TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
C/HQ/ADM/PRESS/37 21/12/2014
Ndugu waandishi wa habari,
Tumewaita hapa leo baada ya kupata
fununu kuwa Rais Jakaya Kikwete anataka kutumia hotuba yake ya kesho na
wanaoitwa, “Wazee wa Dar es Salaam” kutetea wizi mkubwa wa fedha za umma
uliofanyika ndani ya Benki Kuu (BoT), kupitia Akaunti ya Tegeta Escrow.
Tunazo taarifa kuwa Rais Kikwete
amejipanga kuuhadaa umma kwa kisingizio cha uchunguzi wa Ikulu, ili kuwalinda
watuhumiwa ambao wanapaswa kuwajibishwa kwa kuwafuta kazi, kushitakiwa na kufirisiwa. Habari tulizozipata kutoka ndani ya Ikulu
kwenyewe, zinasema Rais Kikwete amejiandaa kumlinda Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi.
Tunapenda
kumtahadharisha Rais Kikwete kuachana mara moja na mpango wowote wa kumlinda
Profesa Muhongo na Maswi, ambao hadi muda huu walipaswa siyo kuwa nje ya ofisi,
bali walitakiwa kuwako gerezani.
Ndugu waandishi wa habari;
Umma unafahamu kwamba anayejiita
mmiliki wa kampuni ya PAP, alikabidhiwa fedha zilizokuwa katika Akaunti ya
Escrow, kabla ya kuwa mmiliki halali wa kampuni hiyo.
Ushahidi wa hili, unapatikana katika
kesi iliyofunguliwa Mahakama Kuu ya Tanzania na James Rugamalira, dhidi ya
Gavana wa Benki Kuu (BoT), Prof. Benno Ndulu, kampuni ya PAP na Benki ya
Stanbic, tawi la Tanzania.
Rugamalira alifungua shauri hili
baada ya kukuta fedha zilizokuwapo kwenye akaunti ya Escrow zimeshachukuliwa,
wakati yeye akiwa bado hajamaliziwa kiasi chake cha fedha alichokuwa anadai
baada ya kuuza asilimia 30 ya hisa zake katika IPTL.
Katika shauri hilo lililomalizika
kwa njia ya usuluhishi wa mahakama, Mahakama Kuu ya Tanzania, pamoja na
mengine, ilisema yafuatayo:
·Kwamba baada ya kampuni ya VIP kulipwa fedha zake
zilizotajwa katika mkataba, itailipa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) kodi
yote ya mapato inayotokana na mkataba inayofikia Sh. 38,
186,584,322/- (bilioni thelathini na nane milioni mia moja na themani na sita laki
tano na elfu themanini na nne na mia tatu ishirini na mbili) kama
zilivyokadiriwa na TRA kupitia Kadirio la Kodi Na. 427038820 la tarehe 15
Januari 2014.
Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani
tarehe 8 Januari 2014 na VIP ENGINEERING AND MARKETING LIMITED (VIP) kama mdai
na iliunganisha kesi za madai Na. 49/ 2002 na kesi ndogo Na. 254 YA 2003.
· Kwamba baada ya VIP kulipa kodi hiyo
kwa TRA, fedha zake zilizobaki hazitalipwa kwake mpaka pale itakapowasilisha
Cheti cha Kulipa Kodi na hati za kuhamisha asilimia 30 ya hisa zake katika IPTL
kwa mwanasheria wa PAP, na wasilisho hilo lilitakiwa kufanyika kabla ya saa 10
jioni ya tarehe 27 Januari 2014.
·Aidha, baada ya kulipwa kiwango chote cha mkataba
kilichotajwa hapo juu, VIP itathibitisha uridhiaji na ukubali wake wa
kuhamishwa asilimia 70 ya hisa za MECHMAR CORPORATION (MALAYSIA) BERHAD katika
IPTL, na uridhiaji na ukubali huo unarudishwa nyuma kuanzia tarehe ya mauzo na
uhamishaji wa hisa hizo kwa PAP.
Ndugu waandishi wa habari;
Hii maana yake nini? Jibu ni kwamba,
wakati PAP analipwa kiasi cha Sh. 321 bilioni kutoka BoT, haikuwa mmiliki
halali wa IPTL. Hakuwahi kusajili hisa zake BRELA wala hakuwa amenunua asimia
30 ya hisa za VIP.
Huu ni wizi ambao hauwezi kuvumiliwa
na umma na chama chetu, ambacho ni tegemeo la Watanzania katika kulinda
rasimaliza za taifa, ikiwamo fedha na kutetea haki za wanyonge na kusimamia
misingi ya uwajibijkaji, hakiwezi kunyamaza na kumuacha Rais Kikwete
akitekeleza mradi wake wa kulinda wezi. Hakiwezi!
Kwa msingi huo, tunamtaka Rais
Kikwete katika hotuba yake ya kesho, kuwajibisha wale wote walioshiriki kwa
namna moja au nyingine, katika kutekeleza wizi huo.
Miongoni mwao, ni Prof. Muhongo,
Maswi, Gavana wa BoT, Prof.
Ndulu, Katibu Mkuu wizara ya Fedha, Silviacius Likwelile, Waziri wa Fedha,
Saada Mkuya, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredric Werema na Mkurugenzi
Mkuu wa Tanesco, Felicesmi Mramba.
Ndugu waandishi wa habari,
Watanzania bado wanakumbuka kauli
iliyotolewa bungeni wakati wa mkutano uliopita kuwa familia ya Rais Kikwete
nayo iko nyuma ya sakata hili ikiwa mnufaikaji mkubwa kupitia kwa mtu aitwaye
Albert Marwa ambaye ana uhusiano na familia hiyo.
Kitendo cha Rais Kikwete kushindwa
kuchukua hatua madhubuti katika jambo hili, utakuwa ni ushahidi wa wazi kuwa
kigugumizi ambacho kimekuwa kikiikabili serikali yake katika jambo hili
kinasukumwa na jambo kubwa nyuma yake, ikiwamo kujilinda binafsi na kulinda
familia yake.
Ndugu waandishi wa habari,
Suala la miamala iliyofanyika
kupitia Benki ya Stanbic katika sehemu ya kashfa hiyo ya Akaunti ya Escrow, si
suala la kufanyia mzaha au kupuuzwa hata kidogo katika ufisadi huu.
Ni kupitia benki hiyo ndiko kiwango
kikubwa cha fedha zaidi ya Sh. 160 bilioni, zilibebwa kwa magunia, malumbesa na
sandarusi ndani ya siku moja mchana kweupe, tena tunaambiwa wengine walikwenda
kwa magari yenye nambari za serikali na fedha hizo zilipelekwa Ikulu ambako
Rais Kikwete anafanyia kazi na kuishi.
Ni ukweli ulio wazi kuwa hakuna
benki ndani ya nchi yetu inayoweza kufanya miamala ya mabilioni ya fedha kwa
kiwango hicho, bila BoT kuidhinisha. Kwa mantiki hiyo hiyo, Gavana Prof. Ndulu
hawezi kukwepa uwajibikaji kwenye jambo hili zito kwa kuwa alilifahamu na
kulilidhia.
Tunatarajia Rais Kikwete ataueleza
umma wa Watanzania hatua zilizochukuliwa dhidi ya watumishi hawa wa umma na
siyo kuja na visingizio vya miamala iliyochukuliwa katika Benki ya Mkombozi.
Watanzania wanasubiri kusikia Rais
Kikwete anachukua hatua dhidi ya Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum ambaye
wakati fedha katika Akaunti ya Escrow zinatolewa kati ya Septemba na Desemba
mwaka jana, alikuwa ndiye Kaimu Waziri wa Fedha.
Wakati huo, aliyekuwa Waziri wa
Fedha, Dk. William Mgimwa alikuwa katika matibabu ya ugonjwa uliopelekea kifo
chake ambacho kimedaiwa kuwa na utata, nchini Afrika Kusini.
Ndugu waandishi wa habari;
Aidha, katika kuwatafuta watu
waliochukua fedha za Akaunti ya Escrow kwa magunia na malumbesa, Rais Kikwete
aweke wazi kile kinachoonekana ushirika wa ufisadi kati ya serikali, Benki ya
Stanbic na chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia Katibu Mkuu wa
chama hicho, Abdulahman Kinana.
Tunazo taarifa za uhakika kwamba
Kinana alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo na Mjumbe wa Bodi ya Stanbic,
na ambaye alikuwa kiunganishi kikubwa kati ya serikali, CCM na Benki katika
kufanya miamala ya aina hiyo ya kifisadi.
Rais Kikwete anatarajiwa kumwagiza
Kinana awataje watu waliokwenda kuchukua mabilioni ya fedha kwa malumbesa,
magunia na sandarusi, vinginevyo atakuwa anahalalisha madai haya kuwa
ushirikiano huu si bahati mbaya na ndiyo maana, fedha kutoka Akaunti ya Escrow
ya Tegeta, zilipitia katika benki hiyo.
………………………
Arcado Ntagazwa
MWENYEKITI WA BODI YA WADHAMINI
CHADEMA.