BODI YA PAROLE YA MKOA WA KAGERA YAZINDULIWA RAMSI KUSHUGHULIKIA WAFUNGWA WENYE MWENENDO MZURI MAGEREZANI
Bodi ya Parole ya Mkoa yazinduliwa
rasmi Mkoani Kagera na Mkuu wa mkoa Mheshimiwa John Mongella na kupelekea bodi
hiyo kukaa kikao chake cha kwanza cha kisheria Mrchi 26, 2015 baada ya kuteuliwa rasmi na
Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi ili kujadili wafungwa waliojirekebisha na
kuonesha tabia na mwenendo mzuri gerezani.
Parole ni utaratibu au mfumo wa
kumwachilia mfungwa kutoka gerezani baada ya kutumikia sehemu ya kifungo kwa
imani kwamba mfungwa huyo hatatenda kosa tena, na kwamba atafuata masharti.
Mfungwa huyo lazima awe ameonesha tabia njema na kujirekebisha kwa kipindi
chote alichokaa gerezani.
Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini
Katika uzinduzi huo wa Bodi ya
Parole ya Mkoa Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Magereza Mtiga H. Omary alisema wajumbe wanne na Mwenyekiti walioteuliwa
na Waziri wa Mambao ya Ndani watadumu katika nafasi hiyo kwa muda wa miaka
mitatu kuanzia na tarehe 26/12/2014 hadi tarehe 26/12/2017.
Kamishina Mtiga aliwataja
walioteuliwa na Waziri kuwa wajumbe wa Bodi ya Parole kuwa ni Askofu Methodius
Kilaini (Mwenyekiti), na wajumbe ni Alhaji Haluna Kichwabuta (Manispaa ya
Bukoba), Thepista Balagama (Biharamulo), Stella Ndyekobora (Karagwe) na Peter
Emmanuel Buhiye (Missenyi).
Kamishina Mtiga pia alibainisha
kuwa bodi za Parole za Mkoa wa Mkoa wa
Kagera zilizowahi kuwapo ni nne tangu mwaka
Juni 2003 aidha, bodi hizo kwa vipindi vya miaka mitatu mitatu ziliweza
kukaa vikao 35 na wafungwa 370 walijadiliwa katika vikao hivyo, wafungwa 229
waliweza kuachiliwa kwa mpango wa Parole na Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi
chini ya kifungu namba 6(4) cha sheria za Parole.
Akizindua Bodi hiyo ya Parole ya
Mkoa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. John Mongella aliwasistiza wajumbe kuzingatia
uadilifu, uaminifu, na umakini mkubwa katika utendaji wao wa kazi ili kutenda
haki kwa wafungwa wanaoonesha mwenendo mzuri wakiwa magerezani.
Mhe. John Mongella aliwakumbusha
wajumbe hao kutoshughulika na wafungwa ambao waliingia magerezani kwa makosa ya
kuua wenzao kikatili au wale wote wanaojihusisha na kuwaua watu wenye albinism,
ama kutowapendelea wafungwa ambao jamaa zao wana uwezo mkubwa wa kifedha na
walitenda makosa ambayo hayawaruhusu kutoka kwa sheria za Parole.
Mwenyekiti wa Bodi ya Parole ya
Mkoa wa Kagera Askofu Kilaini akitoa shukrani zake alisema atahakikisha yeye na
wajumbe wake wanatenda haki ili kulinda
usalama wa jamii kule wafungwa hao wanakotoka na kuachiwa kurudi kuishi ili
amani katika jamii isivurugike kwa kuisi kuwa mfungwa aliyeachiwa bado ni
jambazi.
Bodi ya Parole ya Mkoa inaundwa
na Mwenyekiti na wajumbe wanne wa kuteuliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani,
Mwanasheria Mfawidhi wa serikali katika Kanda husika, Afisa Mwandamizi toka
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mganga Mkuu wa Mkoa, Afisa Ustawi Mwandamizi Kutoka
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, na wengine wanaoingia kwa nyadhifa zao ni Kamanda wa
Polisi Mkoa na Mkuu wa Magereza wa Mkoa.
Changamoto kubwa inayoikumba Bodi
ya Mkoa ya Parole ni Wananchi kutokuwa na uelewa mzuri juu ya sheria ya Parole,
Sheria yenyewe kuacha wafungwa wengi ndani ya magereza, aidha jamii kuwa na
mtazamo hasi juu ya wafungwa wanaoachiwa, pia jeshi la magereza kutokuwa na
raslimali fedha kwenda vijijini kupata taarifa za wafungwa.