DIAMOND PLATNUMZ NI KIOO CHA WASANII KATIKA JAMII YETU
NA PRUDENCE KARUGENDO
MKOA wa Kigoma ni hazina kubwa ya vipaji hapa
nchini Tanzania. Tangu zamani kulishuhudiwa vipaji vingi toka mkoani humo hasa
vya wanamichezo na wasanii. Mfano kwa upande wa kandanda tutaona kwamba mkoa
huo ulitingisha sana kwa vipaji vya wanasoka.
Kina Manara,
Kitwana Manara, Sunday Manara, Kassim Manara na ndugu zao wengine wanatoka
Kigoma. Baadaye kikafuatia kizazi cha kina Edbili Lunyamilla, Nteze John, Omari
Mavumbi, Itutu Kigi na wengineo wengi.
Kwa upande
wa wasanii wa muziki Kigoma imetoa watu wengi wenye majina makubwa katika sanaa
hiyo, kama Shem Kalenga, Hassan Rehan
Bitchuka, Marijani Rajabu, Zahir Ally Zorro, Banana Zorro, Wema Abdallah, Nyota
Waziri na wengineo wengi.
Kwa upande
wa muziki wa kizazi kipya Kigoma imefanya kufuru. Imetoa vijana wengi wa muziki
huo wakiongozwa na mtaalamu wa muziki, kwa maana ya kutunga, kuimba, kucheza
kila ala ya muziki na kutengeneza muziki, Emmanuel Bizimana Ntavyo, maarufu
kimziki kama Bizman. Vilevile wapo wengine wengi wa muziki wa kizazi kipya,
kama kina Ally Kiba, Banana Zorro, Jacqueline Ntuyabaliwe, maarufu kama K-Lynn
na wengine wengi.
Lakini
pamoja na wote hao makala hii ni mahususi kwa moja ya vipaji hivyo vya mkoa wa
Kigoma ikiwa imemlenga chiriku wa muziki wa kizazi kipya kwa sasa hapa nchini,
Nassibu Abdul, maarufu kama Diamond Platnumz.
Diamond
kadhihirisha kipaji cha sanaa ya muziki kutokana na mafanikio aliyoyapata kwa
kipindi cha muda mfupi alioutumia katika sanaa hiyo. Naweza kusema kwamba ni
kipindi kisichozidi miaka mitatu. Hiyo ni tofauti na kipindi alichokitumia
mfalme wa muzuki wa pop duniani, Michael Jackson, kuwa kileleni mwa mafanikio.
Michael Jackson alitumia zaidi ya miaka kumi kufika kileleni, kati ya 1967 –
1979.
Lakini ndani
ya miaka mitatu Diamond ameweza kuibeba Tanzania na kuiweka kwenye chati ya
kimataifa kwenye fani hiyo ya muziki wa kizazi kipya. Na ninaposema ngazi ya
kimataifa sina maana ya kuvuka tu mipaka ya nchi na kuingia nchi za jirani kama
Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Zambia, Malawi, Msumbiji wala Kongo, kama
ambavyo wameweza kufanya wasanii wengine wa muziki huo wa hapa nchini,
ninamaanisha kimataifa kwa maana halisi. Nalenga nchi za mbali na Tanzania.
Muziki wa
Diamond kwa sasa unapigwa kwenye nchi mbalimbali za Afrika kuanzia Afrika
Kusini, Afrika ya Kati, Mashariki na Afrika Magharibi, ukiondoa nchi za Kiarabu
kwa upande wa Afrika Kaskazini, ambako sina uhakika kama muziki wa kizazi kipya
una mashabiki kulingana na utamaduni wa Kiarabu ulivyo.
Kwa maana
hiyo Diamond kaiweka Tanzania kwenye chati ya kimataifa kwa maana halisi
kimuziki. Kwa sasa msanii huyo anakula
sahani moja na wasanii wa kimataifa kama kina Peter Okoye na Paul Okoye,
Wanigeria wanaounda kikundi cha P Square, ambao mara kadhaa wamemuomba watoe
naye vibao vya pamoja. Pia yuko kwenye kiwango cha wanamuziki kama Youssou
N’Ndour wa Senegal na wengine wa aina hiyo.
Kwa eneo
hili la Afrika Mashariki, nashindwa kumtofautisha Diamond na mwanamuziki wa
Uganda, Joseph Mayanja, maarufu kama Chameleone. Kwa sasa wanamuzi hao
wanafanana kwa kwa mambo kadhaa nitakayoyajadili hapa chini.
Tanzania
iliwahi kuvuma sana duniani miaka ya nyuma kupitia kwa wanamichezo, hususan
wanariadha, kina Filbert Bayi, aliyewahi kuwa bingwa wa mbio za mita 1500
duniani, ambaye mpaka sasa anashikilia rekodi ya mbio hizo kwenye michezo ya
Jumuiya ya Madola aliyoiweka mjini Christchurch nchini New Zealand mwaka 1974.
Wengine ni Seleman Nyambui, Adventina Mtakyawa, Juma Ikangaa, Gidmas Shahanga
na wengine wengi.
Lakini
kutokana na umri kuwatupa mkono nyota hao, jina la Tanzania limefifia katika tasinia ya
michezo na kuifanya nchi yetu isahaulike kabisa kana kwamba haipo kwenye nyanja
ya michezo na burdani!
Hivyo
Diamond ni kijana aliyedhamiria kulipandisha tena jina la nchi yake kupitia tasinia
ya burdani. Na niseme kwa uhakika kabisa kwamba ameweza. Hilo linashadidiwa na
tuzo mbalimbali za kimataifa anazozipata kwa sasa kwa upande huo wa burdani
baada ya kushindanishwa na wasanii wengine wa kimataifa toka nchi mbalimbali.
Kitu cha kipekee
nilichokigundua kwa Diamond na kuhisi kwamba pengine ndicho kinachochochea
mafanikio yake ni tabia yake ya kusikiliza ushauri na kuufanyia kazi.
Wakati
fulani nilimpa changamoto, ambayo vilevile niliwahi kuitoa kwa Joseph Mayanja
(Chameleone) wa Uganda nilipokutana naye Jijini Mwanza, Mei mwaka jana, kwamba
kwa kiwango alichopo hapaswi kuendelea kuimba muziki kwa kutumia mtindo wa
“play back”, kwa maana ya kuimba kwa kufuatiza muziki uliorekeodiwa tayari, kwamba anatakiwa kuwa na vyombo vyake na
kupiga muziki wa moja kwamoja pasipo kutumia CD. Diamond kanielewa na kusema
kwamba hilo analifanyia kazi kwa bidii kubwa.
Kitu kingine
ni namna anavyoendesha mahusiano na jamii aliyomo. Kawaida kuna dhana ya kwamba
wasanii ni watu wasioeleweka vizuri ndani ya jamii, wahuni, na huo kuwa mwanzo
wa neno usanii, kwamba fulani kanifanyia usanii ikiwa na maana ya kanifanyia
uhuni.
Lakini hilo
ni tofauti kabisa kwa Diamond. Yeye anapenda sana kuwasaidia wenye mahitaji
kulingana na hali halisi ilivyo. Kipindi fulani kwa mfano, kwa kuuthamini
mchango wa Baba wa Muziki hapa nchini, Marehemu Muhidini Mwalimu Gurumo,
aliamua kumpatia msaada wa gari jipya. Huo ni usanii kwa upande wa pili
anaouonyesha Diamond tofauti na upande uliozoeleka kwa jamii.
Diamond
anasema kwamba amejipangia kila mwezi kuwa anatembelea vituo vya watoto yatima
na kutoa misaada mbalimbali kadri inavyowezekana. Huo ni mchango mwingine
katika jamii anaoufanya kijana huyo.
Anawashauri
vijana wenzake, hasa wasanii, wanaojiingiza kwenye ulevi uliopindukia pamoja na
matumizi ya madawa ya kulevya waache mambo hayo mara moja. Anasema kwamba mambo
hayo yanaharibu vipaji na wakati mwingine kusababisha kupoteza maisha. Anasema
ili kukilinda kipaji chake yeye anahakikisha anaepukana na mambo hayo yasiyo na
maana na yaliyo hatari kwa maisha ya binadamu.
Diamond
anasema kwamba alizaliwa Septemba 22, 1990, Kigoma, na kwamba kabila lake ni
Mmanyema.
Anasema
kwamba kilichomfanya aingie kwenye muziki ni kipaji chake kilichojitokeza tangu
akiwa shule ya msingi. Eti alikuwa akipendelea kuimba kwenye kwaya ya shule na
burdani nyingine za shuleni.
Huyo ndiye
Nassibu Abdul, au ukipenda Diamond Platnumz, ambaye wasanii wengine vijana wanapaswa
wamtumie kama kipimo ya mafanikio katika usanii huo wa muziki wa kizazi kipya
wanaoufanya. Bilashaka watakaofuata mwenendo wake watafanikiwa kama yeye
alivyo.
0784 989 512