BUNGE LAPITISHA MUSWAADA WA SHERIA YA BAJETI YA MWAKA 2014
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo limepitisha muswada wa
sheria ya bajeti wa mwaka 2014 ambao unatajwa kuwa utakuwa suluhu ya
kudumu ya matumizi ya fedha za umma kwa nidhamu na kuliepusha taifa na
vitendo vya ubadhirifu vilivyoshamiri hapa nchini.
Akijibu hoja za wabunge mbalimbali kabla ya muswada huo kupitishwa
waziri wa fedha Mhe.Sada Mkuya amesema muswada huo utawabana pia baadhi
ya viongozi wa wizara wakiwemo mawaziri ambao wamekuwa na tabia ya
kushinikiza taasisi ambazo zipo chini ya wizara zao kuwapa fedha za
kuendesha wizara pindi bajeti ya wizara husika inapoisha kabla ya
wakati.
Naye Mbunge wa Jimbo la Pangani Salehe Pamba pamoja na yule wa
Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa wameitahadharisha Serikali kuangalia
pia utendaji kazi wa wafanyakazi wake sambamba na kudhibiti vitendo vya
rushwa ili kufanya muswada huo uweze kutimiza malengo yake.
Kwa upande wake Mbunge wa Mbozi Magharibi David Silinde amesema
Muswada huo utalisaidia kikamilifu Taifa la Tanzania kama pia
utawasilishwa pia katika baraza la wawakilishi ili kufanya pande zote
mbili za Muungano kunufaika nao.