KAGASHEKI : CCM KAZI IPO MWAKA HUU
Dar es Salaam. Hofu kuhusu nafasi ya CCM kwenye Uchaguzi Mkuu
ujao inazidi kuongezeka baada ya mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis
Kagasheki kukitabiria chama hicho tawala “kazi kubwa”, akisema hali ya
sasa “siyo ile iliyokuwa nayo miaka mitano iliyopita”.
Kagasheki pia alikitahadharisha chama hicho dhidi
ya kuzidi kukua kwa nguvu ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) akisema
iwapo umoja huo utamchagua mgombea makini, CCM itakuwa na kazi ngumu.
Balozi Kagasheki, ambaye alikuwa Waziri wa
Maliasili na Utalii kabla ya kujiuzulu kutokana na sakata la Operesheni
Tokomeza, alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa mahojiano maalum na
gazeti la Mwananchi.
Kauli yake inaungana na za vigogo wengine wa CCM
waliotahadharisha mwenendo wa chama hicho dhidi ya ongezeko la nguvu ya
upinzani, akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye, ambaye alisema
rushwa inakimaliza chama hicho, na Naibu Waziri wa Sayansi na
Teknolojia, January Makamba, ambaye alisema kuwa chama hicho kisitegemee
ushindi wa kishindo.
Akijibu swali la maoni yake kuhusu Uchaguzi Mkuu
ujao na nafasi ya CCM, Kagasheki alisema: “Ipo kazi, nafasi ya CCM
sasa... Jamii imeanza kuwa na maswali mengi kuhusu chama chetu, viongozi
wachukue hili kwa umakini, wakifuatilia watajua.”
Mbunge huyo alisema kuwa matokeo ya uchaguzi wa
Serikali za Mitaa hivi karibuni yametokana na wananchi kuona CCM
imeshindwa kuisimamia vizuri Serikali.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Desemba mwaka jana
CCM ilishinda kwa asilimia 79.81 (vijiji) na 79.83 katika vitongoji,
wakati kwenye mitaa mingi ikiwa maeneo ya mijini kimeshuka kikipata
asilimia 66.66, ikilinganishwa na ushindi wa asilimia 89.2 katika mitaa,
asilimia 91 katika vitongoji na asilimia 91.6 katika vijiji katika
uchaguzi huo mwaka 1999.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, kulikuwa na ongezeko
kubwa la ushindi wa wapinzani kwenye baadhi ya maeneo, hasa kutokana na
kusimamisha mgombea mmoja chini ya Ukawa inayounganisha vyama vya
Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
“Mengine yametokana na CCM kutoisimamia vizuri
Serikali au kutotimiza wajibu. Wapo wananchi wanaosema CCM inakumbatia
waovu. Kama inataka kuendelea kuaminika na kutumainiwa, CCM isibweteke,
isione aibu kuikosoa Serikali.
“Hapa natambua juhudi za Katibu Mkuu Abdulrahman
Kinana kuwa karibu na watu. Ipo haja kwa CCM kujitazama upya, itazame
mikakati yake, inaweza kujipanga kurudisha imani.” Kauli hiyo ya Balozi
Kagasheki imekuja siku chache baada ya Makamba, ambaye ni mbunge wa
Bumbuli kuwataka wanachama wa chama hicho kikongwe kujiandaa
kisaikolojia kwa matokeo yoyote yanayoweza kutokea katika Uchaguzi Mkuu
wa Oktoba.
“Wana-CCM wanatakiwa kujiandaa kisaikolojia kwani
walizoea ushindi wa asilimia 90 au 80, huu ulikuwa ushindi wa nyuma.
Tusishangae tukipata ushindi wa asilimia 50, 60, 57 au 70 ni kitu cha
kawaida kutokana na kukua kwa demokrasia, hususan ushindani wa vyama
vingi vya siasa kuanza kuimarika,” Makamba alisema katika kipindi cha
Power Breakfast cha Radio ya Clouds
Nguvu ya Ukawa
Kuhusu nguvu ya Ukawa, Balozi Kagasheki alisema kwamba itakuwa ni makosa kwa watu na CCM kuudharau umoja huo.
“Watu wasidharau Ukawa. Hiyo ni kitu tofauti.
Wakiweka mtu anayeeleweka, CCM iwe makini. Iweke mtu atakayeonekana
anaweza; isikurupuke, lazima awe mtu mwenye kujiamini.”
Ukawa iliibuka wakati wa Bunge la Katiba baada ya
wajumbe kutoka vyama hivyo kupinga mwenendo wa vikao vya chombo hicho
maalumu wakidai kuwa kilikuwa hakijadili maoni ya wananchi
yaliyowasilishwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na badala
yake kuweka maoni ya CCM. Uamuzi wao wa kupinga mwenendo huo uliishia
kwa vyama hivyo kujitoa kwenye mchakato wa Katiba na baadaye kukubaliana
kusimamisha mgombea mmoja kwenye chaguzi zote.
Atishwa na wanaosaka urais
Akizungumzia nafasi ya urais na waliojitokeza au
kutajwa kutaka kuwania nafasi hiyo hasa ndani ya CCM, Balozi Kagasheki
alisema anatishwa na wimbi la watu wanaosaka nafasi hiyo kwa nguvu na
kutumia pesa.
“Na hiyo mimi ndiyo inanitisha, kila mtu anaamini kwamba anaweza akakabidhiwa nchi. Jamani urais ni kitu kizito.”
Mbunge huyo alinukuu maneno ya Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere akisema: “Mimi hupenda kumnukuu hayati Mwalimu
Nyerere, yeye alisema ‘Ikulu ni mzigo’. Watu wasichukulie kauli hiyo
kama mzaha.”
“Kwanza wajipime, kuna mtu akitangaza kuwania
urais watu watasema tulitegemea, lakini mwingine akitangaza nia, watu
watasema kazi ipo, hata huyu?”
Alisema kuwa Tanzania inataka kiongozi imara,
shupavu mwenye maadili atakayeivusha nchi kutoka ilipo sasa kuipeleka
wanapotaka wananchi na kwamba wapo watu wenye rekodi nzuri za utendaji
wanaofaa kwa nafasi ya urais.
Balozi Kagasheki pia alisema kuwa utaratibu uliopo
sasa nchini hauandai viongozi wa baadaye kwa nafasi za kitaifa,
akibainisha kuwa siyo haramu kuandaa watu na kujua mapema watu wanaofaa
kuwa viongozi.
“Nashangaa kila mtu kutaka kuwa rais, binafsi naona ni zito.
Ingekuwa (jambo) jepesi, ningeshatangaza kuuwania,” alisema Balozi
Kagasheki na kusisitiza:
“Nadhani wapo watu wanaweza kuwa rais, watu
wasiwachukulie tofauti kwa hili au lile. Lakini walio wengi wanajaribu
jaribu tu bahati zao. lakini pahali penyewe pabaya, Ikulu ni sehemu
nyeti.”
Alipotakiwa kutaja watu watano anaodhani wanafaa
kwa nafasi hiyo ya urais ndani ya chama hicho, Kagasheki alisema hawezi
kutaja kwa kuwa kazi hiyo itafanywa na CCM kupitia vikao vyake.
Hata hivyo, alitaja sifa za mtu anayefaa kuwa rais
ajaye wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akisema ni lazima aweze
kuisimamia na kuitetea Katiba ya nchi bila woga.
“Zipo sifa za msingi, huwezi kuwa na makundi ukawa
rais; huwezi kuwa rais wakati Katiba inavunjwa; asiwe chanzo cha
kuvunja Muungano. Wanaotaka urais wajiulize wanaweza kusimamia hayo,”
alisema Balozi Kagasheki.
MWANANCHI
MWANANCHI