WAKULIMA WA KAMACHUMU WAJIKOMBOA NA MUCOGA
Mkuu wa wilaya Muleba katikati mwenye Kaunda suti na viongozi wa MUCOGA
Mkuu wa wilaya Muleba, Francis Isack, akitoa hotuba ya uzinduzi
Muhandiki akiongea kwenye ufunguzi wa MUCOGA
Wana MUCOGA Muhandiki wa tatu toka kushoto waliokaa
Mkuu wa wilaya Muleba, Francis Isack, akitoa hotuba ya uzinduzi
Muhandiki akiongea kwenye ufunguzi wa MUCOGA
Wana MUCOGA Muhandiki wa tatu toka kushoto waliokaa
Na Prudence Karugendo
HATIMAYE kilio cha siku nyingi cha wakulima wa zao la
kahawa mkoani Kagera kimeelekea kufika mwisho baada ya baadhi ya wakulima
kubuni njia zao wenyewe za kujikomboa kwenye lindi la manyanyaso na hujuma.
Ubunifu huo wa kujikomboa toka kwenye makucha ya mfumo onevu wa kuwageuza
watumwa, kwa maana ya kuwalazimisha kuzalisha wasichonufaika nacho,
umeshangiliwa na wakulima wote wa kahawa mkoani Kagera.
Sanasana
kilichofanya ubunifu huo ukashangiliwa kwa furaha sana na hata wakulima ambao
hawajajiunga na ubunifu wenyewe ni mwanga mzuri uliojionyesha wa juhudi za
wakulima hao, wazalishaji wa kahawa, walizokuwa wakizifanya kutaka kuyaona
manufaa ya zao lao hilo kuu la kibiashara kwa miongo nendarudi bila kuyaona
matunda yake ndani ya mfumo mkongwe unaotumika kwa sasa wa ushirika, ambao
kusema ukweli ni kama umekwama na kushindwa kuwakwamua wakulima kiuchumi.
Wabunifu wa
njia hiyo ya kujikomboa kiuchumi ni wakulima wa kahawa wa Kamachumu, wilayani
Muleba, Kagera, wakiongozwa na Archard Felician Muhandiki, aliyekuwa mwakilishi
wao katika chama kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd. lakini baadaye
akafanyiwa mizengwe ya kifisadi na kuondolewa kwenye uwakilishi wake ili kuzima
kelele zake za kutaka kuuwajibisha uongozi mbovu wa chama hicho cha ushirika.
Baada ya
mizengwe hiyo iliyofanyika kwa nguvu kubwa zilizowezeshwa na kipato cha
ushirika, ambacho lakini hakitumiki kuwawezesha wanaushirika wenyewe kiuchumi,
ndipo Muhandiki, kwa kushirikiana na baadhi ya wakulima aliokuwa akiwawakilisha
katika ushirika huo, walipoamua kubuni njia mbadala za kulishughulikia zao lao
la kahawa nje ya mfumo wa ushirika.
Wakabuni
Jumuiya ya Wazalishaji wa kahawa wa Muleba na kuipa jina la Muleba Coffee
Growers Association (MUCOGA), na kisha kuitafutia usajili katika wizara ya
Mambo ya Ndani chini ya kitengo cha Vyama vya Kijamii na baadaye kupata leseni
ya kufanya biashara ya kahawa.
Wameamua
kufanya hivyo ili kuondokana na urasimu wa ushirika unaoonekana unawalazimisha wakulima
kuutumikia mfumo huo bila wao kupata chochote.
Baada ya
taratibu zote kukamilika, uzinduzi rasmi wa MUCOGA ulifanyika tarehe 29 April,
2015, kwa baraka za mkuu wa wilaya ya Muleba, Francis Isack, ambaye ndiye
aliyekuwa mgeni rasmi katika sherehe hiyo. Sherehe hiyo ya uzinduzi
ilifunguliwa na mwenyekiti wa muda wa MUCOGA, Dauda Mahamud.
Katika
nasaha zake za uzinduzi wa MUCOGA, mkuu huyo wa wilaya ya Muleba, Francis
Isack, alikumbusha kwamba mikakati ya kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ilipata
Baraka za mtangulizi wake wilayani humo, na yeye akapata bahati ya kuizindua.
Akasema kwamba hilo ni lazima linamfurahisha mtangulizi wake kule aliko,
kwahiyo akawaomba wana MUCOGA kuiendeleza jumuiya hiyo ili ishamiri kusudi hata
yeye atakapokuwa amehamishiwa kwingine akiendelea kusikia mafanikio yake awe
anajivunia kushamiri kwake, kwamba ni yeye aliyeizindua kama anavyofurahi
mtangulizi wake aliyeuanzisha mchakato wa kuwepo kwake.
Alisema
kuwepo kwa jumuiya inayojihusisha na kitu ambacho tayari kinashughulikiwa na
chombo kingine ni jambo jema kwa vile kunaleta ushindani, akaongeza kwamba
ushindani ndio unaochochea maendeleo ya eneo lolote. “Sababu huyu akisema
niboreshe hivi na huyu anasema nizidishe ubora kwa njia hii, kinachopatika
katika ushindani wa aina hiyo ni maendeleo ya sehemu zote mbili”, akasema
Isack.
Akaongeza
kwa kusema kwamba uwepo wa MUCOGA ni lazima utawapatia tija hata wanaushirika
wa KCU (1990) Ltd. kwa vile chama hicho kitajitahidi kuwanufaisha wanachama
wake ili kiendelee kuwepo. Kwamba chombo kikibaki kimoja kinajisahau na
kubweteka kutokana na kukosa changamoto na hivyo kuyafanya maendeleo kuyeyuka.
“Nawaomba
muendeleze moyo huu wa kijumuia bila mifarakano ili kuyafikia malengo, yaani
mafanikio mliyoyakusudia, yaliyo mfano wa kuigwa”, alisema mkuu huyo wa wilaya ambaye anaonekana
bado ni kijana, tena anayependelea kujichanganya sana na wananchi wa wilaya
yake, ikizingatiwa kuwa ana muda mfupi tangu ahamishiwe kwenye wilaya hiyo ya
Muleba.
Deocres
Rutabana, katibu mkuu wa muda wa MUCOGA, alisema katika risala aliyoisoma mbele
ya mgeni rasmi, kwamba MUCOGA ni kwa ajili ya wakulima wote wa kahawa wilayani
Muleba wanaojisikia kujiunga na jumuiya hiyo. Pia akaongeza kwamba MUCOGA
imefungua milango yake hata kwa wakulima wa kahawa wa nje ya mipaka ya wilaya
ya Muleba ambao wanayaona manufaa ya muundo huo wa kulishughulikia zao la
kahawa na kuwapa tija wazalishaji wake.
Vilevile
walikuwepo waalikwa toka chama cha ushirika cha Magata, Muleba, kilichojitenga
na chama kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd. ikiwa ni kuonyesha kwamba
pamoja na MUCOGA kujiendesha nje ya utaratibu wa ushirika bado haina uhasama na
ushirika.
Kiongozi wa
msafara wa waalikwa hao toka Magata, Enock Babu, katika salaamu zake toka kwa
wanaushirika wa Magata aliwashauri wana MUCOGA kuweka pembeni itikadi za
kisiasa na kidini na kuangalia tu suala moja la kiuchumi. Akasema kwamba wana
MUCOGA wahakikishe jumuiya yao inawafikisha kwenye malengo yao ambayo ni
mafanikio ya kiuchumi bila kugawanywa na mambo ya itikadi za kisiasa wala imani
za kidini.
Naye muasisi
wa wazo la kuwa na jumuiya hiyo ya wazalishaji wa kahawa wa Muleba, Archard
Felician Muhandiki, aliamua kuitumbuiza hadhara iliyokuwa kwenye uzinduzi huo
kwa wimbo uliokuwa na maneno haya; “Ekyomwantumile nakileta, Kihanja Ihangiro milembe”
wenye maana ya kwamba (mlichonituma nimekileta, Kihanja Ihangiro kote mambo
salama. Kihanja ndiko liliko eneo la Kamachumu, au kwa ramani ya kisiasa
likiitwa Muleba Kaskazini. Ihangiro, kwa
ramani ya kisiasa ndiko Mulena Kusini.
Katika
kuonyesha jinsi walivyojipanga, wana MUCOGA wameanzisha salaamu yao mpya iliyo
tofauti na ile ya wanaushirika wa KCU (1990) Ltd., inayosema (ushirika mwitikio
wake ukiwa ni pamoja tujenge uchumi). Salaamu ya MUCOGA inasema (MUCOGA
mwitikio wake ukiwa ni tujenge uchumi imara).
Baada ya
uzinduzi huo uliofana sana watu wa maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kagera wakaanza
kupiga simu kuulizia utaratibu wa kujiunga na jumuiya hiyo, kitu kinachoonyesha
kuwa wamechoshwa na utaratibu unaotumika kulishughulikia zao lao la kahawa kwa
sasa.
Kwa mujibu
wa katiba ya jumuiya hiyo uongozi uliopo kwa sasa ni wa mpito kwa ajili ya
maandalizi ya jumuiya hiyo mpya. Baadaye utaitishwa uchaguzi mkuu kwa ajili ya
kuwapata viongozi wa kudumu kulingana na muda uliowekwa na katiba hiyo.
0784 989 512