HALMASHAURI ZOTE NCHINI KUJENGEWA UWEZO WA KUKABILIANA NA MAAFA
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. Florens Turuka
akiongea na wajumbe wa wa Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa mkutano huo, Jijini Dar es Salaam,
tarehe 4 Mei, 2015.
Baadhi ya wajumbe wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Waziri Mkuu wakifuatilia mkutano
huo Jijini Dar es Salaam, tarehe 4 Mei, 2015. (wa kwanza) ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Regina Kikuli.
Baadhi ya wajumbe wa Mkutano wa Baraza la
Wafanyakazi la Ofisi ya Waziri Mkuu
wakifuatilia mkutano huo Jijini Dar es Salaam, tarehe 4 Mei, 2015.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. Florens Turuka
(mwenye tai nyeupe ) akiwa na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu mara baada ya
kufungua mkutano huo , Jijini Dar es Salaam, tarehe 4 Mei, 2015.
Na
Mwandishi Maalum
Serikali kupitia Ofisi ya
Waziri Mkuu imesema kuwa katika jitihada za kukabiliana na athari za maafa nchini,
imejipanga katika utekelezaji wa bajeti
ya mwaka 2015/2016 kujenga uwezo wa kukabiliana na maafa kwa Halmashauri zote
nchini kupitia mafunzo ya kukabiliana na maafa pamoja na kuandaa Mipango
ya Kujiandaa Kukabili Maafa katika Halmashauri
zote nchini.
Ofisi ya Waziri Mkuu
imeshazijengea uwezo wa kukabiliana na maafa
Halmashauri za mikoa mitano nchini kwa kuandaa Mipango ya kukabiliana na maafa pamoja
na kufanya zoezi la mezani la utekelezaji wa mipango hiyo kwa Halmashauri zake;
Mikoa hiyo ni; Dodoma, Shinyanga,
Simiyu, Kilimanjaro na Mtwara.
Akiongea mara baada ya
kufungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Jijini Dar
es Salaam, tarehe 4, Mei 2015, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. Florens
Turuka alisema kila Halmashauri inayo
majanga ambayo huisumbua mara kwa mara lakini kwa kutumia mafunzo na Mipango ya
kukabiliana na maafa zinaweza kuyakabili maafa zenyewe.
“Mafunzo ya maafa yanaweza
kuiwezesha jamii kupata elimu kuhusu
athari za ujenzi na kuendesha shughuli za uchumi katika maeneo hatarishi,
umuhimu wa usafi wa mazingira matumizi ya mbegu zinazostahimili ukame pamoja na
kuzuia ujenzi katika maeneo hatarishi hivyo Majanga ya mafuriko, Ukame, na
mlipuko wa kipindupindu ambayo yamekuwa
yakizisumbua Halmashauri zetu mara kwa mara yanaweza kukabiliwa kwa uwezo wa
Halmashauri husika” alisema Turuka.
Turuka aliongeza kuwa pamoja
na kuwa na mafunzo ya namna ya kukabiliana na maafa, aidha halmashauri
hazinabudi kulipa kipaumbele suala la
Kupunguza Athari za Maafa katika mipango
na programu za maendeleo.
“Halmashauri zinaweza
kupunguza utegemezi wa rasilimali za kukabili maafa, kwa kuondokana na mtazamo
wa kukabili maafa uliozoeleka ambao unatenganisha kwa kiasi kikubwa hatua za
utoaji wa misaada ya kibinadamu, kurudisha hali na shuguli za kawaida za
maendeleo. Kwa mantiki hii Halmashauri zetu nchini kupitia mafunzo ya maafa zitaweza kuondokana na
mtazamo huo uliozoeleka ” alisisitiza Turuka.
Aliongeza kuwa nchi yetu imekuwa ikikumbwa na majanga yakiwemo ya asili na
yanayosababishwa na vitendo vya binadamu. Katika kukabili maafa hayo yamekuwa
yakijitokeza mapungufu katika Halmashauri za hapa nchini, ikiwemo kutokuwepo
mipango madhubuti iliyoandaliwa ya kukabiliana na maafa mara yanapotokea.
Alifafanua kuwa kila
Halmashauri inaweza kuwa na uwezo wa kukabili maafa yanayoikumba kwa kuwa na
jamii yenye kuhimili maafa kwa Kuzuia, kupunguza athari na kujiandaa kama vipaumbele katika
menejimenti ya maafa katika ngazi zote. Ili kuhakikisha kunakuwa na jamii hiyo,
kila Halmashauri inapaswa kukaa na wadau wote katika halmashauri husika na
kuainisha maeneo ya kushughulikia kwa haraka na kuwa na mgawanyo bayana wa majukumu.