UTETEZI WA GURUMO WA IKULU WAZUA MSHANGAO
MAJIBU tata ya Mnikulu, Shabani Gurumo mbele ya
Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma yalizua mshangao kwa
wananchi waliokuwepo.
Pia utetezi huo ulizua mvutano mkubwa kati ya Gurumo
na wanasheria wa sekretarieti ya maadili, kwa upande mmoja, na pia mvutano kati
ya wanasheria hawa na wakili wa Gurumo, kwa upande mwingine.
Mwansheria: Majina yako kamili ni yapi
kiongozi?
Gurumo: Naitwa Shaban Rajab Gurumo.
Mwanasheria: Kiongozi, unaweza ukaliambia
Baraza hili unafanya kazi gani?
Gurumo: Kazi yangu ni mnikulu. Nasimamia
watumishi wote wa ndani ya Ikulu; nasimamia ukarabati wa majengo yote ya Ikulu;
naratibu ikulu ndogo zote nchini; napokea mabalozi wapya kutoka nchi za nje; na
ninaandaa tafrija zote za ikulu zinazomhusisha rais.
Mwansheria: Kiongozi, akaunti namba
00110102645401 iliyofunguliwa Benki ya Mkombozi 04 Februari mwaka 2014 ni ya
nani?
Gurumo: Akaunti hiyo ni yangu. Niliifungua
baada ya rafiki yangu James Rugemalira kunielekeza nifungue akaunti katika
benki hiyo?
Mwansheria: Kiongozi, tarehe 05 Februari 2014
akaunti hiyo ilipokea shilingi 80,850,000. Hiyo fedha ni mali ya nani?
Gurumo: Hiyo fedha ni mali yangu halali.
Mwansheria: Kiongozi, hiyo fedha ulipewa na
nani?
Gurumo: Nilipewa na rafiki yangu aitwaye
James Rugemalira.
Mwanasheria: Kiongozi, wewe na James
Rugemalira mlifahamiana vipi na tangu lini?
Gurumo: Sikumbuki vizuri. Lakini nadhani
nilimfahamu tangu zamani kupitia daktari wa familia yangu aitwaye Fred
Limbanga, ambaye nimekuja naye hapa leo kama shahidi.
Mwansheria: Kiongozi, kwenye nakala ya
Ankara za benki uliyowasilisha katika ofisi za sekretarieti ya maadili
inaonekana fedha hizo zilitoka kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd na
sio kwa James Rugemalira. Unasemaje kuhusu jambo hili?
Gurumo: (Anatazama nakala ya ankara kwanza).
Ndio leo nimeligundua jambo hili. Hapo kabla sikuwa nimechukua muda kuisoma
ankara hii. Muda wote nilijua fedha zimetoka kwa James Rugemalira.
Mwansheria: Kiongozi, hiyo fedha ulipewa kwa
ajili gani na ziliambatana na masharti gani?
Gurumo: Sikuambiwa ni kwa sababu gani na
hakuna masharti yoyote niliyopewa kuhusu matumizi yake. Naomba akaulizwe James
Rugemalira.
Mwanasheria: Kiongozi, James Rugemalira
alikuingizia fedha hizo kwa sababu uliziomba au hapana?
Gurumo: Sikumwomba James Rugemalira fedha. Na
sijui kwa nini aliniwekea fedha hizo. Hata aliponiambia nifungue akaunti benki
ya Mkombozi ili aniwekee fedha sikumwuliza fedha hizo ni za nini. (Kicheko
kutoka kwa wananchi).
Mwansheria: Kiongozi, kwa sasa karibu fedha
yote umekwisha kuitumia. Uliitumia katika mambo gani na kwa nini?
Gurumo: Niliitumia katika matumizi mbalimbali
yakiwemo matibabu ya ugonjwa wa kansa uliokuwa unamsumbua mke wangu.
Mwansheria: Kiongozi, fedha hizo ambazo
umekiri ni mali yako, uhalali wake unatokana na nini. Ni mshahara, posho, faida
katika biashara, urithi, kuokota, zawadi au kitu gani?
Gurumo: Sio mshahara, posho, faida katika
biashara, urithi, au zawadi. Pia hazikuokotwa. Ni fedha nilipewa tu. (Kicheko
kutoka kwa wananchi).
Mwansheria: Kiongozi, unawezaje kutumia fedha
nyingi kiasi hicho bila kwanza kutafiti sababu fedha hizo kuingizwa katika
akaunti yako?
Gurumo: Sikuwa na hofu yoyote kwani James
Rugemalira ni rafiki yangu kwa zaidi ya miaka kumi sasa.
Mwansheria: Kiongozi, kwa mujibu wa sheria ya
maadili ya viongozi wa umma, umewahi kutoa taarifa ya fedha hizi kwenye
sekretarieti ukionyesha kwamba ni miongoni mwa mali yako mpya?
Gurumo. Tayari. Nilifanya hivyo tangu 29
Desemba, 2014 kupitia fomu maalum. Fedha hizi zimetajwa kwenye ukurasa wa kumi
na saba. (Anaonyesha nakala ya fomu aliyoijaza).
Baada ya kikao, MwanaHalisi Online ilipata fursa ya
kungea na wanasheria wa sekretarieti ya maadili kuhusu maana ya neno “zawadi”
kwa mujibu wa sheria. Swali hilo pia nililielekeza kwa wakili wa Gurumo.
Kwa upande wake, Gurumo alisema neno hilo halina
fasili rasmi katika sheria za Tanzania. Lakini, wanasheria wa shekretarieti
walikuwa na maoni tofauti.
Walisema, “Gurumo amekiri kwamba fedha zile ni mali
yake. Mali inaweza kupatikana kupitia mshahara, posho, biashara, urithi,
kuokota, au zawadi. Gurumo amekanusha yote haya. Kwa hiyo fedha hizo
anazimiliki kwa mujibu wa kanuni gani?,” walihoji.
“Fedha zile alizipokea kama zawadi na kinyume cha
sheria ya maadili ya viongozi wa umma na atatiwa hatiani na Baraza,”
walihitimisha.
CHANZO: mwanahalisionline