GHALA PEKEE NCHINI LA KUHIFADHI VITUNGUU SAUMU
Sehemu ya Ghala la kuhifadhi vitunguu Saumu liliojengwa na MIVARF, lipo Mkoani Manyara Wilayani Mbulu, kijijini Bashay. Ghala hilo lina uwezo wa kuhifadhi tani 50 za vitunguu Saumu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
MIVARF yaboresha soko la Vitunguu Saumu
Mbulu.
Na.
Ibrahim Hamidu
Programu
ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini
(MIVARF) imeboresha Soko la Vitunguu Saumu kwa kujenga ghala la kuhifadhi
vitunguu mkoani Manyara, wilayani Mbulu
katika kijiji cha Bashay.
Ghala
hilo lenye uwezo wa kuhifadhi tani 50 za vitunguu, limegharimu Jumla ya
shilingi milioni 88 ikiwa MIVARF
imechangia asilimia 95 ya fedha hizo na Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu
imechangia asilimia 5 ya fedha hizo.
Akiongea
na timu ya wataalam kutoka MIVARF
ofisini kwake hivi karibuni wakati timu hiyo ilipokuwa ikikagua
utekelezaji wa shughuli za Mradi huo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya
ya Mbulu Bw. Nicholaus Haraba, alifafanua kuwa ujenzi wa ghala hilo umeongeza
mnyororo wa thamani wa zao la vitunguu Wilayani Mbulu.
“Tunaushukuru
Mradi wa MIVRAF kwa ujenzi wa ghala hili la kuhifadhi vitunguu ambalo ni ghala
pekee kwa hapa nchini lenye viwango sitahiki na uwezo wa kuhifadhi
tani nyingi za vitunguu. Kwa mantiki hiyo ghala hili limewawezesha
wakulima wa zao hilo kuongeza thamani ya mazao yao ambayo awali yalikuwa
yanapotelea shambani kwa kukosa eneo la kuyahifadhi ” alisema Haraba.
Haraba
alieleza kuwa, kupitia MIVRAF wananchi wa Mbulu wamepata mafunzo ya jinsi ya
kufungasha mazao yao pamoja na kuwezeshwa vifungashio vya vitunguu hali ambayo
imelijengea ubora zao hilo katika soko.
“Wananchi
awali walikuwa wanauza mazao yao huko mashambani, katika mabeseni na lumbesa
lakini baada ya mafunzo ya MIVARF ya jinsi
ya uhifadhi wa mazao yao hivi sasa wananchi wanauza vitunguu kwa vipimo kwa
kutumia vifungashio maalum hii inamfanya
mkulima kunufaika na mauzo hayo” alisisitiza Haraba
Aliongeza
kuwa, katika kuhakikisha Soko la Vitunguu linakuwa imara Wilayani Mbulu, MIVARF
imejenga barabara kwa kiwango cha
Changarawe kutoka Bashay, Diyomat, Dirima hadi Muslur yenye Urefu wa km 25 kwa
gharama ya shilingi milioni 789 ikiwa asilimia 95 ya fedha zilizotolewa na
MIVRAF na asilimia 5 zimetoka katika Halmashauri ya Mbulu. “Ujenzi wa barabara hii
pia utasaidia kwa wafanyabiashara kusafirisha kwa usalama mazao hayo baada ya
kuyanunua kutoka Mbulu” alisisitiza Haraba
Katika
kuunga juhudi za MIVARF za kuboresha Soko la Vitunguu tayari Halmashauri ya Wilayani
Mbulu katika bajeti yake ya mwaka 2015/2016 imetenga kiasi cha shilingi milioni
18 kwa ajili ya ununuzi wa mashine ya kusindika vitunguu ili wafanyabiashara
wanunue vitunguu ambavyo tayari vimesindikwa na tayari kumuuzia mtumiaji wa
mazao hayo.
“Tunategemea
MIVARF iendelee kuliboresha soko hili la vitunguu na jukumu letu nikuchangia
kwa kile tunachowezeshwa na MIVARF hivyo tumeamua kutenga fedha katika bajeti
ya mwaka ujao ili tutakapowezeshwa kununua mashine ya kusindika vitunguu tuwe
tayari kwa ajili ya ununuzi wa mashine yetu” alisema Haraba
Akiongea
na Wataalamu wa MIVRAF katika ghala la kuhifadhi Vitunguu la Bashay Wilayani
Mbulu, Mkulima wa zao hilo, Bi. Wema Edward alibainisha kuwa Mradi wa MIVRAF
umeliboresha soko la vitunguu wilayani humo kwa kuongeza mnyororo wa thamani wa
zao hilo.
“Kutokana
na uhifadhi bora wa vitunguu na vifungashio bora hivi sasa tunauza kilo ya
vitunguu kati ya shilingi elfu 3,000/= hadi
elfu 4, 000/= , wakati awali tulipokuwa
tunatumia mabeseni kuhifadhi mazao yetu tulikuwa tunauza kilo kwa shilingi elfu
1,500/=. ” alisema Wema.
Mradi
wa MIVRAF ambao unahudumia wananchi 4,800 wilayani Mbulu ulianza kutekelezwa
katika wilaya hiyo kuanzia mwaka 2013, katika kata tatu za Wilaya hiyo, kwa
kuongeza thamani mazao na ujenzi wa miundo mbinu ya masoko.
Programu
ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini
(MIVARF) ni Programu iliyobuniwa na Serikali Tanzania ikishirikana na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Benki
ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na Taasisi ya Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA).
Programu hii ni ya miaka saba inayotekelezwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara
na Zanzibar. Utekelezaji wake ulianza
rasmi mwezi Julai 2011.
Mwisho.