MAASKOFU WAWATAKA WAKRISTO KUWA WATULIVU WAKATI SAKATA LA ASKOFU GWAJIMA LIKISHUGHULIKIWA KISHERIA.
Siku moja baada ya kiongozi wa kanisa la ufufuo na uzima kuachiwa kwa
dhamana na jeshi la polisi, maaskofu na wachungaji kutoka makanisa
mbalimbali wameibuka na kuwataka wakristo kote nchini kuwa katika hali
ya utulivu wakati sakata la askofu Josephat Gwajima likishughulikiwa na
vyombo vya sheria.
Wakizungumza jijini Dar es Salaam na vyombo vya habari, maaskofu na
wachungaji kutoka makanisa mbalimbali, licha ya kukataa kusema
walichozungumza na mkuu wa jeshi la polisi nchini, wamewataka wakristo
kote nchini kuwa katika hali ya utulivu huku wakiendelea kuenzi tunu ya
amani iliyopo hapa nchini wakati vyombo vya sheria vikiendelea
kushughulikia sakata hili la askofu Josephat Gwajima.
Wakizungumzia kauli ya askofu Gwajima aliyotamka kwa vyombo vya
habari wakati akitoka kuhojiwa katika kituo cha polisi cha Osterbay
jijini Dar es Salaam kuhusu kusimamia kauli zake, maaskofu hao wamesema
kwamba askofu Gwajima hawawezi kusaliti kauli iliyotolewa na jukwaa la
waakristo Tanzania na akifanya hivyo hata wao watamshangaa na ndio maana
askofu Gwajima aliwaambia waandishi wa habari kwamba yeye kama mtumishi
wa mungu lazima akemee jambo analoona haliendi sawa.
Maaskofu hao na wachungaji wamempongeza kwa dhati askofu mkuu wa
jimbo kuu la Dar es Salaam Cadinali Polcarp Pengo kwa kutangaza kusamehe
yote yaliyotokea kati yake na askofu Josephat Gwajima kwani kwa kufanya
hivyo ndio ukiristo wa kweli.