WAFUGA NYUKI WA KAGERA KUTEMBELEA SHAMBA (MANZUKI) LA MH. PINDA
Wafuga
nyuki kutoka mkoa wa Kagera watafanya ziara ya mafunzo kwenye manzuki ya Waziri
Mkuu, Mh. Pinda iliyoko Dodoma mwezi ujao.
Akizungumza na Bukoba Wadau Media juu ya ziara hiyo, Mratibu wa Ushirika
wa Wafuga Nyuki Kagera (Kagera Nyuki Mali Cooperative) Bwana Sadick Mwesiga
amesema kuwa Ushirika umepata mwaliko wa kwenda kujifunza kwenye moja ya
manzuki ya kisasa nchini. Mwaliko huu umepatikana baada ya kufanya mawasiliano
kupitia kwa wasaidizi wa Waziri Mkuu.
Katika
ziara hii Wafugaji wa Kagera watajifunza kwa kuona namna bora ya kufanya
ufugaji wa kisasa kwa kutumia mizinga iliyoboreshwa. Pia watajifunza jinsi ya
kuzalisha malkia wa nyuki, kutengeneza makundi ya nyuki na kuendesha manzuki
kibiashara kwa mbinu za kisasa.
Ujumbe
utakaofanya ziara Dodoma utajumuisha wafuga nyuki 20 wote kutoka Kagera. wawapo Dodoma wafuganyuki hawa watapata fursa
ya kulitembelea Bunge na kutambulishwa wakati wa vikao vya Bunge la Bajeti ya
mwaka 2015/2016 kwa mwaliko wa Mbunge wa Bukoba Vijijini Mh. Jasson Rweikiza.
Kagera
Nyuki Mali Cooperative ni Ushirika ulioanzishwa na wafuga nyuki mkoani Kagera kwa
malengo ya kuwaunganisha wafuga nyuki ikiwa ni jitihada za kuyafanya mazao ya
nyuki kuwa mazao mbadala ya kibiashara mkoani Kagera, kuongeza ubora na
uzalishaji wa mazao ya nyuki kutoka Kagera, kuwahakikishia wafugaji nyuki
masoko ya mazao ya nyuki yenye uhakika na yenye tija, kutafuta pembejeo na
mitaji ya kuwawezesha wanaushirika kukukuza shughuli zao katika sekta ya nyuki
na kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine katika kukuza sekta ya
nyuki Tanzania.
Ili
kufanya vema majukumu yake Ushirika umeanza zoezi la kuwatambua wafuga nyuki
mkoani Kagera. Wadau wa sekta hii wanaweza kuwasiliana na ushirika kupitia nyukimali@gmail.com
na simu namba 0767-988-173.