MUHONGO AMFUATA JK USWISI
WAKATI Watanzania wakisubiri kujua hatima ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, aliyewekwa kiporo na Rais Jakaya Kikwete baada ya kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, waziri huyo amesafiri kwenda Davos nchini Uswisi kuungana na rais katika Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani maarufu kama World Economic Forum.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Muhongo ameondoka nchini jana.
“Profesa ameondoka leo (jana) kwenda Switzerland (Uswisi) ambako ataungana na rais kwenye mkutano huo utakaoanza Januari 21 hadi 24,” kilipasha chanzo hicho.
MTANZANIA ilipomtafuta Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Salva Rweyemamu, ili kuthibitisha taarifa hiyo, hakuweza kutoa jibu na badala yake kumporomoshea mwandishi matusi huku akimwambia aachane na habari hiyo.
“Acha habari zenu za kipumbavu hizo,” alisema Salva.
Alipoulizwa habari za kipumbavu ni zipi na kwanini anatukana badala ya kutoa majibu alisema: “Nimekwambia acha upumbavu, kama unataka habari nipigie na kama hutaki usinipigie, siyo kila kitu mnachoandika tu lazima nizungumzie,” alisema na kukata simu.
Akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam Desemba 22 mwaka jana, Rais Kikwete alitangaza kumuweka kiporo Profesa Muhongo akisubiri kupata ufafanuzi kuhusu mambo kadha wa kadha ili kujiridhisha kabla kuujulisha umma juu ya hatua atakazochukua dhidi ya waziri huyo.
Wakati akimuweka kiporo Muhongo, Rais Kikwete alitangaza kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka baada ya vyombo vya Serikali kubaini na kujiridhisha amekiuka maadili ya utumishi wa umma kwa kuingiziwa Sh bilioni 1.65 kwenye akaunti yake binafsi.