RAIS KIKWETE AKABIDHIWA RASMI UENYEKITI WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI
Tanzania inaunga mkono kwa dhati Ushirikiano wa Kikanda na
muumini mkubwa wa Umoja wa Africa na Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC).
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema hayo jijini
Nairobi mara baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa EAC na Rais Uhuru
Kenyatta wa Kenya ambaye amekua mwenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa kipindi
cha mwaka mmoja uliopita
"Tunaamini kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki
iliyogawanyika, haitaweza kuchukua nafasi yake kamili na heshima
katika familia ya Mataifa ya Afrika na dunia kwa ujumla" Rais amesema
na kuongeza kuwa Tanzania inakua kuwa masoko yaliyogawanyika,
miundombinu hafifu baina ya nchi, havina nafasi katika dunia ya leo
wala ya baadaye.
Rais
Kikwete amesema na kumpongeza Rais Kenyatta kwa kusimamia
utekelezwaji wa maazimio na miradi ya pamoja ya Jumuiya wakati wa
kipindi chake cha uenyekiti na kuahidi kuwa Tanzania haitawaangusha
wana Afrika Mashariki katika kutekeleza azma yao ya pamoja ya
kuendeleza Jumuiya ambayo inaundwa na nchi za Burundi, Kenya, Rwanda,
Tanzania na Uganda.
Rais
Kikwete amesema katika utekelezaji wa ajenda ya EAC, biashara
imeongezeka kwa kiasi kikubwa na kwamba nchi zote wanachama zinayaona
matunda hayo.
Katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2013 biashara katika nchi za EAC
imeongezeka kutoka dola za kimarekani 3, 722.9 hadi dola 5,805.6
ambapo kati ya mwaka 2012 hadi 2013 kumekua na ongezeko la asilimia
6.
"Kama biashara isiyo rasmi ingerasimishwa, kwa hakika,
ongezeko hili la biashara lingekua juu zaidi ya hapa, hivyo imefikia
wakati muafaka kurasimisha biashara isiyo rasmi katika ushirikiano
wetu" Rais amesema na kuongeza kuwa " kwa njia hii serikali
zitakusanya kodi na hivyo kuna umuhimu wa kuelekeza nguvu katika
kusaidia biashara ndogo ndogo na zile zisizo rasmi kwa kuziwekea
mazingira mazuri".
Rais
Kikwete amerejea nyumbani mara baada ya mkutano huo ambao umehudhuriwa
na Marais wa nchi zote tano za Jumuiya na Rais Salva Kiir wa Sudan
Kusini ambaye amehudhuria kama mualikwa maalum katika kipindi hiki
ambapo mazungumzo ya awali ya kuijadili nchi yake kama inaweza kupata
uanachama katika EAC yanaendelea.
Rais Jakaya
Mrisho Kikwete na mwenyeji wao Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya pamoja na
Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Rais Paul Kagame wa Rwanda na Rais
Pierre Nkurunzinza wa Burundi wakizungumza chemba kabla ya kuingia
kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Kenyatta International
Convention Center(KICC)Nairobi,Kenya katika mkutano wa kawaida
wa 16 wa Wakuu wa nchi za Afrika Mashariki uliofanyika Ijumaa Februari
20, 2015
Rais Jakaya
Mrisho Kikwete na mwenyeji wao Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya pamoja na
Rais Paul Kagame wa Rwanda kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa
Kenyatta International Convention Center(KICC)Nairobi,Kenya
katika mkutano wa kawaida wa 16 wa Wakuu wa nchi za Afrika
Mashariki uliofanyika Ijumaa Februari 20,
2015
Rais Jakaya
Mrisho Kikwete, Naibu Rais wa Kenya, Mhe. William Rutto na maafisa
wengine wakiwa kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa
Kenyatta International Convention Center(KICC)Nairobi,Kenya
wakati wimbo wa Taifa wa Tanzania katika mkutano wa kawaida wa 16 wa
Wakuu wa nchi za Afrika Mashariki uliofanyika Ijumaa Februari 20,
2015
Kutoka kushoto ni
mgeni mwalikwa, Rais wa Sudani Kusini, Mhe Salva Kiir, Rais wa
Burundi, Mhe Pierre Nkurunziza, Rais Jakaya Mrisho
Kikwete(Tanzania),Rais Uhuru Kenyatta(Kenya)Rais Yoweri Museveni
(Uganda) Rais Paul Kagame (Rwanda) na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) Balozi Dk Richard Sezibera wakiwa kwenye ukumbi wa
mikutano kwenye mkutano wa kawaida wa 16 wa Wakuu wa nchi za
Afrika Mashariki
Rais Jakaya Mrisho
Kikwete(kushoto)akipokea bendera ya Afrika Mashariki(EAC)kutoka kwa
Rais wa Kenya,Uhuru Kenyatta ikiwa ni ishara ya kumkabidhi rasmi
Uenyekiti wa EAC kwenye mkutano wa kawaida wa 16 wa
Wakuu wa nchi za Afrika Mashariki uliofanyika leo Ijumaa Februari 20,
2015 katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini
Nairobi. Picha na IKULU