Bukobawadau

BUNGENI LEO MAY 15,2015

Wabunge wameendelea kujadili bajeti ya ofisi ya waziri mkuu ambapo baadhi ya wabunge wamesema changamoto kubwa ya rais ajae ni kuhakikisha rasilimali za nchi zinakuwa mikononi mwa watanzania ili kujenga uchumi imara wa nchi badala ya kuwapa kipaumbele wageni.
Wakichangia bajeti hiyo katika kikao cha bunge kinachoendelea mjini Dodoma baadhi ya wabunge akiwemo mbunge wa Simanjiro Mh Christopher Olesendeka amesema mgombea yoyote wa chama chochote mwenye ndoto ya kuliongoza taifa la Tanzania ni lazima awaeleze watanzania namna ambavyo rasilimali zao zitabaki mikononi mwao.

Katika mjadala huo suala la ahadi za rais likaibuka ambapo wabunge wa vyama vyote wamelalamikia kitendo cha ahadi za rais kutokutekelezwa hadi leo ikiwemo ahadi ya meli ziwa Victoria ambayo aliwaahidi wananchi wakati wa kampeni zake pamoja na baadhi ya barabara ambazo ziliahidiwa kujengwa lakini hadi leo ahadi hizo hazijatekelezwa.

Wakati huohuo ndani ya mjadala huo serikali imetakiwa kuwa na mpango mkakati wa kuondoa matabaka yaliyojengeka nchini kati ya walionacho na wasiokuwa nacho ambayo yamekuwa yakiwakosesha wananchi haki zao za msingi ikiwemo huduma bora za afya na elimu huku baadhi ya wabunge wakiwataka wanasiasa kuhonga wananchi maendeleo badala ya fedha.
Next Post Previous Post
Bukobawadau