USAHIHI:UKAWA MAZUNGUMZO YANAENDELEA VIZURI
Uongo ukiachwa ukasemwa sana bila kusahihishwa unaweza kugeuka kuwa ukweli.
Tungependa kusahihisha propaganda nyepesi zinazoendelea kuenezwa ili kuusaidia umma usiendelee kupotoshwa kwa mambo yasiyokuwa ya msingi huku kukiwa na mambo makubwa yanayohitaji 'attention' ya Watanzania kuamua mustakabali sahihi wa nchi yao kwa kuchagua MABADILIKO kupitia uchaguzi wa kihistoria hapo Oktoba 25.
1. Zipo taarifa zinaendelea kuenezwa kuhusu makada wa CCM wakiongozwa na Edward Lowassa kuwa wana mpango wa kuhamia CHADEMA. Hadi sasa tunaziona habari hizo kupitia mitandaoni na kwenye vyenye mainstream media. Bila shaka wenye taarifa sahihi za mipango hiyo ni hao hao wanaozieneza. Nasi hatuwajibiki kabisa kuwasaidia kutoa uhakika wa uenezi huo wanaofanya kwa maslahi wanayoyajua.
2. Viongozi wakuu wa chama wakiongozwa na Mwenyekiti wa Taifa Freeman Mbowe na Katibu Mkuu Dk. Willibroad Slaa wamekuwa wakiendelea na majukumu yao mbalimbali kwa kadri ya nafasi zao na ratiba za chama hususan wakati kama huu kuelekea defining moments za uchaguzi mkuu ambapo mara kadhaa wamekuwa katika vikao na viongozi wakuu wenzao katika UKAWA ili kutafuta mwelekeo sahihi kwenda Oktoba 25.
Wanaoeneza habari kwamba Mkiti Mbowe na KM Dk. Slaa wamekuwa na mtafaruku eti kwa sababu ya 'ujio dhanifu' wa Lowassa basi watu hao watakuwa hawajui utaratibu wa utendaji kazi wa Chama kwa ujumla na hususan Viongozi hao wawili ambao siku zote hufanya kazi kwa maelewano ya hali ya juu sana kiasi cha kuendelea kuwa sehemu ya uimara wa CHADEMA.
3. Propaganda hizo zinazojengwa katika misingi ya siasa nyepesi zimekwenda mbali hadi kumsemea uongo mmoja wa waasisi wa CHADEMA Mzee Mtei eti amekodiwa ndege kuja kutuliza mtafaruku.
3. Tunajua lengo la upotoshwaji huo ni kutaka kuwachaganya Watanzania wanaojiandaa kuiondoa CCM madarakani mwaka huu. Waenezaji uongo wanataka kuwaaminisha Watanzania wanaowaka moto wa mabadiliko kuwa CHADEMA nayo imegawanyika kama ilivyo kwa CCM ambayo imesambaratika juzi Dodoma kiasi cha wajumbe kumzomea Mwenyekiti wao wa chama.
4. CHADEMA iko imara kuliko wakati mwingine wowote ule, hasa katika kipindi hiki ambapo inaendelea kujiandaa kuwatumikia Watanzania na kupanga mikakati mbalimbali, kwa kushirikiana na washirika wenza kwenye UKAWA, kuikabili CCM iliyomeguka vipande vipande na kuiondoa madarakani.
NB; Kuhusu #UKAWA Julai 14
Kama ambavyo Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA Prof. Ibrahim Haruna Lipumba alisema Jumamosi usiku alipozungumza na waandishi wa habari kuwa leo umoja huo utafikia na kutangaza kwa umma makubaliano juu ya mambo makubwa mawili;
1. Mgombea mmoja wa urais
2. Majimbo yaliyokuwa yamesalia katika mgawanyo kwa maana ya kusimamisha Mgombea mmoja
Aidha, Prof. Lipumba alisema kuwa UKAWA wameshafanikiwa kufikia mwafaka katika majimbo kwa asilimia 97 na sehemu iliyobakia ni ile ambayo itahitaji mashauriano au (bilateral) mwafaka kati ya vyama viwili katika majimbo fulani fulani ambapo vyama hivyo vilikuwa bado vinapitia vigezo vilivyokubalika.
Tangu asubuhi ya leo vikao vimekuwa vikiendelea. Majadiliano yamekwenda vizuri kabisa. Baadae Summit (kikao cha Viongozi wakuu) itakutana kwa ajili ya wayfoward na kuzungumza makubaliano kwa Vyombo vya Habari kwa ajili ya Watanzania.
Vyombo vya Habari vitataarifiwa muda na mahali ambapo Summit ya UKAWA itakutana nao kwa ajili ya taarifa hiyo inayosubiriwa na umma wa Watanzania.
Stay tuned
Makene
July 14,2015