KUHUSU KUGAWANA MAJIMBO
CHAMA CHA DEMOKRASIA NA
MAENDELEO
(CHADEMA)
TAARIFA KWA UMMA
KUHUSU UKAWA KUGAWANA MAJIMBO
Tangu jana
kumekuwa na taarifa kupitia njia mbalimbali za upashanaji habari kuhusu msimamo
wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi
ya ubunge kwenye majimbo ya uchaguzi nchini.
Habari hizo
ambazo zingine zimeripotiwa kwenye vyombo vya habari hususan magazeti ya jana
(Alhamis) na leo (Ijumaa), zimesema kuwa UKAWA ‘wameshagawana’ majimbo kadha wa
kadha na kwamba bado kuna ubishano katika baadhi ya majimbo kutafuta mwafaka wa
kufikia lengo la kuwa na mgombea mmoja badala ya kila chama kuweka mgombea
wake.
Tunapenda
kutoa ufafanuzi juu ya habari hizo ambazo kwa namna moja ama nyingine
zimesababisha usumbufu usio wa lazima kwa wafuasi, wapenzi, wanachama na
viongozi wa CHADEMA na wanachama wa vyama vingine vinavyounda UKAWA.
CHADEMA kama
walivyo washirika wenza wa UKAWA, kiko kwenye mazungumzo vyama vingine katika
umoja huo ili kuhakikisha lengo la kusimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi
mkuu wa mwaka huu utakaohusisha nafasi za udiwani, uwakilishi, ubunge na urais,
linafikiwa.
Mazungumzo
bado yanaendelea vizuri. Hayajafikia tamati. Hivyo taarifa hizo ambazo
zimeendelea kusambaa kwamba UKAWA ‘wameachiana au kugawana majimbo’ na kwamba
kuna maeneo tayari yamepewa chama fulani na maeneo mengine mwafaka haujafikiwa,
si rasmi wala si sahihi.
Kwa uzito wa
hatua hiyo, mazungumzo yakikamilika na makubaliano kufikiwa, viongozi wakuu wa
vyama vinavyounda UKAWA, kikiwemo CHADEMA, watatoa taarifa rasmi na sahihi kwa umma
wa Watanzania ili Watanzania waelewe kwa ukamilifu uamuzi huo.
Wafuasi,
wapenzi, wanachama na viongozi wa CHADEMA wanaendelea kufanya kazi za ujenzi na
uimarishaji wa chama katika kila eneo kadri ya maagizo ya vikao vya chama,
hususan kupitia program endelevu ya CHADEMA ni Msingi, operesheni mbalimbali
mf; kuhamasisha wananchi kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura kwenye uchaguzi
mkuu mwezi Oktoba, n.k.
Katika
shughuli za uenezi na uimarishaji wa CHADEMA, kwa kadri ya maagizo ya chama,
viongozi waendelee kusimamia misingi ya ushirikiano wa UKAWA kwa ajili ya
matumaini na haki za Watanzania ambao wanajiandaa kutimiza kiu yao ya kufanya
mabadiliko kwa kuiondoa CCM madarakani kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Imetolewa leo Ijumaa, Machi 20, 2014
na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na
Mawasiliano