HALMASHAURI ZASHAURIWA KUPUNGUZA UTEGEMEZI WA RASILIMALI ZA KUKABILI MAAFA
Na.
Mwandishi Maalum.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe.
Halima Dendego amezitaka Halmashauri za mkoani humo kupunguza utegemezi wa rasilimali
za kukabili maafa kutoka kwa wafadhili wa nje badala yake zitumie rasilimali
zilizopo mkoani humo katika kujenga uwezo wa kukabili maafa kwa kulipa
kipaumbele suala la Kupunguza Athari za Maafa katika mipango na programu za maendeleo.
Akiongea wakati wa uzinduzi
wa Mpango
wa Kujiandaa Kukabili Maafa Mkoani Mtwara ulioandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu,
Idara ya uratibu wa shughuli za maafa, tarehe 24 Aprili, 2015, mkoani
Mtwara,
Dendego alibainisha kuwa Halmashauri zinaweza kupunguza utegemezi wa rasilimali
za kukabili maafa, kwa kuondokana na mtazamo wa kukabili maafa uliozoeleka
ambao unatenganisha kwa kiasi kikubwa hatua za utoaji wa misaada ya kibinadamu,
kurudisha hali na shuguli za kawaida za maendeleo.
“Majanga ya mafuriko, Ukame,
na mlipuko wa kipindupindu yamekuwa yakizisumbua Halmashauri zetu mara kwa mara.
Tunaweza kutumia rasilimali zetu
kukabili majanga haya badala ya kutegemea wafadhili wa nje, kwa kutumia
rasilimali zetu tunaweza kutoa elimu kuhusu athari za ujenzi na kuendesha
shughuli za uchumi katika maeneo hatarishi, umuhimu wa usafi wa mazingira
matumizi ya mbegu zinazostahimili ukame pamoja na kuzuia ujenzi katika maeneo
hatarishi” alisema Dendego
Aliongeza kuwa, Upunguza
Utegemezi wa rasilimali za kukabili maafa unawezekana kwa kuwa na jamii yenye
kuhimili maafa kwa Kuzuia, kupunguza athari
na kujiandaa kama vipaumbele katika menejimenti ya maafa katika ngazi
zote. Ili kuhakikisha kunakuwa na jamii hiyo, kila Halmashauri inapaswa kukaa
na wadau wote katika halmashauri husika na kuainisha maeneo ya kushughulikia
kwa haraka na kuwa na mgawanyo bayana wa
majukumu.
“Juhudi za jamii ni nguzo
muhimu katika kujiandaa kukabili maafa, juhudi hizo zinajumuisha kuainisha na
kutekeleza hatua zinazoweza kuchukuliwa kujiandaa kukabiliana na maafa
yanayoweza kutokea ghafla kama mafuriko na yale yanayochukua muda mrefu na wa
kati kama ukame na janga la mabadiliko
ya tabia nchi” alisema Dendego.
Awali akiongea katika
uzinduzi huo Mkurugenzi Idara ya Uratibu Shughuli za Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu
Brig.Jen Mbazi Msuya alifafanua kuwa kuandaliwa kwa mpango huo ni jitihada zinazochukuliwa na serikali za kujenga uwezo katika ngazi za
Halmashauri kukabiliana na maafa.