Bukobawadau

CCM HAITAKI MGOMBEA WA KUSAFISHA KWA DODOKI

Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amesema chama hicho hakitampitisha mgombea urais asiye na sifa na kuhangaika kumsafisha kwa dodoki ili atakate.
Amesema chama hicho kimeweka mfumo mzuri wa kupata mgombea mwenye sifa, msafi na salama ambaye kazi kubwa itakayokuwapo kwa CCM ni kumwombea kura tu na si kumsafisha.
Alisema CCM ina utaratibu imara ambao utatoa mgombea bora, huku akisisitiza kuwa utawashangaza wengi pale atakapopitishwa mgombea ambaye hakutarajiwa na wengi.
“Mwaka 1995 Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema ‘msinipe mgombea ambaye nikisimama naanza kumsafisha kwanza.’ Tutatafuta mgombea wa kumuombea kura,” Nape alisema jana wakati akizungumza na wahariri wa Magazeti ya Mwananchi na The Citizen alipotembelea ofisi za Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata Relini.
Kauli hiyo ya Nape imekuja siku chake baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete kuwataka wenye sifa kujitokeza kuchukua fomu huku akisema: “Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu wa kupata rais wa awamu ya tano, utakuwa wa kihistoria.”
Nape alisema chama hicho kitatumia misingi yake ya asili ambayo itatoa mgombea ambaye hatatiliwa shaka na kusisitiza kwamba hakitayumbishwa na kelele za barabarani.
Alisema hata wale wanaotabiri kwamba majina (ya wagombea), yakikatwa wataondoka na chama kitapasuka, hawatafanikiwa... “hata kama mtu ataondoka yeye, mkewe na watoto bado CCM itabaki imara.  “Utaratibu wa CCM katika uteuzi haujawahi kuwa na ushawishi wala sababu kutoka nje ya mfumo wenyewe. Kelele na ushabiki ni mambo tu ya barabarani,” alisema.
Akitolea mfano utaratibu uliotumika kupata mgombea urais wa chama hicho mwaka 1995, 2000 na 2010 alisema, “Mwaka 1995 magazeti mengi, yaliandika ‘eti Mkapa (Rais wa Awamu ya Tatu) naye achukua fomu’. Kwenye orodha ya magazeti Mkapa aliwekwa kama mtu wa nane, lakini akawa ndiye mgombea wa CCM na akashinda.”
Alisema mwaka 2000 visiwani Zanzibar, Makamu wa Rais Dk Mohammed Gharib Bilal alipigiwa kura 45 huku Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Karume akipata kura tisa, lakini baada ya majina yao kupelekwa katika vikao vya juu vya chama, Karume alipitishwa kugombea na akashinda.
“Mwaka 2010 watu wengi waliamini kuwa Dk Bilal hana mpinzani, lakini dakika za mwisho alipitishwa Dk Ali Mohammed Shein kuwa mgombea urais wa Zanzibar na akashinda,” alisema.
Alisema mifano hiyo inaonyesha kwamba taratibu ndani ya chama hicho haziyumbi wala kuyumbishwa na matukio mengine yaliyopo nje ya mfumo ambao kimejiwekea.
“CCM ni chama imara kina katiba, sheria, kanuni, taratibu na tamaduni zake. Bado tutaweza na tunaweza kutoa mgombea mzuri, mwenye sifa, mwadilifu na anayeweza kuwa rais na Mwenyekiti wa CCM,” alisema.
 Akiwazungumzia wagombea wanaoungwa mkono na wanachama wa CCM alisema: “Leo nakuunga mkono kwa sababu nautaka uwaziri. Sasa ukitoka kutaka kuhama chama, nitakuwa na uhakika gani kama tukienda wote nitapata ninachokitaka? Wanakwenda na wewe na ukifika mahali umepigwa wanasema siyo riziki wanageukia kwingine.”
Alisema hivi sasa joto katika la uchaguzi limeanza kupanda nchini na kuvitaka vyombo vya habari kutumia weledi katika kuhakikisha nchi inavuka salama katika mchakato huo.
“Joto limeanza ndani ya CCM na nje ya CCM. Lakini joto la ndani ya CCM ni kubwa zaidi kwa sababu inawezekana kabisa kwamba mgombea atakayepitishwa ndiye atakayekuwa Rais wa nchi hii.”
Hadi sasa makada kadhaa wa CCM wamejitokeza na kutangaza nia kuwania nafasi hiyo ya juu kabisa ya uongozi wa nchi huku wengine wakitajwa kujiandaa kuchukua fomu mchakato huo utakapotangazwa rasmi na chama.
Waliokwishatangaza ni Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, January Makamba; Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla; Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Wanaotajwa ni Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba; Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Wengine ni Spika wa Bunge, Anne Makinda; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha - Rose Migiro; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira.
Nape na ubunge
Akizungumzia kugombea ubunge katika Jimbo la Ubungo kama alivyofanya mwaka 2010, Nape alisema: “Sijaoteshwa (kicheko). Lakini hata kama nitaamua kugombea si katika Jimbo la Ubungo. Hata hivyo, mimi na Kinana tumeamua kufanya kazi ya kutengeneza mtumbwi ambao baadaye watu watautumia kuvuka.
“Kwa sasa tunachokifanya ni kuweka akili zetu zote kutengeneza mtumbwi huo, ukitoboa tuuzibe na kuufanyia ukarabati. Kazi yetu zaidi ni urefa na kama nikiamua kucheza mpira ni lazima nivue magwanda ya urefa ili nicheze mpira.”
Mwaka 2010, Nape aligombea ubunge katika Jimbo la Ubungo lakini alishindwa katika kura ya maoni na Hawa Ng’umbi ambaye alishindwa katika uchaguzi huo na John Mnyika wa Chadema.
MWANANCHI
Next Post Previous Post
Bukobawadau