BODI MPYA YA KCU (1990) LTD INAWEZA KUUFUFUA AU KUUZIKA USHIRIKA
NA PRUDENCE KARUGENDO
PAMOJA na wakulima wa kahawa mkoani Kagera kuufurahia
uamuzi wa kuisimamisha kazi Bodi ya Wakurugenzi ya zamani ya chama kikuu cha
ushirika cha KCU (1990) Ltd., bado yapo mambo yanayowatia wasiwasi wakulima hao
wa kahawa na kuwafanya wahisi kwamba Bodi mpya iliyochaguliwa siku chache
zilizopita inaweza isifanye kazi zake kwa usahihi kutokana na kuathiriwa na
kinachoonekana kama vidudu nyemelezi toka kwenye Bodi iliyotangulia.
Wakulima hao wanakuwa na
mtazamo huo katika sehemu mbili tofauti. Sehemu ya kwanza inaonyesha kwamba
uamuzi wa kuisimamisha Bodi ya zamani, pamoja na kuonekana ni uamuzi mzuri,
lakini eti ulicheleweshwa sana
kiasi cha kuifanya Bodi hiyo kusambaza virusi vyake ambavyo vimeleta madhara
makubwa na kuifanya kazi ya kuyasafisha madhara hayo iwe ngumu.
Inasemwa kwamba ugumu wa
kuyasafisha madhara yaliyoachwa na Bodi iliyotangulia uko namna hii; Bodi hiyo
ilisimamia uchaguzi wa vyama vya msingi vinavyounda chama kikuu cha KCU (1990)
Ltd.. Usimamizi huo ulikuwa wa mizengwe mitupu ambapo Bodi hiyo ya zamani ya
chama kikuu ilikuwa inahakikisha wanapatikana wawakilishi na wajumbe wa Bodi za
vyama vya msingi ambao walikuwa wanaelewana na wajumbe wa Bodi ya chama kikuu
ambao wangeweza kushirikiana kukihujumu chama hicho bila ya kupigiwa makelele
yoyote.
Inasemekana hayo yalifanyika
kwa imani kwamba wakurugenzi wa Bodi ya chama kikuu pengine wangeendelea kuwa
walewale waliokuwa wakilalamikiwa na wanaushirika muda wote. Kwahiyo mizengwe
iliyofanyika mpaka wakapatikana wawakilishi hao wa vyama vya msingi ilikuwa imelenga kujihami
dhidi ya wanaushirika waliokuwa wakihoji juu ya mwenendo usioeleweka wa
wakurugenzi wa Bodi ya chama kikuu.
Kwahiyo kusimamishwa, au
niseme kuzuiwa kugombea tena, kwa wakurugenzi wa zamani, ni kitu
kilichojitokeza bila kutegemewa na yeyote. Hivyo Bodi mpya ya wakurugenzi wa
KCU (1990) Ltd., ambayo bilashaka haikutegemewa, haiwezi kufanya kazi zake
kiusahihi kwa kushirikiana na wakurugenzi wa Bodi za vyama vya msingi ambao
walikuwa tayari kufanya kazi na Bodi iliyosimamishwa. Pia wawakilishi wa vyama
vya msingi ambao walichaguliwa kwa malengo ya kuibeba Bodi iliyopita watajikuta
wanashindwa kufanya kazi barabara na Bodi mpya.
Bodi mpya, hata kama itakuwa imekusudia kufanya mambo mazuri ya
kuusimamia uongozi wa KCU (1990) Ltd. inaweza ikatatizwa na uwepo wa Bodi za
vyama vya msingi ambazo zimewekwa kwa manufaa ya Bodi iliyosimamishwa. Kwa
mantiki hiyo ingefaa Bodi zote za vyama vya msingi nazo zifumuliwe na kuundwa
upya, na ikiwezekana wajumbe wake wote waliokuwemo nao wazuiwe kugombea tena, kwa mtazamo uleule uliowafanya wajumbe wa Bodi
ya chama kikuu kuzuiwa kugombea tena.
Hiyo ndiyo ingeonekana ni
kuusafisha uchafu uliokuwa kwenye ushirika huo kwa maana halisi. Sababu
haiwezekani kuustawisha mmea kwa kuuangalia tu juu kwenye majani yake bila
kuuangalia kuanzia chini kwenye shina lake. Ushirika unaanzia kwenye vyama vya
msingi, hayo ndiyo mashina ya ushirika, sababu kule ndiko wanaushirika waliko
wanaolima mazao yanayoshughulikiwa na ushirika husika.
La pili wanalolisema
wanaushirika kuhusu Bodi mpya ni la uongozi wa chama hicho kikuu cha ushirika.
Wanasema kwamba tatizo lililokuwa kwenye Bodi iliyopita ni la kutokuelewa
majukumu yake. Wanasema kwamba Bodi ya wakurugenzi kazi yake kuu ni kuusimamia
uongozi na kuutolea maelekezo. Lakini eti kinyume chake uongozi wa KCU (1990)
Ltd. ndio uliokuwa ukiisimamia Bodi na kuielekeza ifanye nini!
Kwamba maamuzi mengi
yaliyoenda kinyume na kuufanya ushirika huo uonekane umeanza kutetereka
yalikuwa yanatolewa na uongozi na kuilazimisha Bodi kuyabariki. Kwa muonekano
huo Bodi haikuwa na maana yoyote, sababu yenyewe ipo kuusimamia uongozi,
“management”, na si kinyume chake.
Kwahiyo wanaushirika wanasema
kwamba ili Bodi mpya ionekane inaleta matumaini ingeanza kwa kuuondoa uongozi
uliokuwepo tangu wakati wa Bodi iliyondolewa kwa kushindwa kazi. Hiyo ingeleta
maana ya kwamba Bodi iliyoondolewa haikuonewa, na zaidi kuonyesha kwamba hii
iliyowekwa sasa imeingia kuboresha kwa kuparekebisha pale ambapo paliishinda
Bodi iliyoondolewa.
Taarifa zinazotoka kwenye
uongozi wa chama hicho cha ushirika zinaonyesha kwamba kwa sasa chama hicho
kinaendeshwa na kitengo chake kimoja cha Moshi Export. Mishahara na mambo
mengine yote yanategemewa kupatikana toka Moshi Export.
Kitengo cha Moshi Export
kilianzishwa kama idara inayojitegemea kwa
lengo la kuitafutia soko, hasa soko la nje,
kahawa inayolimwa Bukoba na maeneo jirani. Lakini hakikuanzishwa kwa
ajili ya kuuendesha ushirika kama kinavyofanya
kwa sasa.
Kwa mantiki hiyo, baadhi ya
wafanyakazi ndani ya uongozi wa KCU (1990) Ltd. wanauliza kwamba kama chama kinajiendesha kwa kukitegemea kitengo chake
kimoja tu kilichoko Moshi, inawezekanaje meneja mkuu abaki yuleyule aliyeko
Bukoba wakati ikionekana hana lolote la kufanya zaidi ya kumtegemea mkuu wa
kitengo cha Moshi Export amalize kila kitu?
Wanasema kwamba kwa sasa
kitengo hicho cha Moshi karibu kinafilisika kutokana na kuwa na majukumu
yaliyokizi uwezo kwa vile hayakuwa malengo yake tangu kilipoanzishwa.
Hapohapo ndipo linajitokeza
swali la kwa nini watumishi wakuu wa KCU (1990) Ltd. kama
meneja mkuu, meneja wa fedha, mhasibu mkuu na wengineo waendelee kunufaika na
vyeo vyao pasipokufanya lolote lenye tija kwa ushirika lililowafanya wakapewa
utumishi huo? Eti kwa nini kisiachwe kitengo cha Moshi tu ndicho kikabaki
kinauendesha ushirika huo kuliko kuendelea kupata maelekezo toka Bukoba ambako
kumebaki mahali pa matumizi tu pasipozalisha kitu?
Hiyo ndiyo changamoto
inayoikabili Bodi mpya ya wakurugenzi ya KCU (1990) Ltd., inatakiwa iliangalie hilo na kujipambanua na
Bodi iliyoondolewa kwa kushindwa kazi. Kwahiyo kwa kutaka kuonyesha kuwa kazi
iliyopewa inaiweza Bodi mpya inapaswa iyafanye yaliyoishinda Bodi iliyopita.
Kama alivyosema mmoja wa wajumbe wa Bodi mpya, Bodi hii
ina mawili, ama kuufufua ushirika wa KCU (1990) Ltd. au kuuzika moja kwa moja.
Kila la heri Bodi mpya.