Wapo walioshindwa kukemea rushwa, sasa wanataka madaraka
Ni miezi takriban kama mitatu na nusu imesalia Watanzania wenye
sifa za kupiga kura wakapige kura kwa ajili ya kuwachagua viongozi,
wakiwamo wabunge, madiwani na rais.
Uchaguzi ungekuwa soka, tungeweza kusema tupo
katika dakika za majeruhi, lakini ukweli ni kwamba hata huo uchaguzi
tunaouelekea upo katika dakika za majeruhi. Nawaasa Watanzania wenzangu
kwamba tusidanganyike na maneno ya wagombea. Tuyapime wayasemayo na
tuyachuje kwa chujio lenye tundu nyembamba kwani wengine wanatumia kila
namna mbinu ilimradi waingie Ikulu. Wako tayari hata kuhonga kufikia
ndoto yao hiyo.
Jambo la kushangaza ni kuwa tabia ya kupokea hongo
kutoka kwa wasaka uongozi imekuwa maarufu na inayokubalika na
Watanzania wengi. Hadi imefikia kuwa asiyetoa rushwa hathaminiki na
nafasi yake ya kupita katka nafasi yoyote ile ni ndogo.
Tena jambo la kushangaza miongoni mwa wagombea
ambao wanataka kuongoza nchi, walishawahi kuwa viongozi tena walikuwa na
nyadhifa za juu serikalini. Tujiulize pia wakati wanatuongoza kipindi
kile walishindwa nini kuweka mambo sawa serikalini au hayo matatizo
wanayoyaongelea leo ndiyo yanatokea wakati wao wapo nje ya uongozi?
Nawaonya Watanzania kuwa makini kwa kutokubali
kuvurugwa na watu wanaotangaza nia ya kugombea urais na ubunge katika
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, badala yake tufanye uamuzi sahihi kwa
kumchagua kiongozi atakayekuwa tayari kulinda rasilimali za nchi yetu.
Kabla ya kufanya uamuzi, tuwaulize watangazania
je, wana mikakati gani ya kulinda rasilimali zetu na kuzitumia
rasilimali tulizonazo kwa masilahi ya taifa?
Je, tutakuwa na uhakika gani kama tukiwapa dhamana
ya kutuongoza, hawatatumia rasilimali zetu kujinufaisha wao, familia
zao na rafiki zao?
Tuwasikilize kwa makini na baadaye tumchague mtu
ambaye ataweza kulinda masilahi ya Watanzania wote siyo masilahi ya
familia yake na kundi fulani lililokuwa likimshabikia wakati anaomba
kura.
Tusimpime mtu uongozi kwa sababu tu katupa fulana,
khanga, kofia, katununulia chakula na katupa nauli ya Sh20,000, kwani
vitu hivyo dhalili vitatugharimu kwa miaka mitano ijayo. Kiongozi
anayekushawishi umchague kwa kukupa zawadi ujue ana lake jambo, kamwe
usimpe kura yako.
Sasa hivi mtawaona wagombea wengi wakija na nyuso
za furaha mpaka nyumbani kwenu, wakiwasihi muwachague, huku wakitoa
ahadi kedekede ambazo awali walizitoa na hawakuzitekeleza, hao msiwape
nafasi, waogopeni kama ukoma.
Wananchi tunatakiwa kubadilika na siyo kila siku
tunadanganywa na sisi tunakubali kama vile hatuoni mbele. Leo hii
utachukua kitenge, sufuria, kofia au hata pesa ili umchague aliyekupa,
lakini je, vitu hivyo utakaa nayo kwa miaka mitano? Je, shida zako za
msingi zitakuwa zimetatuliwa? Jiulize kwanza kabla hujapokea hiyo rushwa
na uipime rushwa hiyo na thamani ya maisha yako.
Haki ni kitu ambacho kinapiganiwa na siyo
kutafutwa pekee. tuipiganie haki yetu ya kuwa na viongozi bora kwa
kuchambua kauli zeo wenyewe.
Tuwasikilize na kuzichambua kauli zao ili tuweze kuwa katika
mazingira mazuri zaidi ya kufanya uamuzi sahihi siku ya kupiga kura.
Nawasisitiza Watanzania tusipoteze haki zetu,
tukajiandikishe kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura ili siku ikifika
tutumie haki yetu ya msingi ya kuwachagua viongozi.
La muhimu siku hiyo ni kufanya uamuzi wa busara kwa kumchagua kiongozi bora.
Na Hussein Issa ,mwandishi mwandamizi wa gazeti la Mwananchi.