Bukobawadau

UFUNGUZI WA KAMBI YA WATOTO (ARIEL CAMP) ILIYOANDALIWA NA SHIRIKA LA AGPAHI

Muonekano wa Meza kuu katika ufunguzi wa kambi ya watoto (Ariel camp) wanaopata huduma katika vituo mbalimbali vya afya vinavyosaidiwa na shirika lisilo la kiserikali la AGPAHI linalofanya kazi katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu. Ufunguzi huo ulifanyika katika hotel ya ELCT Mjini Bukoba.
Mkurugenzi wa  shirika lisilo la kiserikali la AGPAHI Bw. Laurean Bwanakunu akiongea katika ufunguzi huo uliofanyika katika hotel ya ELCT  Mjini Bukoba siku ya jana June 15,2015
 Sehemu ya watoto wakimsikiliza Mkurugenzi.
Ifuatayo ni hotuba fupi iliyotolewa na  Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la AGPAHI, Bw. Laurean Bwanakunu (aliyeko pichani)


Ndugu,
·        Mgeni Rasmi, Mganga Mkuu (M) - Kagera,
·        Madaktari kutoka Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania,
·        Meneja wa Mradi wa AGPAHI – Shinyanga & Simiyu,
·        Wafanyakazi wa AGPAHI,
·        Walezi wa Watoto,
·        Wadau mbalimbali wa Afya na Haki za Watoto,
·        Watoto wa Kambi ya Ariel, Waandishi wa Habari,
·        Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana.
Habarini za asubuhi !
Ndugu Mgeni rasmi, Awali ya yote napenda kutoa shukrani kwako kwa kuacha shughuli zako na kuja kujumuika na sisi hapa kwenye Kambi ya Ariel (Ariel Camp). Tunasema asante sana!

Pia napenda kuwashukuru sana walezi waliokuja na watoto toka Simiyu na Shinyanga. Vile vile napenda kuwashukuru wafanyakazi wenzangu wa AGPAHI na wadau wengine kwa jitihada zao za hali na mali katika kuandaa kambi hii ya watoto. Hii ni mara ya kwanza kwa AGPAHI kuandaa kambi hii katika mkoa wa Kagera, tunafarijika sana kuwa hapa.

Ndugu Mgeni rasmi, Shirika la AGPAHI ni shirika lisilo la kiserikali linaloendeshwa na watanzania na watanzania wenyewe ndio sisi hapa. Kuanzishwa kwa shirika linaloendeshwa na watanzania ilitokana na dira ya serikali ya Tanzania na ile ya wafadhili  yaani serikali ya Marekani kutaka wazawa (serikali pamoja na mashirika yasiyo ya serikali) kuendesha miradi mbalimbali inayoshughulikia masuala ya VVU na UKIMWI na masuala ya afya ya mama na mtoto ili kuwa na miradi endelevu.

Shirika letu linatoa huduma katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Geita. Huduma zitolewazo ni pamoja na tiba na matunzo, kuzuia maambukizi ya virusi toka kwa mama kwenda kwa mtoto na huduma za uzazi wa mpango.  Hadi mwezi Machi mwaka huu, AGPAHI imeweza kuandikisha wateja 96,638 (wanaume 34,342 na wanawake 55,975) kwenye huduma za matunzo ambapo 6,321 ni watoto walio chini ya umri wa miaka 15 na hii sawa ni asilimia 7.

Vilevile AGPAHI imeweza kuwaanzishia dawa wateja wapatao 63,048 (wanaume 21,555 na wanawake 36,969) kwenye huduma za tiba ambapo watoto ni 4,524 ambayo ni sawa na asilimia 7.

Dira ya shirika ni kuhakikisha tunatokomeza maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa watoto na kuondoa UKIMWI kwa watoto. Katika kutekeleza azma hiyo shughuli mbalimbali zinatekelezwa ikiwa ni pamoja na kuwapatia watoto huduma za matunzo na matibabu pamoja na huduma za kisaikolojia. Katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu, kuna jumla ya watoto 694,454 kati yao watoto 6,321 wanaishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Mgeni Rasmi, shirika la AGPAHI lilianza huduma za malezi na kuwakutanisha watoto katika vikundi vidogo vidogo baada ya kuanzishwa kwake. Vikundi hivi vipo katika vituo vya kutolea huduma za afya ambapo hadi sasa tuna jumla ya vikundi vipatavyo 35 vyenye jumla ya watoto 1,541.

Kutokana na kuundwa kwa vikundi hivyo, AGPAHI iliweka utaratibu wa kuendesha kambi ili kuwakutanisha watoto kutoka kwenye vikundi mbalimbali kwa lengo la kujifunza kuhusu afya na stadi za maisha na pia kubadilishana uzoefu. Kambi hizi pia huwajenga watoto na kuwafanya mabalozi wa huduma za watoto katika jamii. Kambi hizi za watoto zimekuwa zikifanyika mara moja kwa mwaka; ambapo kwa mwaka huu tumeweza kufanikisha kuwa na kambi mbili. Hii inamaanisha watoto wengi zaidi wanapata nafasi ya kushiriki kwenye kambi.

Kambi hii ni ya tano kufanyika na kauli mbiu ya kambi hii ni “AGPAHI inajali watoto wakue na kuishi kwenye matumaini chanya.” Kambi za awali zilifanyika katika mikoa ya Pwani, Mwanza na Kilimanjaro.

Mgeni Rasmi, Kambi hii itafanyika kwa muda wa siku tano, leo ikiwa ni siku ya kwanza. Kambi ina idadi ya watoto wapatao 57 wenye umri wa kuanzia miaka 8 hadi 17.  Watoto hawa wanatoka katika vituo mbalimbali kwenye halmashauri zote za mikoa ya Shinyanga na Simiyu.

Katika kipindi hiki cha wiki moja, watoto wataweza kujifunza umuhimu wa vikundi vya watoto, namna ya kujenga tabia ya kutafuta matibabu mbalimbali, umuhimu wa kujitambua, kufuatilia matibabu, ufuasi wa dawa, elimu ya ujana na VVU, jinsi ya kuwasiliana, stadi za maisha na huduma ya kisaikolojia.

Pamoja na mafunzo watakayojifunza katika kambi, watoto pia watafanya matembezi na kuona mto Kagera, Kagera sugar factory, makumbusho vita vya IDD AMIN na mpaka wa Tanzania na Uganda.

Ndugu mgeni rasmi, napenda kutoa shukrani zetu kwa  Watu wa Marekani kupitia shirika lao la CDC ambao ndio wahisani wa kambi hii.   Hata hivyo tuna wafadhili wetu wengine kama EGPAF, UNFPA na USAID ambao nao wanatusaidia katika kazi zetu. Pia shirika letu linafanya kazi kwa karibu sana na ofisi ya Waziri Mkuu –TAMISEMI na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA!
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Bw. Herman Kabirigi (Afisa Afya wa Mkoa wa Kagera) ambaye ndiye alikuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa kambi ya siku tano ya watoto (Ariel -Camp ) inayofanyika katika hotel ya ELCT  Mjini Bukoba akihutubia. 
Madaktari kutoka Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania - Dr. Festo Manyama na Dr. Maimuna Ahmed katika hali ya Usikivu.
Bwana Jasson Lwankomezi ambaye ni mtaalam wa Saikolojia akitoa maelezo kwa watoto hao.
Bi Cecilia Yona akitoa ufafanuzi wakati wa kuanza kambi.
 Watoto wakiwa tayari kujibu maswali .
 Zoezi la utambulisho likiendelea
 Pichani kushoto ni Dr. Scott Amos, Dr Maimuna Ahmed na Dr. Festo Manyama wakati wa utambulisho.
 Bw. Milton Kuhoyelwa ambaye ni mhudumu wa afya kutoka Maswa akisalimia washiriki.
 Muendelezo wa matukio wakati wafanyakazi wa AGPAHI na walezi wa watoto wakiwajibika
 Dr. Festo Manyama akitolea jambo ufafanuzi
Bw. Gastor Njau akizungumza.
Mr. Mugisha akiwajibika katika kupata matukio kwa ajili ya kumbukumbu.

Wafanyakazi wa AGPAHI - Bi Jane Shuma na Bw. Emilian Ng'wandu.
Muonekano wa Menu husika.
Mmoja ya watoto akipata huduma ya Chakula
Waalikwa wakiendelea kupata huduma ya Chakula katika hotel ya ELCT Bukoba .
Taswira mbalimbali wakati watoto  wakishiriki michozo.
Watoto wakiwa katika michezo.
Kwenye viwanja vya Gymkhana Mjini Bukoba watoto hao wakionyesha uwezo wao katika kucheza mpira wa miguu.
Muendelezo wa matukio mbalimbali katika picha.

IFUATAYO NI  HOTUBA FUPI YA MGENI RASMI KATIKA UFUNGUZI WA KAMBI YA WATOTO (ARIEL CAMP) ILIYOFANYIKA ELCT BUKOBA HOTEL - 15/06/2015

·        Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI,
·        Meneja Mradi wa AGPAHI – Shinyanga & Simiyu.,
·        Madaktari kutoka Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania,
·        Wafanyakazi wa AGPAHI,
·        Walezi wa watoto
·        Watoto wa Kambi ya Ariel,
·        Waandishi wa Habari,
·        Wageni Waalikwa,
·        Mabibi na Mabwana 
Napenda kuushukuru uongozi wa Shirika la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) kwa kuandaa kambi hii ya watoto hapa Bukoba na kunikaribisha kuwa Mgeni Rasmi kwenye ufunguzi wa kambi hii.
Ninayo furaha kubwa sana kuwa nanyi hapa na kwa niaba ya Idara ya Afya ya Mkoa wa Kagera. Nawakaribisha sana mkoani kwetu!
Nimefahamishwa kwamba, shirika la AGPAHI linafanya huduma hizi za kisaikolojia kwa watoto katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011.
Nawapongeza kwa kuendelea kuunda vikundi vidogo vidogo vya watoto katika vituo vya kutolea huduma za afya ambapo hadi sasa, mmenieleza mna jumla ya vikundi vipatavyo 35 (vyenye watoto 1,541). Nafurahi pia kusikia kuwa wilaya zote za mikoa ya Shinyanga na Simiyu zimewakilishwa katika kambi hii. Hii inaashiria kuwa AGPAHI inatambua umuhimu na thamani ya huduma za kisaikolojia kwa watoto.
Pia nimefahamishwa kuwa katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu, kuna jumla ya watoto 694,451,kati yao watoto 6,321 wanaishi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Nimefarijika kusikia kwamba, kutokana na vikundi hivi vya huduma za kisaikolojia kwa watoto, AGPAHI ilifanya juhudi za kuanzisha kambi za watoto ambazo hufanyika mara mbili kwa mwaka. Kambi hii ya Kagera ni ya tano kufanyika chini ya uratibu wa shirika la AGPAHI. Kambi mbili za mwanzo zilifanyika mkoani Mwanza na kambi ya tatu na ya nne zilifanyika mkoani Kilimanjaro. Kambi hizi huwakutanisha watoto ili kujifunza mambo mbali mbali kuhusu afya, stadi za maisha, kupata ushauri wa kisaikolojia kutokana na changamoto wanazokutana nazo na pia huduma za kitabibu kutoka kwa madaktari bingwa wa watoto katika kipindi cha kambi. Pia, kambi hizi huwajenga vijana na kuwafanya mabalozi wa huduma za watoto katika jamii.
Vilevile, naomba kuchukua fursa hii, kuwasihi watoto mzingatie masomo, kanuni za afya kama mnavyoelekezwa na wataalam wa afya na endeleeni kuwa wanachama wazuri katika vikundi vya watoto vinavyosimamiwa na AGPAHI.
Pia, ningependa kuwashukuru walezi ambao wamesafiri na watoto kutoka mikoa ya Shinyanga na Simiyu. Napenda mpeleke shukrani kwa walezi wengine waliobaki kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuunda vikundi vya watoto, kuwalea watoto katika maadili mazuri ya kitanzania na kuwaelimisha juu ya huduma za afya.
Mwisho ningependa kuwatakia watoto wote kambi njema. Mzingatie mafunzo na nawatakieni kila heri kwa safari ya kwenda kutembelea mto Kagera, kiwanda cha sukari Kagera, makumbusho ya vita vya Idd Amin na mpaka wa Tanzania na Uganda siku ya Jumatano.
Baada ya kusema hayo machache, sasa napenda kutamka rasmi kuwa, kambi ya Ariel 2015 mkoani Kagera imefunguliwa.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA!

 Watoto wakipata chai ya Jioni .



 






Next Post Previous Post
Bukobawadau