TAFITI ZA KUFANYIWA TAFITI
NA PRUDENCE KARUGENDO
IMEKUWA kawaida kujitokeza taassisi mbalimbali
zinazojifanya kuendesha tafiti kuhusu hali ya kisiasa hapa nchini wakati wa
uchaguzi mkuu. Mara nyingi, kama sio
mara zote, tafiti zinazofanywa zinalenga
kutoa mwelekeo wa uchaguzi utakavyokuwa kwa maana ya ni mtu gani au chama gani
kilicho kwenye mwelekeo wa kushinda uchaguzi.
Jinsi inavyoonekana tafiti
hizi zinalenga kushawishi, kwa namna ya kampeni, badala ya kutoa mwelekeo wa
halihalisi ilivyo. Katika kufanya hivyo tafiti hizi zinaonekana kuwapigia
“debe” baadhi ya watu au vyama vya siasa kwa kuonyesha kuwa ndio au ndivyo
vinavyopendelewa na wananchi walio wengi ambao ndio watakaofanya uamuzi katika
uchaguzi mkuu unaokuja.
Mimi nadhani ipo haja ya
kuzifanyia tafiti hizi taasisi zinazojitokeza kila uchaguzi mkuu unapokaribia. Nazo
zifanyiwe utafiti ili kujua malengo yake na walio nyuma ya hizi taasisi za
utafiti kutokana na tafiti zake mara nyingi
kuwa za utata.
Mfano katika Tanzania hakuhitajiki
sayansi kubwa ili kujua nani atashinda hasa katika ngazi ya urais kulingana na
hali halisi tuliyoizoea inayotokana na
sababu zilizo wazi.
Mojawapo ya sababu hizo ni
kwamba uchaguzi wenyewe kwa hapa Tanzania haujakaa kisayansi kiasi cha kuufanya
utoe picha halisi ya matakwa ya wapiga kura. Katika mazingira hayo ni vigumu
kujitokeza mtu na kudai ametumia mbinu za kisayansi na kujua ni mtu gani
anaweza kushinda au chama kipi kinaweza kushinda kwa maana halisi ya matakwa ya
wananchi.
Mfano Tanzania, kama zilivyo
nchi nyingi zinazoitwa za dunia ya tatu, ambako uchaguzi unafanywa tu kutimiza
mazoea ili ionekane kwamba viongozi wa nchi husika wanatokana na matakwa ya
wananchi, haijataka kuwa na vifaa vya kisasa vya kufanyia uchaguzi tangu kwenye
ngazi ya uandikishaji wa wapiga kura. Na hilo sio jambo ambalo linaweza
kuchukuliwa kama uduni wa nchi wa kutoweza kumudu vifaa vya aina hiyo, la hasha.
Tunayo mambo mengi ambayo
wakati mwingine yanayazidi hata ya nchi zilizo na uwezo zaidi ya nchi yetu, japo
mambo yenyewe si muhimu kama lilivyo suala hilo la vifaa vya kufanyia uchaguzi.
Mfano rais wetu anayo ndege
ya kusafiria ya kisasa na ya gharama kubwa sana, wakati waziri mkuu wa Uingereza anatumia ndege
za abiria wa kawaida anapotaka kusafiri! Ikumbukwe nchi yetu inajiendesha kwa
kutegemea zaidi hisani ya Uingereza na nchi za aina hiyo.
Lakini pamoja na kuonyesha
ufahari wa namna ya kumtunza kiongozi wetu mkuu kuliko wanavyofanya Wangereza,
bado nchi yetu inaona ugumu wa kumwezesha mwananchi kuonyesha matakwa yake
halisi kwa kisingizio cha ufukara!
Tunabaki kufanya uchaguzi kwa
njia za kubahatisha bila ya uhakika wa ni namna gani mtu anaweza kuthibitisha
matakwa yake, kamchagua nani na kumuacha nani. Sababu vifaa vya kutupatia
uhakika huo hatuna. Katika mazingira ya aina hiyo ambayo mpiga kura hawezi kuwa
na uhakika kama alichokikubali ndicho kilichoonyeshwa mtu wa pembeni anawezaje
kutafiti mpaka akajua mpiga kura atamtaka nani na kumuacha nani?
Fikiria katika mazingira
ambayo idadi ya wanaojitokeza kupiga kura wakati mwingine haifiki nusu ya waliojiandikisha
kupiga kura, inawezekanaje mtu atafiti na kutoa mwelekeo wa uchaguzi ulio
sahihi?
Mara nyingi tumeshuhudia
matokeo ya kura yakichezewa kadri ya wasimamizi wa vituo vya kupigia kura
wanavyotaka, kitu ambacho hakitoi taswira ya kweli ya uchaguzi husika. Tumeona
aliyeshinda akionekana ameshindwa na aliyeshindwa akionekana ndiye kashinda!
Hiyo ni kutokana na kutokuwa na vifaa
vya kuzuia uovu wa aina hiyo!
Hizo ni kura halisi za
uchaguzi unaofanyika chini ya usimamizi na ulinzi, inawezekanaje sasa utafiti
usio na usimamizi wala ulinzi ndio utoe matokeo yaliyo sahihi kiasi cha wananchi
kukubaliana nayo kuwa ni ya kweli?
Kitu kingine kilicho kigumu
katika kuzifanya tafiti hizi zisiaminike ni mazoea waliyo nayo Watanzania ya
kutofanya tathimini kabla ya kufanya maamuzi. Kwahiyo ugumu unakuwa kwamba
huwezi kujua mtu ambaye hafanyi tathimini ataamua nini kesho baada ya leo
kuonyesha msimamo fulani. Watanzania walio wengi wamezoea kufanya maamuzi kwa
kitu kilichowafurahisha kwa wakati huo na dakika hiyo, hata kama kitu chenyewe
hakionyeshe mustakabali wa siku kumi zijazo!
Mfano mwaka 2005 Watanzania
walitokea kumpenda Kikwete aliyeonyesha mvuto wa aina yake, naye kwa kuutumia
mvuto huo aliokuwa nao kwa wananchi akawapa wananchi ahadi za ajabu akimalizia
na maisha bora kwa kila mwananchi, hiyo ilikuwa zawadi aliyowapa wananchi
waliotokea kumkubali kwa wingi. Na kweli, kwenye uchaguzi mkuu akapata ushindi wa
kishindo ambao wengine walisema ni wa kimbunga.
Lakini baada ya miaka 5 hatukuyaona maisha bora kwa
kila mwananchi. Kikwete akaongezewa miaka mingine mitano japo kwa kusuasua,
yeye akazidi kuwapa matumaini wananchi kwa kuongeza ahadi, mpaka sasa
anapoelekea kumaliza miaka 10 ya kipindi chake cha kukaa Ikulu ni mafanikio
gani yanayoweza yakaakisi mvuto aliokuwa
nao kwa Watanzania? Je, ni kweli kila Mtanzania anayo maisha bora
yaliyoahidiwa?
Baada ya kuangalia namna
Watanzania walivyo wagumu kufanyiwa tafiti zinazoonyesha msimamo na mwelekeo
wao kisiasa, sasa tuangalie namna tafiti
zenyewe zinavyofanyika.
Maranyingi tafiti hizi
zinatoa takwimu ambazo zinaonekana ni za kubuni au kuhisi, sababu hazionyeshi
zilikofanyikia. Kila mtu anaweza kujiuliza ni lini amewaona watafiti
wakimuuliza kuhusu masuala ya uchaguzi kwamba ni chama gani au mtu gani
anayetaka kumpigia kura. Kama hakuna aliyewaona tuseme hizo tafiti zao
wanazifanyia wapi?
Hii inaweza kutuleta kwenye
hitimisho la kwamba tafiti hizi zina malengo fulani kwa watu au vikundi fulani
ikiwa ni njia mojawapo ya kuwashawishi wananchi wavifikirie vikundi hivyo au
watu hao kwa maana kwamba ndivyo, au
ndio, walio kwenye uwezekano wa
kukubalika. Hizo ni kama njama tu kwa mtazamo wangu. Tafiti za kinjama.
Utafiti kuhusu matakwa na
maamuzi ya Watanzania ni vigumu kufanyika katika hali ya sasa waliyomo
Watanzania. Hii ni hali ya kubahatisha tu ambapo mambo hayawekwi wazi kwa
makusudi mazima kwa hofu ya uwazi huo kuleta matokeo yasiyopendeza kwa baadhi
ya watu. Kwa mantiki hiyo ni lazima matokeo yanayopatikana kwenye tafiti hizo yawe
ya kubahatisha vilevile ambayo hayapaswi kutiliwa maanani.
Kinachoshadidia mawazo yangu
haya ni kama hiki; niliamua kufanya utafiti binafsi katika maeneo ya vijijini
ambako watu hawajali suala la kutathimini mambo, nikawapata watu kama 100 na
kuwauliza ni chama gani wanakitaka kati ya CCM na Chadema, wakanijibu tofauti na swali langu lilivyokuwa.
Wao walisema wana kiu, kama nataka kuuliza maswali yangu kwanza niwapoze kiu. Nikajitutmua
na kuwapa kinywaji.
Baada ya kupata kinywaji
wakawa wanatafuta jibu la kunifurahisha, nao wakaniuliza, kwani wewe ni chama
gani? Nikawajibu CCM, wakacheka na kusema sasa unawezaje kutuuliza habari ya
Chadema wakati unaelewa kuwa hapa miaka nendarudi sisi tunaijua CCM tu? Nilipowambia
kuwa huu ni wakati wa vyama vingi vya siasa na nimeishahamia Chadema papo hapo
wote wakageuka wakawa Chadema, wakisema walikuwa wananipima tu!
Kwa mtindo huo umawezaje
kusema umefanya utafiti na kujua ni chama gani au mtu gani anayekubalika kwa
wananchi wa aina hiyo?
Tafiti za aina hiyo
zinafanyika na kufanikiwa katika nchi ambazo chaguzi zinaakisi matakwa halisi
ya wapiga kura. Kama tunataka kuziiga tafiti hizo basi tuanze kuiga namna ya
kufanya kitu cha kweli, kwa maana ya kuhakikisha kwamba matakwa ya wananchi
yanakuwa ya kweli bila kupindishwa.
Mfano wa wazi ni wa Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 1995. Katika mkoa wa Dar
es salaam wananchi walikuwa wamedhihirisha kukikubali chama cha upinzani cha
NCCR- Mageuzi. Ikaonekana kwamba majimbo yote ya Dar es salaam yangekwenda kwa
chama hicho. Kilichofuatia ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuuvuruga kwa makusudi
uchaguzi katika mkoa wa Dar es salaam na baadaye kutangaza kuwa utarudiwa baada
ya muda fulani. Uliporudiwa mambo yakabadilika!
Sababu zilizotolewa na Tume
ya Uchaguzi hazikuwa na pahala pa mashiko. Sababu haiwezekani uchaguzi ukaenda
vizuri sehemu za Karagwe, mpakani mwa Tanzania na Uganda na Rwanda, zaidi ya kilometa
1500 toka makao makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, halafu uchaguzi huohuo
uvurugike kwa kutotimia vifaa vya uchaguzi maeneo ya Mtaa wa Shabani Robert,
hatua chache toka ofisi za Tume ya Uchaguzi.
Nihitimishe kwa kusema kwamba
tafiti hizi kuhusu uchaguzi zingekoma kuliko kuendelea kuwapotosha wananchi kwa
kuwaelekeza na kuwashawishi namna ya kufanya uchaguzi. Wananchi waachwe
wachague wanavyoona wao inafaa kwa sababu mambo yote ni ya kubahatisha tu.
0784 989 512