WADAU WA KAHAWA MKOANI KAGERA WAPEWA CHANGAMOTO YA KUANZISHA MNADA KAHAWA WA KAGERA ILI KUBORESHA BEI KWA WAKULIMA
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. John Mongella atoa changamoto ya kuinua
ubora wa zao la kahawa na kuimarisha bei yake ili kumuinua mkulima wa Kagera, wakati
akifungua Kikao cha wadau wa Kahawa kanda
ya Kagera kutoka katika Halmashauri zote za mkoa wa Kagera kilichofanyika
katika mkoani hapa Mei 8, 2015.
Mkuu wa Mkoa Mhe. Mongella katika
mkutano huo aliwataka wadau wa kahawa kutoka katika mkoa wa Kagera kuachana na
mifumo ya kizamani ambayo imekuwa wimbo wa kila siku katika utatuzi wa
kudhibiti magendo ya kahawa na kuimarisha bei kwa wakulima ili kuinua uchumi wa
mkoa na taifa.
Wadau wa kahawa wa Kagera
walipewa changamoto ya kuanzisha mnada wa kahawa yao ya Kagera badala ya
kutegemea mnada wa Moshi mkoani Kilimanjaro ambao unaongeza gharama na
kumpunguzia mkulima bei jambo linalowafanya wakulima kuuza kahawa kwa njia za
magendo.
Aidha Mhe. Johna Mongella
aliishangaa Bodi ya Kahawa Tanzania kukata kilo 10 kila kilo 60 kutoka kwa
mkulima kwa ajili ya kupeleka kwa wanunuzi kupima ubora wa kahawa ambapo
alisema robo kilo inatosha sana kupima ubora lakini Bodi ya Kahawa imekuwa
ikiwadhoofisha wakulima bila sababu.
Pia Mhe. Mongella aliwataka
wakulima kubadilika na kuanzisha mashamba mapya
kwa kupanda miche yenye ubora na inayoweza kuzalisha kahawa kwa wingi
kuliko ilivyo sasa ambapo mashamba mengi yamekuwa kama misitu na miche ni ya
zamani nambapo hayahudumiwi ipasavyo ili kuzalisha kahawa bora.
Kwa upande wa wadau wa kahawa katika
kikao hicho walizilalamikia Halmashauri
za Wilaya kwa kutoza kiwango kikubwa cha tozo au ushuru katika zao la kahawa
jambo ambalo linapelekea kushusha bei ya kahawa hasa kwa mkulima.
Kahawa kavu
Wadau hao waliziomba Halmashauri
za Wilaya kupunguza tozo au ushuru
katika zao la kahawa aidha waliiomba serikali pia kupunguza viwango vya
fedha zinazotozwa katika leseni na kupunguza wingi wa leseni ambazo zimekuwa
kero kwa wanunuzi wa kahawa na kupelekea gharama kwenda kwa wakulima.
Changamoto kubwa iliyojitokeza
katika kikao hicho ni kuhusu magendo ya kahawa mkoani Kagera ambapo wakulima
walio wengi wanauza kahawa yao kwa njia za magendo na sababu kubwa ikiwa ni bei
ndogo inayotolewa na wanunuzi wa hapa nchini lakini nchi jirani wananunua kahawa
kwa bei ya juu.
Wanunuzi wa Kahawa wakizungumzia
kuhusu kutoa bei ndogo ya kahawa walisema kuwa inatokana na mwenendo wa bei
katika soko la dunia ambapo bei ikiwa nzuri na wao wananunua kahawa kwa
wakulima kwa bei nzuri ambayo inayoridhisha na bei ya soko ikishuka na wao wananunua
kulingana na bei hiyo.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa
wadau kuweka maazimio ya kuhakikisha kila mdau wa kahawa anahusika katika
kudhibiti uuzaji wa kahawa kwa njia za magendo ili kuingiza mapato katika
Halmashauri za mkoa wa Kagera na taifa kwa ujumla kuliko kunufaisha uchumi wan
chi jirani.