KUFUATILIA UDHAIFU WA UTEKELEZAJI/UTENDAJI WA WIZARA YA MAJI, DAWASA, DAWASCO NA EWURA
Kumb: OMU/MJ/19/01 17/01/2015
Spika
Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania
Ofisi Ndogo
Dar Es Salaam:
Mheshimiwa,
YAH: KUFUATILIA UDHAIFU WA UTEKELEZAJI/UTENDAJI
WA WIZARA YA MAJI, DAWASA, DAWASCO NA EWURA KUHUSU HATUA ZA HARAKA ZA KUBORESHA
UPATIKANAJI WA MAJI SAFI NA USHUGHULIKIAJI WA MAJI TAKA KATIKA JIJI LA DAR ES
SALAAM
Utakumbuka kwamba
tarehe 4 Februari 2013 niliwasilisha Hoja Binafsi ya kutaka hatua za haraka za
kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji
la Dar Es Salaam.
Baada ya kuwasilisha
hoja hiyo Waziri wa Maji badala ya kuchangia kwa kujibu hoja kama kanuni ya 53
(6) (c) aliwasilisha hoja tofauti kwa kutumia kanuni ya 57 (1) (c) ya kuiondoa
hoja yangu isiendelee kujadiliwa kwa maelezo kwamba “tayari kuna mpango maalum
uliotengewa fedha nyingi na Serikali ya CCM na kwa kuzingatia kuwa utekelezaji
wa mpango huo unaendelea vizuri sana”.
Waziri alikiuka kanuni
za Bunge kwa kuwasilisha hoja hiyo kwa kuwa kanuni ya 57 (4) badiliko hilo
lilikuwa linapingana na hoja kwa kuwa linaiondoa hoja yenyewe na kanuni ya 58
(5) ambayo inaelekeza kwamba hoja ikishawasilishwa anayeweza kuondoa hoja ni
mtoa hoja mwenyewe tu tena kwa idhini ya Bunge.
Aidha, Waziri wa Maji
alitoa maelezo yenye kulidanganya bunge, kujenga matumaini hewa fedha za
kutosha zimetengwa na utekelezaji unakwenda vizuri sana. Hiyo ilikuwa kinyume
kabisa na maelezo yake mwenyewe bungeni tarehe 10 Julai 2012, 7 Novemba 2012 na
nyaraka nilizonazo za ndani ya Serikali za Januari 2013.
Pia, Waziri wa Maji
hakutoa maelezo kuhusu mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi
na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam
Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) uliotumia dola milioni 164.6 hata
hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya Wachina,
hautoi maji huku kukiwa na upungufu katika uzalishaji, upotevu wakati wa
usafirishaji, udhaifu katika usambazaji na tuhuma za ufisadi katika matumizi.
Hakujibu pia iwapo
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) atafanya ukaguzi maalum wa matumizi ya fedha matumizi ya
bilioni 96.4 za mradi wa maji safi na mazingira vijijini katika Jiji la Dar es
salaam na Halmashauri zingine na kuwezesha hatua za ziada kuchukuliwa kutokana
na matumizi mabaya ya fedha pamoja na kasoro zingine katika utekelezi wa
Programu ya Maji Safi na Mazingira Vijijini (RWSSP) ikiwemo katika Manispaa za
Jiji la Dar es Salaam ilipaswa kutekelezwa kuanzia mwaka 2005/2006 na
kukamilika mwaka 2010/2011.
Kwa ujumla, hakueleza
hatua zozote ambazo Serikali ingetarajia kuchukua kutokana na hatua tisa za
haraka nilizopendekeza kwenye hoja yangu na masuala niliyotaka yazingatiwe
kutoka katika maelezo yangu ili kuboresha upatikanaji wa maji safi na
ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam. (Nakala ya Hoja nimeiambatanisha).
Ikumbukwe
kwamba mnamo tarehe 23 Machi, 2012 nilishiriki ziara ya kikazi kukagua shughuli
za DAWASA na DAWASCO ambapo wakati wa ziara hiyo nilipatiwa maelezo kuhusu
mpango maalum wa kulipatia maji Jiji la Dar es Salaam, ambao utekelezaji wake
ulianza mwaka 2011.
Katika
ziara hiyo nilitembelea Mtambo wa Maji wa Ruvu Juu, na baadaye chanzo cha maji
cha Ruvu Chini kuona kazi ya upanuzi ya mtambo wa maji wa Ruvu Chini
inavyoendelea.
Hata
hivyo, nilibaini kwamba kasi ya utekelezaji wa mradi haikuwa inaridhisha hivyo
mwezi Oktoba 2012 niliwasilisha taarifa ya hoja binafsi kutaka Bunge lipitishe
maazimio ya hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na
ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar Es Salaam.
Uamuzi
wangu uliifanya Wizara ya Maji itoe kauli ya Serikali Bungeni tarehe 7 Novemba
2012 kuhusu Mpango wa Haraka wa Maji katika Jiji la Dar Es Salaam na kutoa
ratiba ya utekelezaji.
Lakini,
baada ya kufuatilia kwa miezi miwili na kubaini kwamba hatua hizo za haraka
hazichukuliwi kikamilifu tarehe 4 Februari 2013 niliwasilisha hoja binafsi
bungeni kuhusu hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na
ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar Es Salaam.
Uamuzi
huo uliifanya Wizara ya Maji, DAWASA na DAWASCO kuchukua hatua nyingine za
ziada kabla, wakati na baada ya hoja hiyo ambazo nashukuru zimeboresha
upatikanaji wa maji safi katika baadhi ya maeneo na kuongeza jitihada za
kutekeleza miradi mbalimbali ya maji pamoja
na kuwa Waziri wa Maji alisema uongo bungeni na kupendekeza hoja hiyo
iondolewe.
Hata
hivyo, yapo maeneo mengine ambayo bado matatizo yanaendelea na kwa ujumla
Wizara imekuwa haitekelezi kikamilifu ahadi zake ilizotoa bungeni kwa nyakati
mbalimbali miaka ya 2011, 2012, 2013 na 2014.
Aidha,
kumekuwa na udhaifu wa utendaji katika Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka
(DAWASA), Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) na Mamlaka ya Udhibiti wa
Nishati na Maji (EWURA) na hivyo kupunguza ufanisi ambao ungewezesha hatua za
haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka
katika Jiji la Dar Es Salaam.
Hivyo,
kwa kuzingatia Kanuni ya 5 (1) na Nyongeza ya Nane Kanuni ndogo ya 7 (1) (c)
(e) ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Aprili 2013 naomba uelekeze Kamati ya
Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji katika vikao vinavyoendelea kabla ya Mkutano
ujao wa Bunge ifuatilie utekelezaji wa Wizara, DAWASA, DAWASCO, EWURA kwa
kurejea hoja binafsi niliyowasilisha bungeni, udhaifu unaoendelea mpaka sasa na
malalamiko ya wananchi.
Izingatiwe
kuwa mradi wa upanuzi wa Ruvu Chini ulipaswa kukamilika kabla ya mwezi Machi
2013; hata hivyo kutokana na udhaifu mbalimbali mradi huo haujakamilika mpaka
sasa.
Aidha,
kumekuwepo na udhaifu katika utekelezaji wa mradi wa ulazaji wa Bomba Kuu la
kipenyo cha milimeta 1,800 kutoka mtambo wa Ruvu Chini hadi Jijini Dar Es
Salaam ambapo ilipaswa maji yawe yamefika jijini ikiwemo katika Jimbo la Ubungo
Januari 2014 kwa gharama za Shilingi bilioni 192.68.
Kwa
upande mwingine, pamoja na Serikali ya Tanzania kupata fedha kutoka Serikali ya
India dola za Kimarekani milioni 178.125 sawa na Shilingi bilioni 289.45 kwa
ajili ya upanuzi wa chanzo cha maji Ruvu Juu kumekuwepo na udhaifu wa
utekelezaji ambao Wizara ya Maji na DAWASA wanapaswa kutoa maelezo kwa Kamati
tajwa ya Bunge.
Mradi
huo unahusisha ulazaji wa bomba kuu kutoka Mlandizi hadi Kimara; na Ujenzi wa
tanki kubwa katika eneo la Kibamba; usanifu na ujenzi wa mabomba ya usambazaji
katika maeneo ambayo hayana mtandao wa maji.
Ujenzi
wa mradi huo ulipaswa kuanza toka Agosti 2013, hata hivyo mwezi huo ulipita bila
ujenzi kuanza hali ambayo ilichelewesha hatua za haraka za kuboresha
upatikanaji wa maji safi.
Hata
baada ya kusainiwa Januari 2014 kwa mikataba ya ujenzi wa Bomba kati ya
Serikali na kampuni ya Megha Engineering and Infrastructural Ltd na wa upanuzi
wa mtambo wa kusafisha maji Septemba 2014 kati ya Serikali na Kampuni ya
VA-TECH WABAG kuna udhaifu wa utekelezaji.
Kadhalika
usanifu na utayarishaji wa vitabu vya zabuni kwa ajili wa ujenzi wa bwawa la
Kidunda Mkoani Morogoro ambalo litachangia kuboresha upatikanaji wa maji katika
mkoa huo na mikoa ya Pwani na Dar Es Salaam haukukamilika mapema 2013 kama
ambavyo Wizara ya Maji iliahidi.
Serikali
imekuwa ikisuasua kutenga kwa ukamilifu fedha za ujenzi wa bwawa tajwa
zinazokadiriwa kufikia Shilingi bilioni 179.7 hali inayohitaji Bunge kushauri
na kuisimamia Serikali ipasavyo.
Wakati
huo huo, kwa miaka mingi kumekuwepo pia udhaifu katika kuchukua hatua za
kupunguza uvujaji wa maji na maji yasiyolipiwa (non-revenue water) ambapo
ilipaswa toka mwaka 2010 kupunguzwa kutoka katika ya 50-60 mpaka asilimilia 25
lakini mpaka sasa utekelezaji ni hafifu.
Tafsiri
ya hali hii ni kwamba kwa kuondoa tu upotevu wa maji unaohusisha pia ufisadi na
biashara haramu, bila hata kuongeza kiwango cha uzalishaji nusu ya tatizo la
maji katika Jiji la Dar Es Salaam ingeweza kupungua au walau hata robo. Hatua
hii inahitaji shilingi bilioni 17 tu ambazo Wizara ya Maji, DAWASA na DAWASCO
wamekuwa wakisuasua kuzitenga na kutekeleza mipango kwa wakati.
Iwapo
hatua zote hizo za haraka na zingine zingechukuliwa maeneo ambayo mabomba
yalilazwa na kukarabatiwa ambayo hayapati maji na maeneo yote ambayo hayana
mtandao wa maji kwa sasa yangepata maji ya kutosha.
Hatua
hiyo ingeambatana na kuhakikisha maeneo mengine yanajengewa mtandao mpya wa
mabomba ya majisafi hususani Kiluvya, Kibamba, Mbezi Luisi, Mbezi Msumi,
Msakuzi, Makabe, Mpiji Magohe, Saranga, Malambamawili, King’ong’o, Matosa, Bonyokwa,
Kibangu, Kinzudi na Goba katika Jimbo la Ubungo.
Hatua
hizo zingenufaisha pia wananchi wa majimbo mengine katika Jiji la Dar Es Salaam
na Mkoa wa Pwani ikiwemo wa Kinyerezi,
Kipawa, Kiwalani, Vinguguti, Uwanja wa Ndege, Ukonga, Gongolamboto, Pugu,
Chanika, Tegeta, Bahari Beach, Boko, Bunju, Salasala, Mbezi Juu, Madale,
Kisota, Mabwepande, Mpiji, Vikawe, Mapinga, Zinga, Kilombo, Bagamoyo, Kibaha na
Mlandizi ambayo hayakufikiwa na miradi ya awali.
Hivyo, kikao na Kamati ya Bunge
kitawezesha hatua za haraka za kutolewa kwa kiasi cha Shilingi bilioni 138.85
zinazohitajika kufanikisha kazi hiyo.
Yapo
masuala mengi mengine ambayo ni muhimu yakazingatiwa na Bunge kuhusu hatua za
haraka za uboreshaji wa upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka
katika Jiji la Dar Es Salaam ambayo nitayawasilisha kwa Kamati husika ya Bunge
ikiwaita viongozi na watendaji wakuu wa Wizara ya Maji, DAWASA, DAWASCO na
EWURA.
Wako
katika uwakilishi wa wananchi,
John
Mnyika (Mb)