TOFAUTI YA MUZIKI NA MAKELELE
Tusifanye muziki na makelele kuwa ni kitu kilekile
NA PRUDENCE KARUGENDO
KUPUNGUA kwa vipaji vya muziki hapa nchini kwa kiasi
kikubwa kumelifanya neno muziki kubadilishwa maana yake. Baada ya wanamuziki,
kwa maana ya wapiga muziki, kupungua karibu na kuisha wapenda muziki wameanza
kubuni njia nyingine za kuutambua muziki ilmradi neno muziki liendelee kuwepo.
Katika kufanya hivyo chochote chenye kutoa sauti kinadaiwa ni muziki pasipo
kutofautisha kipi ni muziki na kipi ni kelele.
Muziki, kwa maana halisi, ni mpangilio maalumu wa
sauti zinazotoka kwenye ala, vyombo vya muziki, zinazopigwa kiufundi. Sauti
inayopatikana toka kwenye vyombo hivyo ndiyo huitwa muziki.
Sio lazima sauti hizo
ziambatane na maneno, hata kama maneno
yanaingizwa, nyimbo, ni kwa ajili tu ya kuurembesha muziki, sababu maneno peke
yake hayawi muziki bali ni nyimbo. Bado muziki unabaki kuwa sauti zinazotokana
na vyombo vinavyochezwa na binadamu.
Hiyo ndiyo sababu kikundi cha
watu, kwaya kwa mfano, kinachoimba bila kucheza vyombo vya muziki hakiitwi
kikundi cha wanamuziki bali kikundi cha nyimbo au cha waimbaji. Vivyo hivyo kwa
waimbaji wa mashairi, hawaitwi wanamuziki, ni kwa sababu mashairi mara zote
hayahusishi vyomvo vya muziki.
Lakini kwa watu wenye kutumia
vyombo vya muziki kutoa sauti, hata kama hawaweki maneno ya nyimbo, kama
zilivyo bendi za Polisi na Jeshi zitumbuizapo kwenye shughuli maalumu kama gwaride, wanaitwa wanamuziki kutokana na uwezo wao
wa kucheza vyombo vinavyotoa muziki.
Sasa kutokana na ukosefu wa
watu wenye uwezo kuchezesha vyombo vya muziki huku uraiani, ndipo tunaposikia
kitu kinachoitwa muziki wa kizazi kipya! Hicho ni kitu wanachokifanya vijana
wasio na uwezo wa kupiga muziki bali vipaji vya kutunga mashairi na kuyapeleka
kwa watu wanaoitwa maprodyusa, hao kazi yao ni kuwatafutia midundo
iliyotengenezwa kwenye kompyuta na kuichanganya na mashairi yao, baadaye
unakuwa muziki wa kizazi kipya!
Kusema ukweli hapo hakuna
muziki, ni makelele tu. Sababu muziki unatengenezwa na ala za muziki na si
vinginevyo. Au kama ni hivyo basi kompyuta ndiyo tunaweza kuiita mwanamuziki
kwa vile ndiyo inayotoa midundo hiyo. Lakini sio yule aliyepeleka mashairi yake
ili akatafutiwe midundo.
Isipokuwa midundo hiyo kuiita
muziki ni kwakuwa muziki wenyewe unaelekea kutoweka siku hizi. Kwahiyo kwa
kujifariji ili iendelee kuonekana muziki bado upo ndipo yanapotajwa mambo kama ya muziki wa kizazi kipya. Ni kujifariji tu.
Mtu anayeshiriki kutengeneza
muziki, hata kama ni mwimbaji tu asiyejua kucheza chombo chochote cha muziki kama gitaa, kupuliza saksafoni, ngoma nakadhalika, anaitwa mwanamuziki sababu ana utaalamu wa
kupanga sauti ya maneno ya wimbo ili yaendane na midundo ya muziki.
Kituko ni pale mtunzi wa
mashairi asiyejua hata sauti inayofaa kuimbia mashairi yake mpaka atafutiwe na prodyusa,
mbali na kutoweza kupiga chombo chochote cha muziki, eti naye anataka aitwe
mwanamuziki! Kwa muziki gani?
Nashangaa vijana wengi kwa
sasa wanaoimba nyimbo zinazoitwa muziki wa kizazi kipya wanaitwa wanamuziki!
Sielewi ni kitu gani kinachofanya waitwe wanamuziki wakati kusema ukweli kwenye
nyimbo zao, au niyaite mashairi yao,
hakuna muziki wowote unaochezwa mle. Kwa nini tunalazimika kulidhalilisha neno
muziki?
Kinachoonyesha kwamba
wanachokifanya vijana hawa wa siku hizi ni tofauti kabisa na muziki, ni pale
wanapoitwa kupiga muziki wa moja kwa moja “live concert”. Badala ya kujiandaa
na vyombo vya muziki wao wanatayarisha vyombo vya disco, muziki wa kunukuu
ambao mara nyingi unakuwa umerekodiwa kwenye vyombo viitwavyo CD siku hizi, mpaka wanamuweka na DJ!
Wakati wa kuimba mwimbaji
anasema awekewe CD fulani naye kuanza kufanya maigizo kama
anaimba vile kumbe sauti inayosikika inatoka kwenye CD kwa mtindo huitwao “play
back”. Kweli hapo kuna live concert?
Kwakeli tunapaswa
kutofautisha muziki na kelele, kwa maana sio kila kelele tuzisikiazo ni muziki.
Vinginevyo kwa mtindo huo hata mingurumo ya radi wakati wa mvua itabidi
tuicheze kwa kujiridhisha kuwa ni muziki wa asili tuliotengenezewa na Mungu.
Hata mingurumo ya mabomu
yaliyojilipua Mbagala na Gongolamboto tungeicheza kwa kuamini kuwa ni
muziki. Kama sio hivyo basi tuelewe kwamba muziki na kelele ni
vitu viwili tofauti.
Kinachofanyika kwa wakati huu
na kupewa jina la muziki wa kizazi kipya kwa kiasi kikubwa ni makelele. Hilo jina la kizazi kipya
ni la kujifariji kutokana na kutokuwepo kwa muziki wenyewe. Huwezi kuwa na
muziki hai bila vyombo vya muziki.
Kuna usemi katika lugha ya
Kihaya usemao kwamba “obworo bushomba obumaza” ukiwa na maana ya kwamba ukosefu
wa kitu, umasikini, hushawishi ujasiri. Ndio kama ujasiri huo wa kudai makelele
yanayofanywa na fijana kwa sasa ni muziki wa kizazi kipya! Tutafanyaje kama
muziki haupo?
Na tatizo hili naona halipo
tu hapa kwetu, limetamalaki hata kwenye nchi nyingine. Ndiyo maana nimesikia
kijana mmoja wa Kitanzania anayejulikana kama
Diamond akipewa tuzo kedekede za kimataifa eti ni mwanamuziki bora wakati hana
uwezo wowote wa kupiga muziki isipokuwa kuimba tu mashairi.
Kama tuzo hizo alizopewa
zisingehusishwa na muziki ningempongeza sana
Diamond, lakini kwa sasa inaniwia vigumu kumpongeza kwa kitu ninachoamini
kwamba hakijui hata kidogo. Kweli “obworo bushomba obumaza”. Lakini mimi sitaki
tufike huko.
Tuwashauri vijana wa kisasa
wajifunze kupiga muziki kama wanahitaji kuitwa
wanamuziki kusudi tunapowakaribisha kupiga muziki hai, “live concert” watupigie
muziki wa kweli unaotoka kwenye ala za muziki na sio kutuwekea CD zinazotoa
sauti zilizotengenezewa kwenye kompyuta huku wenyewe wakifanya maigizo wakati
hawaimbi.
Ningewashauri vijana hawa wa
kinachoitwa Bongo Fleva wakajifunze muziki kwa kijana aitwaye Banana Zorro au
kwa Judith Wambura (Lady Jaydee) namna ya kupiga muziki na kuacha kutuzuga na
makelele wakidai ni muziki wa kizazi kipya au Bongo Fleva.
Hebu tulipe neno muziki hadhi
yake kwa kuucheza muziki wenyewe na kuacha kufanya vituko kutokana na kuishiwa.
0784 989 512