Bukobawadau

SIKU YA SHERIA TANZANIA YAADHIMISHWA MKOANI KAGERA KUUFUNGUA MWAKA MPYA WA SHERIA 2015

Waheshimiwa Majaji na Mkuu wa Mkoa Meza Kuu
Waheshimiwa Majaji na Mkuu wa Mkoa Meza Kuu
Afande Wekwe Kiongozi wa Gwaride
Gwaride la Jeshi la Polisi Likitoa Heshima kwa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba
Askofu Buberwa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi Akifungua kwa Maombi  Kuiombea Mahakama Kuu Tanzania
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Kagera Sheikh Haruna Kichwabuta akiongoza Dua ya ufunguzi. 
Siku ya Sheria Tanzania imeadhimishwa Mkoani Kagera katika viwanja vya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba na kuhudhuriwa na Majaji, Mahakimu, Mawakili, Wadau mbalimbali wa sheria na wananchi kutoka sehemu mbali mbali za mkoa wa Kagera.

Katika maadhimisho hayo ya kuufungua mwaka mpya wa sheria 2015 kauli mbiu ilikuwa ni Fursa ya kupata haki ni wajibu wa Serikali, Mahakama na Wadau. Aidha, katika maadhimisho hayo hotuba mbalimbali juu ya kupata haki na wajibu wa wadau katika kupata haki hizo zilitolewa.

Wakili wa Kujitegemea na   Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Kanda ya Bukoba Wakili Aron Kabunga alitoa mada juu ya wajibu wa Serikali katika kupata haki, kuwa Serikali inatakiwa kuondoa sheria Kandamizi zinazowafanya wananchi kutopata haki zao kwa wakati na stahili.

Wakili Kabunga pia alisistiza kuwa Serikali inatakiwa kupunguza viwango vikubwa vya kufungulia kesi kwa ajili ya kupata haki mfano katika Mabaraza ya Ardhi  kwani alisema suala hilo ni kandamizi na lina wanyima haki wananchi kupata haki zao za msngi.

Wakili Kabunga alisema Serikali inatakiwa kuacha kutunga sheria za kushughulikia  masuala yaliyopita mfano sheria ya uhujumu uchumi ya mwaka 1984 ambayo ilitungwa kushughulikia mambo ambayo yalitokea kabla ya sheria yenyewe kutungwa ambapo sheria hiyo inakuwa kandamizi kwani wakati makosa yanatendeka sheria husika inakuwa haipo.

Wakili Kabunga alimalizia kwa kuiomba Serikali kutekeleza wajibu wake kwa kuelimish wananchi kuheshimu utawala wa  sheria, kuhakikisha  maamuzi yanayotokana na Mahakama yanatekelezwa bila kuingilia mahakama kama mhimili ulio huru.

Naye Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba  Mhe. Sivangilwa Mwangesi  alisema katika hotuba yake kuwa Mahakama mwaka huu 2015  katika kutekeleza majukumu yake kipaumbele chake ni kushughulikia kesi zote zilizokaa muda mrefu na zenye mvuto wa kijamii ili kutoa haki kwa wahusika.

Jaji Mwangesi pia alisema kuwa wajibu wa wadau wa sheria kama Polisi si kuwafikisha watuhumiwa  mahakamani bali kuwa na ushahidi wa kutosha juu ya watuhumiwa hao. Aidha, Mawakili kuwashauri wateja wao pale wanapoona kesi zao hazina misingi bali kupoteza muda wa mahakama bila sababu. Pia wananchi kutoa ushirikiano pale wanapohitajika kutoa ushahidi mahakamani.

Mkuu wa Mkoa Kagera John Mongella akitoa salamu katika maadhimisho hayo alisema serikali mkoani Kagera itahakikisha inatimiza wajibu wake katika kuleta haki kwa wananchi. Aidha alizitaja changamoto kubwa katika mkoa wa Kagera kuwa ni Rushwa na wananchi kujichukulia sheria mkononi ambapo aliomba vyombo vyote vya ulinzi na usalaama pamoja na mahakama kushirikiana kupunguza  kupambana na changamoto hizo.
Next Post Previous Post
Bukobawadau