TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI HATUA ZA HARAKA ZILIZOCHUKULIWA NA SERIKALI KATIKA KUKABILI MAAFA YALIYOSABABISHWA NA MAFURIKO WILAYANI KAHAMA, MKOA WA SHINYANGA
JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
HATUA ZA HARAKA ZILIZOCHUKULIWA NA SERIKALI KATIKA
KUKABILI MAAFA YALIYOSABABISHWA NA MAFURIKO WILAYANI KAHAMA, MKOA WA SHINYANGA
Kufuatia mvua kubwa
zilizonyesha usiku wa tarehe 04 Machi, 2015 Wilayani Kahama mafuriko makubwa
yalitokea na kuathiri wakazi wa kata ya Mwakata katika vijiji vya Mwakata,
Numbi na Mwaguguma.
Kutokana na mafuriko
yaliyotokea tathmini ya awali inaonesha kuwa watu 42 wamepoteza maisha, watu 82
wamejeruhiwa na watu wanaokadiriwa kufikia 574 wameathirika. Jumla ya nyumba
137 zimeathirika kwa viwango mbalimbali.
Hatua zilizochukuliwa
Serikali imechukua hatua za
haraka kwa kushirikiana na wananchi kuwafikia na kuwanusuru waathirika wa
mafuriko hayo waliokuwa wamezingirwa na mafuriko. Aidha vimeanzishwa vituo vya
muda kuwahifadhi wananchi hao kwenye
Shule.
Serikali imepeleka misaada
ya kibinadamu kama ifuatavyo;
i.
Chakula tani 20. Maharage tani 5, Mafuta ya
kupikia lita 1,126 na Sukari tani 1.3
ii.
Vifaa vya matumizi ya ndani ambayo
vinajumuisha blanketi 650, ndoo 82 za
lita 20, ndoo 82 za lita 10 ; Vifaa vya kupikia seti 82 na madumu 82
Kwa kuwa bado Serikali inalo
jukumu kubwa la kuwawezesha waathirika kurejea katika maisha yao ya kawaida; inapenda kuwatangazia wale
wote wanaoguswa na maafa haya kuwa
Serikali inaendelea kupokea misaada mbalimbali ambayo
inahitajika kwa waathirika.
Mahitaji haya ni pamoja na sare
za shule; daftari za wanafunzi; mavazi ya kike na kiume; na chakula. Aidha kwa
kuzingatia kuwa waathirika hawa wamepoteza mali na fedha katika maafa haya;
misaada ya vifaa vya ujenzi (sementi, mabati, mbao, n.k.) inahitajika sana.
Utaratibu
wa kupokea misaada hiyo kwa walio Dar es Salaam wanaweza kuiwasilisha misaada
hiyo Idara ya Kuratibu Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu au kuwasiliana na Mkuu wa
Mkoa wa Shinyanga_ Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Serikali itaendelea
kuwasaidia Waathirika dhidi ya Changamoto zinazoweza kujitokeza hususani za
kiafya zinazosababishwa na uchafuzi wa vyanzo vya maji na mazingira. Elimu juu
ya ujenzi wa nyumba bora na makazi maeneo salama itaendelea kutolewa.
IMETOLEWA NA
Dkt. Florens Turuka
KATIBU MKUU
OFISI YA WAZIRI MKUU
6 MACHI, 2015.