Bukobawadau

MKUU WA MKOA WA KAGERA AKITEMBELEA KIWANDA CHA KAGERA SUKARI KUJIONEA UTEKELEZAJI WA MATOKEO MAKUBWA SASA KATIKA KILIMO

Katika mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) kitaifa unaolenga kuinua uchumi wa nchi kupitia sekta mbalimbali za kilimo, Maji, Elimu na Miundombinu mkoa wa Kagera  nao umelenga kuinua uchumi wake kupitia  sekta hizo kwa kuweka mikakati mbalimbali za kuutekeleza mpango huo.

Katika kutekeleza mpango  wa Matokeo Makubwa Sasa mkoa wa Kagera ulichagua zao la biashara la miwa linalozalisha sukari kama zao litakalolimwa na kutoa matokeo makubwa kwa haraka kwa kuinua uchumi wa mkoa na wananchi mmoja mmoja.

Zao la miwa siyo geni katika mkoa wa Kagera kwani linalimwa zaidi Wilayani Missenyi ambako kuna kiwanda cha wawekezaji wanaoendesha kilimo hicho kwa teknolojia ya kisasa na kuzalisha sukari. Kwa sasa kiwanda hicho kimeweza kulima hekta  12,000 katika udongo wenye rutuba.
Pamoja na kiwanda cha Kagera Sukari kuwekeza katika kilimo cha miwa  Wilayani Missenyi mkoani Kagera lakini pia wakulima mbalimbali (Outgrowers) katika Wilaya hiyo nao wanaendelea kulima miwa na kukiuzia kiwanda hicho ili kuongeza uzalishaji wa sukari.
Katika kuchochea uwekezaji na kuwahimiza wananchi na kiwanda cha Kagera Sukari kulima miwa kwa mpango wa Matokeo Makubwa Sasa Mkuu wa mkoa wa Kagera Mhe. John mongella alitembelea kiwanda hicho ili kujionea uwekezaji na mikakati ya kiwanda hicho kikishirikiana na wakulima wa nje katika kutekeleza kilimo cha miwa.
Katika ziara hiyo aliyoifanya Mhe. Mongella katika kiwanda cha Kagera Sukari tarehe 30 Marchi, 2015 alijionea jinsi sukari inavyozalishwa kiwandani hapo kuanzia hatua ya kwanza mpaka mwisho aidha alitembelea mashamba na kujionea jinsi uongozi wa kiwanda hicho unavyolima kisasa mbegu na aina mbalimbali  za miwa.
 Aidha katika taarifa yake Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Kagera Sukari Bwana Ranna alisema kiwanda hicho mpaka sasa kimeweza kuwekeza katika kilimo cha kisasa cha miwa katika hekta 12,000 na kutoa ajira zaidi ya 4,000 kwa wananchi wa mkoa wa Kagera na kutoka nje ya mkoa wa Kagera.

Katika kutekeleza mpango wa Matokeo Makubwa Sasa Bw. Ranna alisema tayari wameanza maandalizi  upanuzi wa mashamba katika eneo la Kitengule ng’ambo ya mto Kagera kwa kuanza na utafiti wa kina kuhusu udongo wa eneo hilo kuona kama unafaa katika kilimo cha miwa.
Vilevile Meneja mkuu wa Kagera Sukari aliiomba serikali kutengeneza miundombinu ya barabara katika mashamba ya wakulima wa nje ili kurahisisha uvunaji na usafirishaji wa miwa kutoka katika mashamba hayo hadi kiwandani.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. John Mongella alimwakikishia Menenja mkuu wa Kiwanda cha Kagera Sukari kuwa serikali itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha inatekeleza majukumu yake katika kuhakikisha wawekezaji hawapati vikwazo katika uwekezaji wao, aidha serikali ya mkoa itakikisha inajenga miundombinu ya barabara katika mashamba ya wakulima wa nje ili kuwarahisishia zaidi katika uwekezaji  wao jambo ambalo litawajenga kiuchumi zaidi.
Next Post Previous Post
Bukobawadau