SIRI NZITO CCM 2015
Dar na Z’bar. Vikao vya Kamati Kuu ya CCM na Kamati Maalumu ya
NEC Zanzibar vinaonekana kuwa huenda vikaiweka hadharani siri nzito za
urais wa Jamhuri ya Muungano.
Mkutano wa sekretarieti ndiyo utakaoanza leo
ukifuatiwa na Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar huku Kamati Kuu ya CCM
ikitarajiwa kukutana Jumanne wiki ijayo katika Ofisi Kuu ya CCM
Kisiwandui kujadili na kutathmini hali ya kisasa kuelekea Uchaguzi Mkuu
mwaka huu.
Kikao hicho kimekuja huku wagombea wa nafasi ya
urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho wakipishana
kwa usafiri wa ndege na boti kwenda Zanzibar kutafutwa kuungwa mkono na
wajumbe wa NEC na waliopo visiwani humo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai
alithibitisha kikao hicho kufanyika Zanzibar na kitaoongozwa na
Mwenyekiti wake Rais Dk Jakaya Kikwete ambaye amebakisha muda mfupi
kumaliza muhula wake wa uongozi tangu aingie madarakani mwaka 2005.
Vuai alisema Kamati Kuu ya CCM itakutana, itatanguliwa na Kikao cha Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar.
Alisema suala kubwa ambalo watalijadili ni
kuangalia mwenendo wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka
2010/2015 tangu kumalizika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Hata hivyo, Vuai alisema hayuko tayari kuzungumzia
ajenda ya kikao cha Kamati Kuu kwa vile majukumu hayo yako kwa Katibu
wa Itikadi na Uenezi Taifa, Nape Nnauye.
Pia, alisema Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar
itakuwa na ajenda ya mengineyo itakayojadili hali ya kisiasa tangu
kumalizika uchaguzi mkuu uliopita ambapo kikao hicho tayari matayarisho
yake yamekamilika kabla ya kuanza kamati Kuu kukutana visiwani humu.
Nape
Hata hivyo, Nape alisema jana kuwa Sekretarieti ya
Halmashauri Kuu ya CCM, inakutana leo jijini Dar es Salaam kupanga
ajenda zitakazojadiliwa kwenye mkutano wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu
ya Taifa ya chama hicho itakayokutana Zanzibar Jumanne ijayo.
Alisema kuwa kikao hicho ni cha kawaida cha siku moja chini ya Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete.
Kikao cha Kamati Kuu kinakutana na kukiwa na
patashika ya makada wa CCM wanaotajwa kuwania nafasi ya urais
wakipishana kwa safari za usafiri wa majini na angani na wapambe wao
kukutana na wajumbe wa NEC na mkutano mkuu katika vikao vya faragha
Pemba na Unguja kuomba ushawishi wa kuungwa mkono.
Hali ya kisiasa Zanzibar, inadaiwa kuchafuka na kuhatarisha
uimara wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) baada ya vigogo wa Serikali
hiyo kuanza kunyosheana vidole hadharani.
Inaelezwa kuwa joto la uchaguzi wa urais ndilo
ambalo limesabasisha hali hiyo itokee. Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim,
Seif Shariff Hamad na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein huenda
wakachuana katika uchaguzi wa urais mwaka huu.
Sauala lingine zito ambalo linaweza kujadiliwa
katika vikao hivyo ni la kashfa ya escrow ambayo imewakumba mawaziri na
baadhi ya madaka wa chama hicho.
Mawaziri ambao wamekumbwa na kashfa hiyo ni pamoja
na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa
Anna Tibaijuka ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospter Muhongo.
Profesa Tibaijuka tayari ameondolewa kwenye nafasi
yake ya uwaziri baada ya kupokea kiasi cha Sh1.6 bilioni kutoka kwa
Mfanyabiashara maarufu nchini, James Rugemarila ambaye ni mbia wa
Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL.
Mwingine anayetajwa kuhusika ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge
ya Sheria na Katiba, William Ngeleja na Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo.
Mbali na wahusika wa Akaunti ya Escrow, vikao
hivyo huenda vikajadili ripoti ya maadili ya viongozi ikiwamo
waliokumbwa zuio la kujihusisha na kampeni za kuwania urais mapema kwa
miezi 12, huku mienendo yao ya kisiasa ikifuatiliwa.
Waliozuiwa kufanya kampeni ni Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi, Teknolojia January Makamba, Waziri Mkuu Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na
Uratibu), Steven Wassira na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini
ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Hata hivyo, Nape alipoulizwa kuhusiana na wagombea
wa urais kufanya kampeni za nguvu na wengine kutumia mitandao ya simu
kusambaza ujumbe, alikataa kuzungumza chochote kuhusiana na suala hilo
pamoja na sakata la escrow iwapo litapewa nafasi katika vikao hivyo vya
chama.
Mtikisiko Zanzibar
Maalim Seif hivi karibuni alikaririwa akisema
atapambana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwenye vikao vya
Serikali na kulalamika kuna baadhi ya masheha, wakuu wa wilaya na mikoa
wakiwanyima wananchi haki ya kupata vitambulisho vya Uzanzibari mkaazi
na kutoandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Kupiga.
Akijibu dai hilo, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Balozi Seif
alisema hakuna wananchi wanaokatazwa kupata Vitambulisho vya Mzanzibari
mkaazi na kueleza kuwa chini ya Sheria Namba 7 ya mwaka 2005 hakuna mtu
ambaye anaweza kupewa kama siyo mkaazi wa Zanzibar kwa miaka mitatu.
Balozi Seif alisema Serikali haitakubali kupata
hasara ya kuzalisha vitambulisho kutokana na idadi kubwa ya zaidi
kuandikishwa watu ambao siyo wakazi ya Pemba, wakati kuna vitambulisho
vingi vimeshindwa kuchukuliwa na wenyewe ambao alisema ni mamluki.
Mjumbe mmoja wa NEC ambaye ameomba jina lake
lihifadhiwe, alithibitisha vigogo wanaowania urais na wapambe wao
kumshawishi kuingia katika kundi lao.
Wagombea urais
Vigogo wa urais waliofanya ziara kwa nyakati
tofauti hivi karibuni visiwani Zanzibar ni pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu
Fredrick Sumaye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano) Stephen
Wasira, Mbunge wa Sengerema William Ngeleja na Waziri Mkuu Mizengo Pinda
ambaye amealikwa kuhudhuria Maulid ya Kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) leo
yaliyoandaliwa na Mbunge wa Mpendae na Mafanyabiasha mashuhuri, Salum
Turky.
Kadhalika Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa ambaye wakati wa Sikukuu ya Krismasi ya mwaka jana alikuwa Zanzibar.
MWANANCHI.
MWANANCHI.