Bukobawadau

MWANZO WA KUIPATA PESA NI KUIJUA KWANZA!

 Je? Na wewe ni mmojawapo wa wanaotafuta pesa? Kama jibu ni ndiyo, hiyo pesa unajua ni nini? mbali na kufahamu sura tu ya sarafu na noti? Ukiacha hilo, kuna cha zaidi unachojua kuhusu pesa? Ikiwa jibu ni “hapana” sasa wewe pesa utazipataje wakati huzijui? Mara nyingi watu husema kuwa, “huwezi kuona kitu usichokijua”! Mpaka sasa, ufahamu na uelewa uliopo juu ya pesa ni mdogo sana labda tu! ufahamu uliopo ni wa kujua jinsi pesa zinavyogawanyika na walio wengi tunafahamu zaidi kutoa na kujumlisha pesa, hasa wakati wa kurudisha chenji kwa mteja. Ukiacha hilo, taswira kubwa na ndefu iliyopo nyuma ya pesa (noti na sarafu) haionekani kirahisi kwa watu walio wengi. Ufahamu na uelewa mdogo juu ya maana pana ya pesa upo kwa watu wengi, na hali hii ni kwa wote waliokwenda shule na wale ambao hawakwenda kabisa. 

Ukweli ni kwamba “Pesa ni kitu chochote kinachowezesha watu kubadilishana vitu na huduma. Hapa ndo kuna mkanganyiko kwasababu watu wengi mpaka sasa wanaamini pesa ni kitu halisi na hivyo kusababisha wao kuweza kuiabudu na kuamini pesa kama inavyoonekana katika hali yake ya noti na sarafu. Mtazamo wa kuichukulia pesa kama kitu halisi, unawafanya walio wengi kuwekeza nguvu kubwa Katika kusaka/kutafuta pesa yenyewe kama ilivyo. Lakini wakisha ipata wanagundua kuwa, hitaji lao siyo makaratasi ya noti bali ni vitu na huduma mbalimbali hapo ndipo huzipeleka kwa wenye vitu na huduma, huku wakibakia tupu kabisa.

Katika kutafuta pesa kunakuwa na dhamira tofauti kati ya maskini na tajiri; “Watu maskini wanawekeza muda na nguvu yao kwa dhamira ya kutafuta pesa lakini watu matajiri wanawekeza muda, akili na nguvu yao kwa dhamira ya kutafuta “vitu na huduma”. Kwasababu maskini wengi waliamini kuwa mwisho wa utafutaji wao ni pesa, basi ndipo ugundua kuwa sio mwisho, kumbe mwisho wao ni kupata vitu na Huduma (chakula, dawa, mavazi; usafiri, elimu, utaalam, nguvukazi n.k.). Kwahiyo, pamoja na kutafuta pesa hiyo kwa kutumia nguvu kubwa na muda mrefu, mtu huyo ujikuta akilazimika kuzipeleka mwenyewe kwa tajiri ambaye wakati huo ana vitu na huduma fulani fulani. Kwa maana nyingine tunaweza kusema kuwa watu hawa wanaishi kwa kutafuta pesa na kisha kulipa bill! au madeni basi.

Mahitaji ya mwanadamu ni mengi sana na hayana kikomo, lakini pamoja na hayo, mahitaji haya yamegawanyika katika makundi makuu mawili: yaani “Vitu na Huduma”. Tunaposema “Vitu” inamaanisha vitu halisi na vinavyoshikika kama vile nguo, meza, komputa simenti, gari, simu, vyombo, spare, vitabu n.k); na tunaposema “Huduma” ni vitu ambavyo havishikiki navyo ni kama; usafiri, habari, utaalam, ulinzi na usalama, maombi, ufundi n.k. Kwahiyo, kutokana na ukweli huo hapo juu, ndiyo maana siku zote pesa itakwenda kule kulipo na vitu au huduma hakuna sehemu nyingine.

Kutokana na ukweli huu, ni wazi kwamba unapoona pesa imeingia mfukoni mwako, basi ujue kuna mtu ametuma pesa hiyo kufuata kitu fulani kwako, na iwapo huna kitu chochote ulichonacho basi hutapata pesa yoyote kwasababu hakuna kitu cha kufuata kwako. Sasa unachotakiwa kufanya leo ni kuanza kubadili swali ambalo watu wengi ujiuliza pindi wanapohitaji kupata pesa; swali lenyewe huwa ni hili hapa: “Nitapata pesa wapi?” na kwa kuwa wengi ujiuliza  swali hilo, ndiyo maana huishia tu! kutafuta pesa bila mafanikio.

 Iwapo utaendelea kujiuliza swali la nitapata pesa wapi ndivyo itakavyozidi kuwa vigumu kupata jibu ambalo litakuongoza kupata pesa. Kwahiyo, mtanzania mwenzangu ni wakati sasa wa kubadili swali lako kutoka “nitapata pesa wapi?” kwenda “Pesa itakuja kwangu kufuata nini?”. Na kila mara utakapojiuliza swali la pesa itafuata nini kwako, basi jibu jibu lake tu! litakuwa ndiyo pesa yenyewe kwa maana nyingine utaona watu wakibisha hodi mlangoni kwako, kwaajili ya  kukuletea pesa ambayo miaka yote umekuwa ukikimbia huku na huko kuitafuta bila mafanikio!. Sasa unachotakiwa kufanya ni utafiti katika mazingira yanayo kuzunguka na maeneo mengine unayoweza kuyafikia ili kutambua mahitaji, kero na changamoto zilizopo. Matokeo ya Utafiti yatakusaidia kubuni na kuzalisha vitu au huduma ili kukidhi mahitaji ya jamii husika, na ukifikia hapo ndipo utaona ndani muda mfupi watu wakituma pesa ili ikafuate vitu na huduma kutoka kwako.

Kwahiyo, uwanja ni wako wewe mtanzania unayetafuta mafanikio, kwani tuna imani kubwa sana kuwa unaweza kupata pesa nyingi, iwapo utakubatia na kuifanyia kazi falsafa hii ya “Pesa itakuja kwangu kufuata nini?”.
CREDIT:Maarifashop.blog
Next Post Previous Post
Bukobawadau