalii uwezo wa watu wengine.
Salmin
anadai kwamba Ikulu ya Zanzibar ilipatikana kwa njia ya mapinduzi baada ya
kuondolewa kwa utawala wa kisultan mwaka 1964. Eti hiyo ni baada ya njia ya
demokrasia kukwama tangu mwaka 1957.
Kwa deko
linalomfanya aonekane kama mlevi, Salmin amediriki kutamka kwamba hata umoja wa
kitaifa Zanzibar, unaoufanya upinzani na
chama tawala vishirikiane katika kuiongoza nchi, ni bora uvunjike. Hiyo haina
tofauti na mtoto mwenye deko anavyoweza kuchezea moto kijeuri na kusababisha
nyumba iungue na kuteketeza familia nzima.
Maneno hayo
ya deko lililojaa hatari tupu, Salmin kayasemea kwenye mkutano wa kupokea
kinachoitwa Katiba Mpya inayopendekezwa katika uwanja wa Jitimahi, mkoa wa
Mjini Magharibi, Unguja.
Bila deko
ingembidi Salmin ajiulize maana ya mapinduzi ni nini. Sababu mapinduzi sio tu
kuipata Ikulu kwa maana ya kuuondoa mfumo batili unaoitawala nchi na kuingiza
mfumo mwingine batili. Mapinduzi yanalenga kuondoa utawala kandamizi kwa
wananchi na kuweiweka nchi mikononi mwa wananchi ili wakaamue wenyewe wanataka
nchi yao iendeshweje.
Lakini kauli
ya Salmin ya kwamba wapinzani hawataiona Ikulu kamwe inaonyesha kwamba
uliondolewa usultan ukarudishwa usultan mwingine, kitu ambacho ni sawa na kazi
bure.
Sio kwamba
Wazanzibari walimchukia sultan kwa sababu ya rangi yake ya Kiarabu, hapana,
waliuchukia usultan kwa vile hawakushirikishwa kumpata sultan. Na baada ya hapo
utawala wa sultan ulitaka mfumo batili wa kiutawala uendeshwe kadri ya wachache
walivyotaka badala ya wananchi walio wengi. Matokeo yake ni mapinduzi ambayo
nina imani Salmin hakuyashiriki.
Ikumbukwe
mwongozaji wa mapinduzi hayo alikuwa raia wa Uganda, John Okello, ambaye alifanyiwa mizengwe na kutelekezwa, kwa sababu ya kumhofia, bila shukurani yoyote.
Sasa kama
kilichofanya mapinduzi hayo yakatokea, kuwapora wananchi haki yao ya maamuzi,
ndicho anachokitetea Salmin kwamba kiendelee kuwepo, maana ya mapinduzi ni nini? Au maana yake ni
kumuondoa sultan mwarabu na kumuweka sultan mweusi?
Ikumbukwe
kwamba sio Zanzibar peke yake iliyofanya mapinduzi ya kuyaondoa maamuzi kwa
wachache na kuyaweka mikononi mwa wananchi walio wengi. Nchi nyingi duniani
zimefanya hivyo. Nitoe mfano mmojawapo wa nchi ya Ufaransa. Mapinduzi
yaliyofanyika katika nchi hiyo kati ya mwaka 1789 – 1799, yalilenga kuuondoa
utawala wa kifalme, sawa na usultan, na kuyaweka maamuzi mikononi mwa wananchi.
Kwa maana
nyingine neno maamuzi ndilo tunaloliita demokrasia. Kwa sasa Ufaransa ni nchi
yenye demokrasia nzuri sana duniani, hayo yakiwa ni matunda ya mapinduzi hayo
yanayotajwa. Haijawahi kutokea ikasemwa kwamba maadamu Ikulu ya nchi hiyo
ilipatikana kwa mapinduzi basi hakuna mwingine anayepaswa kuingia bila
mapinduzi. Wananchi walifanya mapinduzi ikaisha , kwahiyo wakabaki wao na
vizazi vilivyofuatia kuyafaidi mapinduzi hayo kwa kuwa na maamuzi ya ni nani
aingie katika Ikulu ya nchi yao.
Lakini
anayesema kwamba wapinzani hawawezi kuingia Ikulu kwa vile jengo hilo lililo
makao ya mkuu wa nchi lilipatikana kwa mapinduzi, anayasema hayo kwa kusukumwa
na deko la kisiasa. Sababu sio wote waliomo kwenye jengo hilo waliyashiriki
mapinduzi ya Zanzibar yaliyolifanya
likawa mikononi mwa wananchi. Na wala haina maana kwamba watu wote walio kwenye
upinzani hawakuyashiriki wala kuyapenda mapinduzi hayo.
Wapo
wapinzani walioshiriki kwenye Mapinduzi ya Zanzibar. Na kilichowafanya
wakashiriki mapinduzi hayo ndicho hiki ambacho Salmin anaapa kuwa hawatakaa
wakione, demokrasia au maamuzi ya wananchi. Kwahiyo kwa kauli yake Salmin
tunaweza kukubaliana naye kuwa anayaelewa mapinduzi? Au kwa kutokujua anajikuta akifanya kazi kama
wakala wa sultan?
Bila kuuliza
wala kujifunza ni kwamba kauli kama ya Salmin ndiyo iliyokuwa kaulimbiu ya
utawala wa kisultan. Kwa vile sultan hakuchaguliwa na wananchi basi mtu
mwingine waliyempenda wananchi kuiona Ikulu zilikuwa ni ndoto za mchana. Hayo
ndiyo anayoyasema Salmin Awadhi Salmin kwa sasa.
Lugha kama
hizo, lugha zinazoyapora mamlaka na haki za wananchi ndizo huziingiza nchi
kwenye majanga na hata ya kumwaga damu. Kama yalivyokuwa mapinduzi, damu
ilimwagika sana. Kwa maana ya kauli za Salmin ni kwamba ili wapinzani waipate
Ikulu ni lazima nao wamwage damu?
Kama hiyo ni
tofauti na anavyofikiria yeye, ana maana gani kwamba wapinzani hawataiona
Ikulu? Na kama anaelewa na kuamini kwamba CCM iko Ikulu kwa ridhaa ya wananchi
anawezaje kusema kwamba wapinzani wa Zanzibar hawataiona Ikulu milele yote? Au anataka
kutuonyesha kwamba CCM haiko Ikulu kwa ridhaa ya wananchi?
Sababu
wanaoamua nani aingie Ikulu na nani asiingie ni wananchi na wala sio CCM
yenyewe. Sasa Salmin anawezaje kutuhakikishia kwamba yumo kwenye roho ya kila
mwananchi na hivyo kuona kwamba wananchi hawawezi kukiingiza chama kingine
Ikulu zaidi ya CCM?
Kitu kingine
ni kwamba kwa mtu anayewatakia mema Wazanzibari hawezi kutamka maneno ya kwamba
umoja wa kitaifa uliopo kwa sasa ni bora uvunjike. Ubinafsi pekee ndio unaoweza
kumsukuma mtu kutoa kauli ya aina hiyo. Hiyo ni kauli iliyojaa maslahi binafsi,
isiyowajali Wazanzibari wengine.
Nimalizie
kwa kusema kwamba deko la kisiasa ni kitu hatari sana. Sababu anayeendekeza
deko la aina hiyo hawezi kuufikiria mustakabali wa nchi wala wa wananchi hata
mara moja, yeye anachong’ang’ana nacho ni atapata ni nini binafsi kupitia timu
iliyo Ikulu bila kujali majaaliwa ya nchi yake wala ya wananchi wenzake. Deko
la kisiasa ni sumu, wananchi tujihadhari
nalo.
0784 989 512