TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU TAARIFA YA UKAGUZI WA FEDHA ZA SERIKALI 2013/2014
·
Upotevu
wa shilingi trilioni 1.151 Serikali kuu pekee hauvumiliki.
·
Makusanyo
yote yaliyotokana na kuongezeka kwa kodi 2013/14 yameyeyuka
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepokea
kwa masikitiko makubwa taarifa za ufisadi wa kutisha uliofanyika kwenye
matumizi ya fedha za umma kama ilivyobainishwa kwenye ripoti za ukaguzi wa
fedha kwa mwaka 2013/2014 zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG)
Wakati chama kinaendelea kuzifanyia uchambuzi wa kina
ripoti zote tano ili kuweka hadharani ubadhirifu mkubwa ambao mwingi hujificha
kwenye maelezo ya kitaalam, tunapenda kutoa taarifa ya awali kama ifuatavyo;
·
Wizara
tatu , Trilioni 1.151 zimepotea
Katika uchambuzi wetu wa
awali tumebaini kuwa kwa upande wa serikali kuu pekee zaidi ya shilingi trilioni 1.151 zimepotea au kuliwa na
wajanja walioko serikalini , kiwangio hiki ni sawa na asilimia 5.231 ya bajeti yote ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha
2015/16 inayoendelea kujadiliwa huko Bungeni Dodoma.
Ripoti ya CAG iliyotolewa jana inaonyesha kuwa katika Serikali
Kuu, Wizara tatu tu ambazo tumezifanyia Uchambuzi mpaka sasa zimepotea kiasi
cha shilingi 1.151 Trilioni , wizara hizo ni;
i.
Wizara ya Fedha (TRA) , Fedha zilizopotea
kutokana na bidhaa ambazo zilipaswa kuuzwa nje ya Nchi ila kutokana na uzembe
zikauzwa ndani ya nchi bila kulipiwa kodi zilikuwa jumla ya shilingi 836 Bilioni.
ii.
Ofisi ya Waziri Mkuu , kitengo kimoja cha
maafa zilipotea jumla ya shilingi 163
Bilioni.
iii.
Wizara ya Ujenzi , ziliibwa jumla ya shilingi 252 Bilioni.
·
Bajeti
ya mwaka 2013/14 Mapato yote ya ongezeko la kodi yameyeyuka:
Mwaka 2013/14 yalifanyika maboresho ya sheria mbalimbali za kodi wakati
wa Bunge la bajeti kodi ambazo kimsingi zilimwongezea mwananchi mzigo mzito wa
kulipia kodi hizo kwa ajili ya kuongeza mapato ya Serikali na ili kuiwezesha
serikali kuwahudumia wananchi wake .
Pamoja na ongezeko hilo la kodi
,ukweli mchungu ni kuwa fedha yote iliyokusanywa kutokana na ongezeko la kodi
mbalimbali katika mwaka wa fedha 2013/14
imepotea yote katika wizara
tatu tu za serikali kutokana na vitendo vya kifisadi, na hii ni kwa mujibu wa taarifa CAG .
Kodi zilizorekebishwa na mapato yake ni kama ifuatavyo;
a. Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA
148; kilipatikana kiasi cha sh.48.977bilioni
b. Sheria ya Kodi ya Mapato,
SURA 332;kilipatikana kiasi shilingi 131.686
bilioni
c. Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;
kilipatikana kiasi cha shilingi 510.017
bilioni
d. Sheria ya Ushuru wa Mafuta,
SURA, 220; kilipatikana kiasi cha shilingi 155.893bilioni
e. Sheria ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Stadi, SURA 82 ;kilipatikana kiasi cha shilingi 28.213 bilioni
f. Sheria ya Usalama Barabarani,
SURA, 168; kilipatikana kiasi cha shilingi 19.710
bilioni
g. Sheria ya Petroli (Petroleum Act) SURA,
392;kilipatikana kiasi cha shilingi 123.725
bilioni
Hali hiyo ilifanya marekebisho yote ya sheria za Kodi
zilizofanywa katika mwaka huo wa fedha kuiwezesha serikali kukusanya jumla ya shilingi 1.018 Trilioni katika mwaka wa
Fedha 2013/2014 na hii ni kwa mujibu wa taarifa ya Hansard ya Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Hali hii haikubaliki na haivumiliki hata kidogo. Hapa
tumezungumzia Wizara tatu tu za serikali kuu bado wizara 30 na idara mbalimbali
za Serikali ikiwa ni pamoja na Halmashauri na Taasisi na Mashirika ya Umma.
Ripoti hizi zimezidi kudhihirisha kwa mara nyingine kuwa
matatizo yanayowakabili Watanzania ikiwa ni pamoja na umaskini, maradhi, ujinga
yanaendelea kudumu kwa sababu watawala wa Serikali ya CCM wameamua yaendelee
kuwepo kwa kukumbatia adui wa nne ambaye ni ufisadi.
Ripoti hizo za CAG ambazo zimeanika ufisadi katika
maeneo yaliyokaguliwa ikiwemo Serikali
Kuu, Serikali za Mitaa, mashirika ya umma na miradi ya maendeleo, kwa mara
nyingine zimedhihirisha wazi kile ambacho CHADEMA kimekuwa kikisema kwa muda
mrefu kwamba ufisadi huu unaoendelea kulitafuna taifa na kuwafanya Watanzania
wazidi kuwa maskini ni matokeo ya kushindwa kwa sera, mikakati na mipango ya CCM.
Wakati kasi ya ufisadi inaongezeka kutoka mwaka hadi
mwaka kwenye Serikali ya Rais Jakaya Kikwete chini ya usimamizi wa CCM, ndivyo serikali
hiyo hiyo inaongeza kasi ya kushindwa kusimamia UWAJIBIKAJI ambayo ndiyo moja
ya nguzo muhimu katika kuhakikisha matumizi ya fedha za umma yanaonekana katika
kuboresha maisha ya wananchi hususan kuweka fursa za kujitafutia maendeleo ya
mtu mmoja mmoja na hatimaye ustawi wa jamii nzima.
Ufisadi huu hauvumiliki tena. Watanzania wasikubali
kuendelea kubeba mizigo ya watawala walioshindwa kutekeleza wajibu wao. Hali ya
siasa inazingirwa na sintofahamu kubwa. Uchumi unazidi kuyumba. Kijamii, maisha
yazidi kuwa magumu na walioko madarakani wamelewa madaraka. Msamiati wa
UWAJIBIKAJI haumo vichwani mwao tena.
Ni mwaka wa Watanzania kuamua kuachana na ufisadi huu.
Imetolewa
leo Jumatano, 20 Mei, 2015;
Tumaini
Makene
Mkuu
wa Idara ya Habari na Mawasiliano- CHADEMA