MASHINDANO YA UMISETA MKOANI KAGERA YAZINDULIWA RASMI
Mkoa wa Kagera umeanza rasmi
mashindano ya UMISETA yanayowashirikisha wanafunzi wa shule za sekondari kutoka
katika Halmashauri zote za Wilaya na
Manispaa ya Bukoba katika mkoa wa Kagera.
Mashindano hayo yalifunguliwa
jana tarehe 21/05/2015 na Afisa Elimu Mkoa wa Kagera Bw. Aloyce Kamamba katika
viwanja vya Chuo cha ualimu Katoke Wilayani Muleba.
Akifungua mashindano hayo Bw.
Kamamba aliwaasa wanafunzi wanamichezo ambao wamejumuika katika chuo cha Katoke kwa kushindana katika michezo mbalimbali
kutumia fursa hiyo kuonesha vipaji vyao kwani kwa sasa michezo ni ajira.
Pia Bw. Kamamba aliwaasa
wanamichezo hao kuhakikisha wanacheza na kushindana kirafiki bila kucheza kwa
kuumizana na kuhakikisha waamuzi wanachezesha bila upendeleo.
Walimu wanaohusika kuchezesha na
kusimamia michezo hiyo katika mashindano hayo ya UMISETA mkoa pia nao walihaswa
kuhakikisha wanasimamia nidhamu na kuhakikisha wanachagua wachezaji wazuri
ambao watakwenda kushindana na kuonyesha vipaji vyao pia kuleta makombe ya
ushindi.
Aidha, Afisa Michezo wa Mkoa wa
Kagera Bw. Kepha Elias akitoa ratiba ya mashindo alisema kuwa mara baada ya
mashindano hayo kukamilika ngazi ya mkoa timu zitakazokuwa zimechaguliwa
zitapiga Kambi kwa siku tatu ili kufanya maadnalizi ya kushiriki mashindano ya
Kanda.
Bw. Kepha alisema kuwa mshindano
ya Kanda yatafanyika mkoani Geita ambapo mara baada ya hapo wachezaji
watakaokuwa wamechaguliwa wataelekea mkoani Mwanza kushiriki mashindano ya
UMISETA kitaifa mkoani humo.