Bukobawadau

HATIMA YA MAKADA SITA WA CCM

Gazeti la Mwananchi Ijumaa May 22,2015
Dodoma. Kamati Kuu ya CCM, ambayo ndiyo inaanzisha mambo yote muhimu ya chama hicho, leo inakutana kuandaa ajenda za mkutano wa Halmashauri Kuu, huku suala linalosubiriwa kwa hamu likiwa ni hatima ya makada sita wanaotajwa kuwania urais ambao wanatumikia adhabu ya kuzuiwa kujihusisha na uchaguzi.
Kwa mara ya kwanza, CCM inakabiliwa na kazi ngumu ya kuamua hatima ya makada iliowafungiwa katika kipindi muhimu cha kuteua mgombea mpya wa urais kutokana na mwenyekiti wa sasa wa chama hicho, Jakaya Kikwete kutoweza kugombea nafasi hiyo kwa kipindi cha tatu kutokana na matakwa ya kikatiba.
Mmoja wa watu walio karibu na uongozi wa chama hicho aliiambia Mwananchi jana kuwa CCM imejikita zaidi katika kutafuta mwanachama atakayekipa ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu, lakini suala la makada waliofungiwa ambao baadhi yao wanapewa nafasi kubwa ya kupitishwa, halitachukua muda mrefu kulijadili.
Kikao hicho kitafanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri Kuu uliopo jengo la makao makuu ya CCM mjini hapa, maarufu kama White House mjini Dodoma.
Ukumbi huo una historia ya muda mrefu ndani ya CCM ya kutolewa kwa uamuzi mgumu katika matukio kadhaa ya kisiasa, ukiwamo ule ulioweka historia ya Aboud Jumbe kuingia akiwa Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, lakini akatoka bila cheo chochote mwaka 1984.
Pia kwenye ukumbi huo kulifanyika uamuzi wa mambo mengine makubwa, hasa nyakati za kuchuja wagombea urais au uongozi wa chama, mambo ambayo pia yanaweza kutokea katika vikao vinavyoanza leo au vya baadaye.
Alipoulizwa kuhusu kikao hicho jana, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema Rais Kikwete ataongoza kikao cha leo kilichopangwa kuanzia saa 4:00 asubuhi na kwamba maandalizi yamekamilika, huku baadhi ya wajumbe wakiwa wameshawasili.
Alipoulizwa kuhusu nini wategemee wanachama na wananchi, Nape alijibu kwa kifupi kuwa watarajie kuwa “CCM watatoka wakiwa kitu kimoja” kuliko inavyotarajiwa na wengi.
Hata hivyo, mbali na hofu kuhusu hatua za kinidhamu kwa wajumbe walioadhibiwa kwa kuanza kampeni mapema na kukiuka maadili, taarifa nyingine kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa vikao hivyo zilidai kuwa mkutano huo utajikita zaidi kuangalia utaratibu mzima wa kuchukua fomu za wagombea wote wa urais, ubunge na udiwani.
“Vikao hivi vinaangalia utaratibu tu wa jinsi ya kuchukua fomu na wala havitagusia suala la mchujo wa wagombea urais wala ubunge,” alisema mtoa taarifa huyo.
Kamati Kuu imetanguliwa na vikao vya mfululizo vya Sekretarieti na Kamati ndogo ya Kanuni.
Kamati ya Kanuni na Maadili ilitarajiwa kukutana jana usiku au leo asubuhi kabla ya Kamati Kuu.

Mtoa taarifa mwingine ambaye ni mjumbe wa NEC, alidokeza kuwa vikao hivyo havitajikita sana na uchujaji wa majina ya wagombea urais, badala yake kwa kuwa muda umekwenda, wameamua kushughulikia ratiba kwa ajili ya uchukuaji wa fomu za wagombea wa ngazi zote za uchaguzi ili nao wapate muda wa kwenda kutafuta wadhamini kabla ya mchujo.
Hata hivyo, mtoa habari mwingine kutoka ndani ya CCM, alisema licha ya kushughulikia masuala ya ratiba, kanuni na kuangalia ilani, bado suala la mchujo wa wagombea ni tata na huenda wakaangalia mgombea ambaye anaweza kukipa ushindi chama kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa huyo, hoja ya watangaza nia sita ya kukiuka kanuni za chama haitakipotezea muda, zaidi ya kuangalia nani anaweza kukipa chama ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Taarifa za ndani kutoka kwa mmoja wa wajumbe wa vikao hivyo vya juu vya CCM alidokeza kuwa kwa hali ya sasa ya kisiasa na joto linavyozidi kupanda hasa kasi ya Ukawa, CCM itafanya kama ilivyofanya kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 wakati Kamati ya Usalama na Maadili ilipokwenda Zanzibar ikiwa na faili la tuhuma za mmoja wa wagombea, lakini vikao vilijikita kwenye mgombea ambaye angekipa ushindi chama.
Kwa mujibu wa taarifa hizo mambo mengi hasa malalamiko ya ukiukwaji wa maadili wa baadhi ya viongozi ngazi za chini, yatamalizwa na Kamati Kuu na yale yatakayohitaji uamuzi wa mamlaka za uteuzi yatapelekwa Halmashauri Kuu.
Mtoa taarifa huyo alisema suala la Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Paul Makonda na makada wawili CCM, Mgana Msindai ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho mkoani Singida, na John Guninita, ambao wamefungua kesi ya madai mahakamani, linaweza kuibua mjadala.
Hivi karibuni Nape alikaririwa akisema kuwa chama hicho katika kushughulikia matatizo yote yaliyojitokeza kitatumia kanuni zake na hakuna atakayeonewa.
“Nasisitiza ni kanuni na wala si mimi, nasisitiza pia kuwa sijazuia watu kuchukua fomu bali chama kinafuata kanuni,” alisema.
Alisema kada yeyote wa CCM akiamua kufanya kampeni kabla ya muda ataadhibiwa, lakini akisubiri hana hatia kwani kinachongomba ni kanuni.
Maelezo hayo ya Nape yalikuwa yanalenga uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM kuwafungia kwa miezi 12 vigogo wa chama hicho uliotolewa Februari mwaka jana kwa kuanza kampeni kabla ya wakati na kikiuka maadili ya chama.
Wakati huo huo, hoteli na nyumba za kulala wageni zimejaa na hiyo kufanya baadhi ya wageni wanaoingia mkoani hapa kulazimika kutafuta malazi nje ya mji.
Uchunguzi wa gazeti hili uliofanywa wa nyumba za kulala wageni katikati ya mji umebaini kuwa wageni waliojaza nyumba hizo ni wajumbe na wapambe.
Next Post Previous Post
Bukobawadau