WASIFU WA MAREHEMU LUTENI KANALI BENEDICTA KITENGA
Marehemu Lt.Col.(Mst) Benedict Kulikila Kitenga
OFISI
YA MKUU WA MKOA WA KAGERA
TANZIA
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera inasikitika kutangaza kifo cha aliyekuwa
Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Lt. Col. Benedict Kulikila Kitenga aliyefariki
tarehe 20.04.2015 katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili.
Marehemu Lt.Col.(Mst) Benedict Kulikila Kitenga alizaliwa mnamo tarehe 15.06.1953
Ifakara Wilayani Kilombero katika Mkoa wa Morogoro.
ELIMU.
Marehemu Lt. Col. (Mst) Benedict Kulikila Kitenga alisoma shule ya Msingi Mafimba Wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro na kuhitimu
darasa la nne 1963, aidha alifaulu na kujiunga na darasa la tano shule ya Ilete Middle School iliyoko
katika Wilaya ya Ulanga na kuhitimu mwaka 1970.
Baada ya hapo marehemu alijiunga shule ya Sekondari Galanosi iliyoko
Mkoani Tanga na kuhitimu kidato cha nne mwaka 1974.
Mafunzo mengine aliyoyapata marehemu wakati wa uhai
wake ni mafunzo ya awali ya Uhandisi nchini Pakistani mwaka 1978. Vile vile marehemu alipata mafunzo ya Diploma
ya uhandisi nchini Ujerumani mwaka 1999.
KAZI ALIZOWAHI
KUFANYA.
Wakati wa Uhai wake marehemu aliweza kufanya kazi kama Mwanajeshi katika
Jeshi la Wananchi Tanzania na kuweza kupanda vyeo hadi kufikia Cheo cha Luteni
Kanali. Aidha akiwa katika Jeshi la
Wananchi Tanzania alikuwa; Mkuu wa kikosi Songea, Mkuu wa kikosi Ngerengere, Mkuu
wa mafunzo IMT-Monduli Mkoani Arusha.
Mwezi Machi, 2009 marehemu Lt. Col. (Mst) Benedict
Kulikila Kitenga aliteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. Jakaya Mlisho Kikwete kuwa Mku wa Wilaya Rorya iliyoko Mkoani Mara ambapo
alifanya kazi hadi tarehe 08 Machi, 2012 alipohamishiwa katika Mkoa wa Kagera
Wilaya mpya ya Kyerwa.
USHIRIKI WAKE
KATIKA SHUGHULI ZA KITAIFA.
Marehemu Benedict Kulikila Kitenga alishiriki vita ya Operesheni
Zimbabwe, Vita ya Operesheni Kagera
na Vita ya Operesheni Chakaza.
Akiwa Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa yafuatayo ni
machache kati ya mengi aliyoyafanya; Alikuwa Mwanzilishi wa Wilaya Mpya ya
Kyerwa mwaka 2012, Alisimamia utekelezaji wa mradi wa Umeme vijijini, na Aliimarisha
mahusiano mema kati ya nchi jirani za Rwanda na Uganda.
Aidha Marehemu Kitenga alisimamia na kuinua uchumi wa wananchi wa Wilaya
ya Kyerwa. Alikuwa mchapakazi hodari na
aliweza kusimamia na kupambana na wimbi la magendo ya kahawa na bati, pia alikuwa
ni kiungo mahususi kati Serikali Kuu na Halmashauri ya Wilaya, na alikuwa
kiongozi mwepesi, aliweza kutoa huduma wakati wowote.
UGONJWA HADI
MAUTI
Marehemu Lt. Col (Mst) Benedict Kulikila Kitenga alianza kuugua siku ya
Jumanne tarehe 14/04/2015 akiwa anasumbuliwa na maumivu ya moyo na miguu na
tarehe 15/04/2015 Jumatano jioni alilazwa katika hospitali Teule ya Nyakahanga
iliyoko katika Wilaya ya Karagwe.
Kutokana na hali yake kutokuwa nzuri siku hiyo hiyo Jumatato usiku wa saa 6.00 ililazimika kuhamishiwa katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera lakini hali yake iliendelea kutokuwa nzuri
ndipo tarehe 16/04/2015 siku ya Alhamisi alipewa rufaa na kupelekwa katika
hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dar es Salaam ambapo alikuwa akiendelea na
matibabu hadi mauti yaliyomkuta hapo tarehe 20/04/2015 saa 9.15 alasiri kutokana
na shinikizo la damu na kupooza.
SHUKRANI
Kwa niaba ya Uongozi wa Mkoa wa Kagera, napenda kutoa shukrani kwa
madaktari na Wauguzi wa Hospitali Teule ya Nyakaanga – Karagwe, Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Kagera na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dar es Salaam kwa
jitihada kubwa walizozifanya kuokoa maisha yake.
Mwisho kwa masikitiko makubwa napenda kutoa pole kwa familia, ndugu,
jamaa na marafiki pamoja na wananchi wa Wilaya ya Kyerwa na Mkoa wa Kagera kwa
ujumla, kutokana na msiba huu mkubwa.
Bwana
Ametoa, Na Bwana Ametwaa jina Lake Lihimidiwe.
AMEN.