WILAYANI KYERWA NA UTATU MTAKA FUJO!!
Picha kutoka maktaba yetu.
NA PRUDENCE KARUGENDO
KYERWA ni wilaya mpya
iliyoundwa kutoka katika wilaya
ya Karagwe mkoani Kagera. Wilaya hiyo iko mpakani mwa Tanzania na nchi
mbili za Uganda, upande wa Kaskazini na Rwanda kwa upande wa Magharibi,
Kaskazini
Magharibi mwa Tanzania.
Wananchi wa wilaya hiyo
kisiasa kwa sasa wanaimba wimbo wa majuto ni mjukuu. Hiyo ni baada ya
kukabiliana na hali ambayo hawakuitegemea, walidhani kutengewa wilaya ya kwao
wakiwa wametolewa kwenye wilaya ya Karagwe, kungewapatia faraja ambayo wangeitumia
kuboresha ustawi wao. Lakini badala yake wanasema wameingizwa kwenye matatizo
ambayo hawakuwahi kuyashuhudia tangu nchi yao
iwe huru zaidi ya miaka 53 iliyopita.
Wengine wamediriki kusema
kwamba hali ilivyo kwa wakati huu kule Kyerwa haikuwahi kuwa hivyo hata wakati
wa wakoloni. Watu wameyakimbia makazi yao na kuhamia maporini ili kujinusuru na
mashambulizi ya vyombo vya dola yanayofanyika kwa maelekezo ya viongozi wa
wilaya hiyo waliochukizwa na maamuzi halali ya wananchi wakati wa uchaguzi wa
serikali za mitaa.
Wana Kyerwa wanasema kwamba
uchaguzi wa serikali za mitaa upo kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu, na kwamba
uchaguzi huo umefanyika kwa kuvihusisha vyama vingi vya siasa ambavyo navyo
vipo kwa mujibu wa Katiba ya nchi. Kwamba katika uchaguzi wa aina hiyo wao wana
haki ya kumchagua mtu kutoka katika chama chochote ambaye wanamuona anawafaa.
Hakuna sheria inayoamuru kwamba achaguliwe tu wa chama fulani, kiwe chama
tawala au cha upinzani. Eti kama sheria ingesema hivyo wala kusingekuwepo na
haja ya kuhangaika na uchaguzi.
Lakini wananchi hao
wanashangaa kuona viongozi wa serikali wanawachukulia kama watu wahalifu
kutokana na maamuzi waliyoyafanya ya kuamua wamchague nani na wamuache nani,
kana kwamba maamuzi yao
hayo yamevunja sheria au Katiba ya nchi.
Wanasema kwamba katika maeneo
mbalimbali ya wilaya hiyo matokeo ya kura zilizopigwa yalitangazwa chini ya mtutu
wa bunduki na mengi yakiwa yamegeuzwa kimabavu kwa kuwatangaza walioshindwa
kuwa ndio wameshinda. Waliojaribu kuyahoji matokeo hayo ya kughushi
walichukuliwa kwamba wanafanya fujo na hivyo kushambuliwa na vyombo vya dola
huku wengine wakikamatwa na kuwekwa ndani kwa visingizio mbalimbali. Zaidi ya
vijana 50 waliwekwa ndani.
Katika hali hiyo wananchi wa
Kyerwa, bila kujali tofauti zao kiitikadi, wamelalamika sana wakisema kwamba kwa mtindo huo uongozi
wa wilaya hiyo umeshindwa kabisa kuiongoza na hivyo kuviachia vyombo vya dola
kuitawala kwa mabavu dhidi ya matakwa ya wananchi.
Sababu wanasema kwamba
kuongoza ni pamoja na kuwashawishi wananchi ili wakikubali na kukiamini
wanachoelezwa kuwa ni cha kweli. Lakini kiongozi anayeshindwa kufanya hivyo
wananchi wanaachana naye na kumchukua yule anayeweza kuwashawishi wakamuamini.
Ila walio madarakani hawataki kukiri kuwa wameshindwa kuwashawishi wananchi,
ndipo wanapotumia ushawishi walio nao kwa vyombo vya dola kuanza kuwashambulia
wananchi kama njia ya kulipiza kisasi kutokana
na kukataliwa kwao!
Eti viongozi hao wa mabavu,
walio chini ya chama tawala, wanachotaka kieleweke kwa wakubwa wao kitaifa ni
kwamba wamefanikiwa kuwafanya wananchi wawakubali viongozi waliogombea kupitia
chama tawala wakati sio kweli.
Jambo hilo limewafanya hata wale waliokuwa
wanakipenda chama tawala waanze kufikiria vinginevyo, sababu wanasema kwamba
tofauti za kiitikadi sio uhasama. Wapo watu wanaotofautiana kiitikadi lakini
bado ni ndugu na marafiki. Hakuna mwana CCM aliye na ndugu mwana Chadema, kwa
mfano, anayependa kumuona ndugu yake akilala porini kuwakwepa polisi wasije
kumkamata kutokana na kutompigia kura mtu wa CCM.
Suala hilo ndilo limeifanya CCM kuanguka chali
katika maeneo mengi ya vijijini tofauti na kawaida ya miaka nendarudi, na
kinyume cha imani ya chama hicho kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa
mwaka jana.
Kwa ufupi wananchi hao wa
Kyerwa wanasema kwamba vyama vingi vya siasa havikuja kuwatenganisha wananchi
na kuwavunjia undugu au urafiki. Wanasema hayo yote yanatokana na tatizo la
kutokubali kushindwa kunakotokana na kutoiheshimu demokrasia ya vyama vingi vya
siasa wala kuelewa maana yake. Wanaongeza kwamba tatizo hilo
limo sana kwenye chama tawala ambacho
kinawakumbatia sana
watu wenye uwezo mdogo kiushawishi.
Aidha, wamesema ni aibu sana kwa wakati huu, baada
ya miaka 54 ya uhuru wa nchi, chama tawala kinakosa watu wenye kujenga
ushawishi ili wananchi wakikubali chama hicho, na badala yake kinaegemea kwenye mabavu na
vitisho vya vyombo vya dola. Wanakumbusha jinsi Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere,
alivyokuwa na uwezo mkubwa wa kujenga hoja na kushawishi tangu kwenye harakati
za kudai uhuru wa nchi hii.
Kwamba uwezo huo wa Nyerere
ulimfanya asifikirie hata mara moja kutumia mabavu ya kivita kuudai uhuru. Eti
baada ya miaka 53 ya uhuru makada wa chama tawala ndipo wanafikiria mabavu ya
kivita baada ya kushindwa kuwashawishi wananchi!
Kitu wanachokionyesha
wananchi hao wa Kyerwa kuwa ndilo tatizo kuu linalowavurugia usalama wao ni
kile wanachokiita “utatu mpenda fujo”. Wanasema utatu huo unaundwa na mbunge wa
wilaya hiyo, Eustace Katagira, MNEC wa CCM wa wilaya hiyo, Daniel Damian na
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Kashunju Runyogote.
Wananchi wa Kyerwa wanasema
kwa nguvu zote kwamba fujo zinazofanywa na utatu huo, hata kama
zinafanywa zionekane ni za kukihami chama tawala, eti hazina uhusiano hata
kidogo na chama hicho. Eti hizo ni fujo binafsi zilizolenga kwenye maslahi
binafsi ya watu wanaounda utatu huo. Kwamba kwa hapo utatu huo unakitumia chama
tawala kama kinga ya mambo yao
binafsi wanayoyafanya bila chama hicho kuwa na habari nayo.
Fujo za utatu huo ndizo zinazowafanya
hata walio wana CCM katika wilaya ya Kyerwa kuanza kujiuliza kwa nini chama
chao kisizimulike fujo hizo? Sababu eti hazionyeshi uhusiano wowote na chama
chao wala kuonyesha kama wahusika wanayafanya
hayo kwa mapenzi ya chama chao, sababu eti wanayoyajua wao kwamba ndicho chanzo
cha fujo hizo hayana manufaa yoyote kwa chama hicho.
Wananchi hao wanaeleza kwamba
katika utatu huo wa fujo kuna biashara ya ulanguzi wa kahawa ambayo haitakiwi
ifanywe na mtu mwingine yeyote. Pia eti asilimia kubwa ya ardhi ya wilaya ya
Kyerwa imehodhiwa ndani ya utatu huo, eti maeneo mengi makubwa ya ardhi
yamefungwa kwa matumizi ya wananchi wengine, bila kujali ni wana CCM au wa
vyama vingine, kiasi cha wananchi kukosa mahali pa kufanyia shughuli zao za
kawaida, kama kulima mazao ya msimu kama vile
karanga, njugumawe, viazi mviringo nakadhalika.
Pia kutokana na tatizo hilo la kuhodhi ardhi, wanachi wanasema wanapata shida ya
malisho kwa mifugo yao.
Eti hilo ni
tatizo lisilokuwa na uhusiano wowote na CCM. Kwamba chama hicho kisingependa
kuona hata walio wananchama wake wanapata usumbufu unaolazimishwa na utatu huo
wa fujo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Kyerwa, Kashunju Runyogote, anasemwa na wananchi hao kuwa aliwahi kukabiliwa na
kashfa ya ubadhirifu wa pesa za halmashauri ya Karagwe, kabla ya kutenganishwa
na Kyerwa, kiasi cha chama chake kutuma wakaguzi kuangalia kuna nini kwenye
halmashauri hiyo. Inadaiwa alitumia pesa hiyo kwenda kufanya “matanuzi” kutalii
nchini Rwanda.
Kwahiyo inapaswa ieleweke
kwamba manyanyaso wanayoyapata wananchi kwa visingizio vya kiitikadi na
kuwafanya waishi kama wananchi haramu kwenye nchi yao, siyo yote yanafanyika kwa msukumo wa
kukipenda chama hicho tawala. Ila wapo wanaotumia jina la chama hicho kufanya
mambo yao machafu kwa wananchi, hata kwa
walio wanachama wa chama hicho, kwa
ajili ya maslahi binafsi bila chama hicho tawala kuwa na habari.
Rai yangu ni kwamba CCM
inatakiwa kulifanyia kazi suala hilo
kabla hali ya mambo haijawa mbaya zaidi kiasi cha kukifanya chama hicho
kushindwa kuimiliki.
0784 989 512