Bukobawadau

HABARI KUBWA SIKU YA LEO FEB 25,2015

Baraza la maadili ya utumishi wa umma limeshindwa kumuhoji mbunge wa Bariadi Magharibu Mh Chenge.
Baraza la maadili ya utumishi wa umma limeshindwa kumuhoji mbunge wa Bariadi Magharibu Mh Endrew Chenge baada kuwasilisha zuio la mahakama kuu lililozua kutokuendelea kujadili miamala ya Escrow huku wanasheria wa sekretarieti ya baraza hilo wakipingana naye kwa madai kuwa wao wanajadili ukiukwaji wa maadili na siyo miamala ya Escrow.
Kufuatia hali hiyo mwenyekiti wa baraza hilo jaji mstaafu Hamisi Msumi ameahirisha kikao hicho hadi Feb 26 mwaka huu ili wajumbe wapate muda wa kupitia zuio hilo ambapo baraza litakuja na uamuzi ama wa kuendelea au kusitisha hadi pale mahakama itakapotoa uamuzi wa sakata hilo.
Akisoma hati ya malalamiko dhidi ya Chenge, mwanasheria wa sekretarieti ya maadili, Hassan Mayunga amesema mlalamikiwa amekiuka maadili ya viongozi wa umma ambapo akiwa mwanasheria mkuu wa serikali AG mwaka 1995 aliishauri serikali kuingia mkataba wa miaka 20 na kampuni ya Independent Power Solution Limited IPTL wa kuongeza uzalishaji wa umme.

Aidha ameongeza kuwa wakati anafanya hayo hakuweka wazi kuwa ana maslahi binafsi na baada ya kustaafu wadhifa huo Desemba 2005 aliingia mkataba wa kuwa mshauri mwelekei wa kampuni ya Vip Engineering and Marketing Limited iliyokuwa na hisa asilimia 30 kwenye kampuni ya IPTL kitendo ambacho ni ukiukwaji wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma ambalo linamzuia kiongozi wa umma kujinufaisha na utumishi wake uliopita.

Akitetea hoja yake ya kutaka baraza hilo lisitishe zoezi la kumuhoji Mh Chenge amesema malalamiko dhidi yake ni chimbuko la uamuzi wa bunge na kutaka apewe mwongozo wa suala hilo kuendelea kujadiliwa wakati mahakama kuu imeshazuia huku akilitaka baraza hilo kutokuingia kwenye misukumu ya kisiasa badala yake wafuate sheria za nchi na kukabidhi hati hiyo kwa mwenyekiti wa baraza.

Hata hivyo mara baada ya kutoka nje ya ukumbi waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari walipotaka kufanya naye mahojiano juu ya suala hilo Mh Chenge majibu yake yalikuwa hivi.
Mwenyekiti wa baraza hilo jaji mstaafu Hamisi Msumi akizungumza mara baada ya kuahirisha zoezi hilo amesema amelazimika kufanya hivyo ili wapate fursa ya kupitia zui hilo ili kila upande uweze kupata haki.

Kwa upande wa wanasheria wa sekretarieti ya baraza hilo wamepinga hoja alizotoa mh chenge na kudai kuwa wao walipitia zuio hilo na kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kumuta na awali walishafanya naye mahojiano lakini hakutoa hoja hizo.

 Katuni ya leo inahusu mbio za urais 2015
 Waziri mkuu mh. Pinda aziagiza halmashauri kuacha siasa katika ujenzi wa maabara.
Waziri mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda amezitaka halmashauri zote nchini kuacha siasa katika suala la ujenzi wa maabara kwenye shule za sekondari na badala yake waongeze nguvu na kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kabla ya mwezi juni mwaka huu ili wanafunzi waanze kujifunza masomo ya sayansi kwa vitendo.
Waziri mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi katika shule ya sekondari Songwe wilayani Mbeya ambako pia ametembelea na kukagua vyumba vitatu vya maabara ambavyo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100.

Katika hatua nyingine Pinda ametemebelea na kuweka jiwe la msingi katika soko la kimataifa la Mwanjelwa jijini Mbeya ambako pia ameagiza ujenzi wa soko hilo ambao umechukua zaidi ya miaka mitano sasa, kuhakikisha unakamilika na wananchi wanaanza kulitumia kabla ya mwezi juni mwaka huu huku akitaka wafanyabiashara waliokuwepo wakati soko hilo likiungua mwaka 2006 kupewa kwanza sehemu ya kufanyia biashara zao kabla ya watu wengine.

Meya wa jiji la Mbeya amesema kuwa ujenzi wa soko hilo umechelewa kukamilika kutokana na mkandarasi wa kwanza kufungua kesi mahakamani wakati akiondolewa, huku umkurugenzi wa jiji la Mbeya, Mussa Zungiza akidai kuwa ujenzi wa soko hilo la kisasa umezingatia tahadhari ya moto ili kuepusha matukio ya masoko kuungua moto ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara jijini Mbeya.
Ujenzi wa soko la mwanjelwa ulianza mwaka 2009 na ulitarajiwa kukamilika mwaka 2013 lakini haukukamilika na sasa unatarajiwa kukamilika aprili 30, mwaka huu.CHANZO ITV.
 UKAWA umeitaka serikali kusitisha zoezi la upigaji wa kura ya maoni ya katiba kutokana na kutokidhi vigezo vya kisheria.
Viongozi wa vyama vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi UKAWA umeitaka serikali kusitisha zoezi la upigaji wa kura ya maoni ya katiba kutokana na zoezi hilo kutokidhi vigezo vya kisheria na badala yake ielekeze nguvu na rasilimali fedha katika zoezi la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ili kuliepusha taifa kuingia katika machafuko.
Viongozi wakuu wa vyama vinavyounda umoja huo wa katiba ya wananchi ukawa wakiongozwa na Profesa Ibrahinmu Lipumba wa chamacha wananchi CUF na Freeman Mbowe wa chama cha demokrasia na maendeleoChadema na chama cha NLD Dr Emmanuel Makaidi na chama cha NCCR mageuzi Mosena Nyambabe wameitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari.

Mwenyekiti wa CUF Prof Ibrahimu Lipumba amemtaka rais Prof Jakaya Mrisho Kikwete kutoa kauli ya kuusitisha mchakato wa kura za maoni ya katiba pendekezwa kwa kuwa zoezi hilo kwa sasa haliwezi kutekelezeka April 30 ya mwaka huu kama rais alivyotangaza licha ya kutokuwa na mamlaka ya kutangaza tarehe ya kufanyika kwa kura hizo za maoni.

Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo Chadema Freeman Mbowe ameitaka serikali kuelekeza fedha kidogo zilizopo katika zoezi la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa kuwa zoezi hilo linakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kutosha na kusitisha kabisa zoezi la kura za maoni ya katiba ili kuiepusha nchi na kile alichodai kuwa ni machafuko yanayowea kuzuilika.
Bukobawadau

Hivi sasa taifa liko katika maandalizi ya kushiriki katika zoezi la kura za maoni ya katiba pendekezwa linalotarajiwa kufanyika alhamis ya April 30, 2015 kama ilivyotangazwa na mh rais wa jamhuri ya mungano wa Tanzania licha ya uwepo wa kauli za kulipinga zoezi hilo kutoka hasa katika vyama vya siasa vya upinzania na baadhi ya vyama vya kiraia kwa sababu kadha wa kadha.
 Katuni ya Masoud Kipanya leo Feb 25,2015
 Taarifa kutoka katika gazeti la Mwananchi :Lowassa, Membe yametimia

Dar es Salaam. Kamati Kuu ya CCM (CC) inakutana Jumamosi wiki hii huku mambo muhimu sita yakitarajiwa kujadiliwa, likiwamo suala la makada wa chama hicho waliopewa adhabu ya onyo kali kwa kuanza kampeni za urais mapema na ukiukaji wa maadili.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, licha ya kutoeleza ajenda za kikao hicho, ilisema kitafanyika jijini Dar es Salaam na kuongozwa na mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete kuanzia saa 4 asubuhi.
Kikao hicho kinafanyika wakati upepo wa kisiasa ndani ya chama hicho ukiwa haujatulia huku kukiwapo masuala mazito ya kitaifa yanayotikisa medani za kisiasa, likiwamo suala la uandikishaji wapiga kura, maandalizi ya kura ya maoni za kupitisha Katiba Inayopendekezwa na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, ambayo yameelezwa na wachambuzi wa siasa kuwa hayawezi kukwepeka katika kikao hicho.
Adhabu kwa wagombea
Itakumbukwa kuwa kikao hicho kitafanyika ikiwa ni siku 10 baada ya kukamilika tarehe ya mwisho ya adhabu kwa makada sita wa CCM, waliokuwa wakitumikia adhabu ya miezi 12 kwa ukiukwaji wa maadili kwenye mchakato wa kutaka kuteuliwa na CCM kugombea urais.
Kikao kilichopita cha CC kilichoketi Januari 13, mwaka huu kilibainisha kuwa baada ya muda wa adhabu zao kuisha, Kamati Kuu ingefanya tathimini kuona iwapo wagombea hao walizingatia masharti ya adhabu zao na endapo kungekuwa na ambao hawakuzingatia masharti  adhabu zao zingeongezwa.
Wiki iliyopita, Nnauye alithibitisha kuwa muda wa adhabu hiyo ulikuwa ukingoni na kuwa viongozi hao wangefanyiwa tathmini na kamati ndogo ya maadili ili kubaini iwapo adhabu hiyo ilitekelezwa ipasavyo.
Makada waliokuwa wakitumikia adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Waziri wa Kilimo na Ushirika, Stephen Wasira na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Kikao hicho huenda pia kikazungumzia mwenendo wa uandikishaji wa wapiga kura katika Daftari la Kudumu kwa kutumia teknolojia ya alama za vidole (BVR), iliyozinduliwa jana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
CCM, ni miongoni mwa vyama vya siasa nchini vinavyoungana na vyama vinavyounda Umoja ya Katiba ya Wananchi (Ukawa), kuhoji mara kwa mara ufanisi wa mfumo wa BVR katika kuandikisha wapigakura kutokana na historia yake isiyoridhisha.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, Dk Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema anaamini CC itajadili pamoja na mambo mengine, matokeo ya Kamati ya ndogo ya maadili inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Philip Mangula, iliyojadili suala la wagombea na kashfa ya Tegeta Escrow.
Dk Bana alitolea mfano suala la kashfa ya ufisadi katika Akaunti ya Escrow kuwa ni suala mbalo CCM wanaweza wakaamua kulibeba kama hoja na kuyapeleka kwa ajili ya kujadiliwa na kikao hicho kikubwa cha chama.
“Hili suala la ufisadi wa Tegeta Escrow ni ‘critical issue’, ni muhimu kwa chama chao kulijadili na kuja na majibu ya maswali yanayowasumbua wananchi wengi, hasa ukizingatia kuwa suala hilo lilikitikisa sana chama hicho,” alisema Dk Bana.
Alisema jambo lingine linaloweza kuchukuliwa kama ajenda katika kikao hicho na kuamua kulijadili ni wale wanachama wake waliojitangaza kugombea urais na ambao waliopewa adhabu ya mwaka mmoja ambapo anasema wanaweza kutaka kufanya mapitio, kama walitekeleza maagizo
“Vile vile wanaweza kuangalia kalenda ya uchaguzi ya chama chao na wajadili na kupendekeza utaratibu wa jinsi ya kuwapata wagombea wao…vile vile lipo suala la hali ya siasa nchini, hali imebadilika, upepo hauvumi kuelekea CCM,” alisema.
Aliongeza kuwa masuala mengine wanayoweza kujadili ni matukio ya kutisha na yasiyo ya kawaida yanayojitokeza nchini kama vile matukio ya kutekwa kwa watu na kuteswa, kuibuka kwa panya road na mengine yanayofanana na hayo ambayo anasema ni ukweli ulio wazi kuwa matukio hayo yanaashiria kuvurugika kwa amani na utulivu wa nchi.
“Matukio mengi yasiyo ya kawaida yameibuka hivi karibuni, mfano suala la vijana wa JKT nao wanaandamana wanataka ajira, lakini kila mtu anajua kuwa wale vijana wanajulikana wanafundishwa kujenga nidhamu, sasa wanaandamana, kunaonekana lipo tatizo nchini. Yote haya hayaleti mwelekeo mwema kwa jamii,” alisema.
Aliongeza kuwa, “tuhuma nzito zinazowakabili wanachama wake wanajua madhara yake na wanajaribu kutaka kuyarekebisha ili kurejesha ushindi ambao kwa kweli unaonekana kuwaendea vibaya.  Haya yote yanaweza kuwasukuma kuitisha vikao nyeti kama hivi na kujadili mustakabali wa chama chao ili waendelee kupata ushindi wa kishindo.
Alisema kitu kingine muhimu ambacho hawawezi kukikwepa kukijadili ni pigo walilolipata katika chaguzi za serikali za mitaa, ambapo chama hicho kilionekana kupata anguko kubwa kuliko matarajio.
Mengine aliyosema yanawezwa yakawa ajenda katika kikao hicho ni pamoja na kura ya maoni ya Katiba iliyopangwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu, muda anaosema hata wana CCM wenyewe wanajua kuwa hautoshi.
Mhadhiri mwingine wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alisema kubwa ambalo CCM linalowahangaisha na ambalo kwa namna yoyote huenda likawa miongoni mwa ajenda katika kikao chao ni kuleta utulivu wa ndani ya chama na kumjua mwanaCCM atakayepeperusha bendera yao.
“Nadhani hata wale wanachama wake sita waliopewa adhabu bado hawajaelezewa kama adhabu zao zimekwisha.  Ingawa muda wa adhabu umekwisha, lakini hawajaelezwa hatma yao, kwa hiyo hili ni jambo muhimu ambalo hawawezi kuliacha.

Mbunda alisema jambo lingine muhimu kabisa ambalo huenda itapewa uzito ni hili la kumpata mgombea anayekubalika katika jamii na ambaye ataweza kupeperusha vyema bendera ya chama na kukubalika na makundi yote.
“CCM waliozoea kuwa hakuna sababu ya kuangalia ni mgombea gani anayekubalika na jamii kwa imani kuwa wakisimamisha yeyote atapita, hali ya sasa kwa namna yoyote lazima waweke mtu anayekubalika katika jamii na hii ni ajenda kubwa inayohitaji mjadala mpana.
“Na ile tabia ya kutengeneza mazingira fulani awepo na huyu asiyepo, lazima waichukulie kwa uangalifu,” alisema Mbunda.
Mbunda alisema jambo lingine ni suala la kura ya maoni ya Katiba, ambalo pia ni suala nyeti na muhimu kwa CCM na kuwa wanapaswa wajipange vyema endapo wanataka Katiba waliyoipendekeza ipite.
Imeandikwa na Nuzulack Dausen na Joyce Mmasi
Next Post Previous Post