MH.LOWASSA ASHANGAZWA NA KAULI YA NAPE
Siku moja baada katibu wa itikadi na uenezi wa chama cha mapinduzi
(CCM) Nape Nnauye kutoa kauli ya chama hicho kuhusu makundi
yanayojitokeza kumshawishi waziri mkuu mstaafu Mhe Edward Lowassa
kugombea urais, kuwa yanaweza kumkosesha sifa kiongozi huyo ya kuwania
nafasi hiyo Mhe Lowassa amejibu kauli hiyo na kudai anashangazwa nayo
huku akihoji imetokana na maamuzi ya kikao gani ndani ya CCM.
Mhe Lowassa anatoa kauli hiyo katika muendelezo wa kupokea makundi
mbalimbali ya jamii kumshawishi kuwania nafasi urais ambapo safari hii
waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda zaidi ya 60 na wananchi wa
kawaida wamefunga safari kutoka wilayani mbarali mkoa wa Mbeya mpaka
mjini Dodoma kumshawishi agombee ambapo amesema kauli ya Nape Nnauye
inamshangaza kwani chama cha mapinduzi kina utaratibu wake wa kujadili
mambo kama hayo kupitia vikao mbalimbali.
Mhe Lowassa pia akawataka wanaoendelea kumnyooshea vidole kuhusu
hatua ya wananchi wenye imani naye kujitokeza kumshawishi awanie nafasi
hiyo wasubiri ufike wakati muafaka ili wana-CCM na wananchi waweze kutoa
maamuzi yao huku akisisitiza watu hasa vijana kujitokeza kwa wingi
kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ili wapate haki
yao ya kikatiba ya kuchagua kiongozi wanayemuhitaji.
Awali kundi hilo la vijana na bodaboda waliosafiri umbali wa
kilometa zaidi ya 600 wakiongozwa na kamanda wa UV-CCM wilaya mbarali
Ibrahim Ismaili wamesema lengo la safari yao hiyo ni kuungana na
watanzania wengine kumtia moyo Mhe Lowassa ashawishike kuwania urais
kwani wana imani kubwa naye huku wakidai pamoja na mambo mengine kama
alivyoweza kujenga shule za kata nchi nzima pia ataweza kutegua bomu la
tatizo la ajira hasa kwa vijana.