WANAHABARI KUTIWA KITANZI MUSWADA WA TAKWIMU
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania limepitisha miswada mitatu ndani ya saa tatu huku moja ya
miswada hiyo ikiwa ni kitanzi kwa waandishi wa habari ambapo mwandishi
atakayeandika takwimu za kutoka katika chanzo sahihi cha Serikali na
baadaye kugundulika amepotoshwa na chanzo hicho atahukumiwa miaka
mitatu jela au kulipa faini ya shilingi milioni kumi.
Miswada ambayo imepitishwa ni ile ya wakala wa usimamizi wa maafa
ya mwaka 2014,muswada wa sheria ya usimamizi wa kodi wa mwaka 2014
pamoja na ule wa sheria ya takwimu wa mwaka 2013 ambapo umesababisha
majibizano kati ya,Mbunge wa Ubungo John Mnyika,Mbunge Viti Maalum Ester
Bulaya pamoja na mwanasheria mkuu wa Serikali George Masaju kuhusiana
na kuwepo kipengele kisichofaa.
Kipengele hicho ni kile kinachosema mwandishi wa habari
atakayeandika takwimu za kutoka katika chanzo sahihi cha Serikali na
baadaye kugundulika amepotoshwa na chanzo hicho atalazimika kuchukuliwa
hatua za kisheria na Serikali ikiwemo kifungo cha miaka mitatu ama
kulipa faini ya shilingi milioni kumi ambapo wabunge hao wamekipinga
ilhali mwanasheria mkuu wa Serikali amesema kinafaa.
Maazimio ambayo yamepitishwa bungeni hapo ni la kuridhia mkataba wa
msingi na kanuni za utumishi wa umma na utawala barani Afrika la mwaka
2011 na lile la kuridhia makubaliano ya msingi ya ushirikiano katika
bonde la Mto Nile .