KILOMETA 6,276 ZA BARABARA ZAJENGWA NCHINI KWA MIAKA 10
Wakati wakandarasi walipokuwa wanajenga daraja hili katika eneo la Miangalua kwenye barabara ya Tunduma-Sumbawanga mwaka 2011. Barabara hiyo sasa imekamilika.
Barabara ya Mwanza-Musoma iko katika hali nzuri.
Ujenzi wa barabara ukiendelea katika baadhi ya miradi nchini.
Ujenzi wa barabara ya Iringa-Dodoma umekamilika kwa asilimia 95, bado maeneo machache tu likiwemo hili la Mlima Nyang'oro ambapo Wachina wameuchonga ili kupunguza kona katika umbali wa kilometa 15. (Picha zote na Daniel Mbega wa www.brotherdanny.com).
Na Daniel Mbega, brotherdannyblog
Sumbawanga: NAJIWEKA vyema kwenye
kiti na kutazama nje kupitia dirishani. Japokuwa giza limetanda majira haya ya
saa 4:30 usiku, lakini ninaweza kuhisi jinsi basi hili nililopanda la kampuni
ya Majinjah linavyotafuna lami.
Abiria mwenzangu wa jirani ananiambai tutaingia
saa sita kasoro usiku mjini Sumbawanga mjini. Nafarijika japo uchovu ni mwingi, maana kuketi kwenye basi kwa saa takriban 15 siyo mchezo ingawa tulipata nafasi mara kadhaa za kupumzika 'kuchimba dawa' na kupata mlo.
“Barabara yote ni lami tupu ndugu yangu,
kasoro tu ni haya matuta kutoka Tunduma hadi Sumbawanga, lakini yamesaidia
kupunguza mwendokasi,” ananieleza.
Tunduma tumeondoka kama saa tatu hivi
kuzikabili kilometa 222 hadi Sumbawanga, lakini safari hii ya kutoka Dar es
Salaam inayokadiriwa kuwa na umbali wa kilometa 1,000 imekuwa siyo ndefu licha
ya uchovu wa kiuno na mgongo kutokana na kuketi tangu saa 12 alfajiri. Faraja pekee
ni kwamba ninatumia siku moja tu kufika Sumbawanga, tofauti na miaka mitano
iliyopita ambapo nililazimika kutumia siku mbili huku nikiingia gharama za
ziada za kulala Lodge pale Mbeya kutokana na kutokuwepo na usafiri wa uhakika kutokana
na ubovu wa barabara.
Wakati huo, ukilala Mbeya unalazimika tena
kuamka mapema kuwahi basi ambalo licha ya kuondoka saa 12 alfajiri, bado
litafika Sumbawanga saa 8 mchana.
Jirani yangu ananiambia kwamba sasa unaweza
kwenda na kurudi Sumbawanga mara mbili ukitokea Mbeya kwani mabasi ni mengi na
njia ‘inateleza’.
“Wametukomboa sana, magari hayajazi kama
zamani, unasafiri kwa raha na kwa wakati – muda wowote unaotaka,” ananieleza.
Ndiyo. Nakumbuka safari moja wakati
nikitokea Sumbawanga jinsi basi lilivyokuwa limejaza abiria mpaka sehemu ya
kupita ikakosekana. Walioketi walikuwa wachache kuliko waliosimama, sasa piga
hesabu lilikuwa na abiria wangapi! Hata kondatka mwenyewe alilazimika kupita
kwa kuinama juu ya siti ili kwenda nyuma kuwapanga abiria waliosimama na
kuchukua nauli. Ilikuwa ni hatari.
Lakini leo barabara hii imetandikwa lami na
imekuwa sehemu ya barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 6,276 ambazo
zimetengenezwa na utawala huu wa Awamu ya Nne, huku sehemu kubwa yabarabara
hizo ikiwa imesimamiwa na Dk. John Pombe Joseph Magufuli kama Waziri wa
Miundombinu.
Nimezunguka karibu nchi nzima nikifanya habari za uchunguzi kwa miaka kumi iliyopita. Mazingira ya wakati ule na ya sasa ni tofauti kabisa, maeneo ambayo yalikuwa hayafikiki, hivi sasa hali ni nzuri.
Tangu Januari hadi Juni 2015 pekee nimezunguka karibu kilometa 20,000 hapa nchini. Nimezunguka nikitokea Iringa kwenda Arusha kupitia Dodoma-Singida hadi Manyara; nimezunguka kutoka Dar es Salaam-Kiteto-Kondoa hadi Babati; nimepita Babati-Kondoa-Mayamaya hadi Dodoma; nimepita Mwanza-Shinyanga-Tabora-Mpanda hadi Sumbawanga mpaka Mbeya; nimetoka Dar es Salaam-Njombe-Songea hadi Mbambabay; nimetoka Mwanza-Musoma hadi Sirari; nimezunguka Mwanza-Sengerema-Geita hadi Bukoba; nimetoka Bukoba kupita Kahama hadi Dar es Salaam; nimetoka Shinyanga-Maswa-Bariadi hadi Lamadi; na maeneo mengine mengi kwa miezi sita.
Hakika nilichokiona kinastahili kupongezwa kwamba kimefanyika. Ingawa barabara kadhaa zimesimama kutokana
na kukosekana kwa fedha kufuatia msukosuko wa wafadhili kushindwa kutoa fungu,
lakini nyingi kati ya hizo zimekamilika na kuiunganisha vyema Tanzania.
Nilipita wakati fulani ilipoanza
kutengenezwa barabara hii, nadhani ilikuwa mwaka 2011 nikiwa katika harakati
zangu za kuandika habari za maendeleo vijijini. Barabara hii ilimegwa katika
vipande vitatu ili kuharakisha ujenzi wake na kuzingatia ubora.
Kipande cha kwanza kilikuwa kutoka Tunduma hadi
Ikana chenye urefu wa kilometa 63.2 ambacho kilijengwa na kampuni ya Consolidated
Contractors Group kwa gharama ya Dola 82.521
milioni; Kipande cha pili chenye urefu wa kilometa 64.2 kilikuwa kutoka Ikana
hadi Laela na kilijengwa na kampuni ya China Newera (64.2km Ikana-Laela) kwa
Dola 46.812 milioni; na kipande cha mwisho kilikuwa kutoka Laela hadi
Sumbawanga chenye urefu wa kilometa 95.31 ambacho kilijengwa na kampuni ya Aarsleff-Interbeton J.V kwa gharama ya Dola 130.038 milioni. Kwa hiyo
kilometa zote 222.71 ziligharimu jumla ya Dola 259.371 milioni ambazo ni fedha
za wahisani na fedha za ndani.
Ni
fedha nyingi sana lakini haziwezikuzidi thamani halisiya barabara hii ambayo
licha ya kuwakomboa wananchi wa pembezoni hasa katika mikoa ya Mbeya, Rukwa na
Katavi, lakini pia itasaidia kuiunganisha Tanzania na nchi jirani ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo kwa sababu ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 112
kutoka Sumbawanga-Matai hadi bandari ya Kasanga katika Ziwa Tanganyika
unaendelea chini ya kampuni ya China Railway 15th Bureau
Group Corporation - CR15G kwa gharama ya Dola 80.912 milioni.
Dk. Magufuli, ambaye sasa
ni mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), anazifahamu karibu barabara
zote nchini na hatua zilikofikia. Alipoingia kwa mara ya kwanza bungeni mwaka
1995 baada ya kushinda katika jimbo la Chato akiwa na miaka 36 tu, Rais Benjamin Mkapa akamteua kuwa Naibu Waziri
katika Wizara ya Miundombinu. Kazi ya Ubunge na unaibu waziri ilimpeleka salama
hadi mwaka 2000.
Uchaguzi wa mwaka 2000
ulipoitishwa, Dk. Magufuli aligombea na kushinda kwa mara ya pili. Rais Mkapa
akamteua kuwa Waziri wa Wizara ya Miundombinu, wadhifa aliodumua nao hadi
kipindi cha uongozi wa Mkapa kilipomalizika.
Mwaka 2005 alishinda ubunge
kwa mara ya tatu, lakini safari hii aliingia katika orodha ya wabunge waliopita
bila kupingwa. Rais Jakaya Kikwete akamteua kuongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi hadi mwaka 2008 alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,
ambayo aliiongoza hadi mwaka 2010.
Mwaka 2010 akagombea tena
ubunge, lakini safarihii akapambana na mgombea wa Chadema, Rukumbuza Vedastus
Albogast ambaye alitoa upinzani mkubwa ingawa hatimaye Magufuli alishinda kwa
asilimia 66.39 dhidi ya asilimia 26.55 za mpinzani wake. Rais Kikwete
akamrudisha katika Wizara ya Ujenzi ambako yuko hadi hivi sasa.
Tangu kuelekea uchaguzi
mkuu wa mwaka 2005, wengi walikuwa wakimtaja Magufuli kwamba anafaa kuwania
urais, lakini yeye alikaririwa akisema wakati huo kwamba hana mpango huo.
Hata makada wenzake
walipoanza kuonyesha nia kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka huu, yeye hakuwa na
papara na iliwashangaza wengi Mei 29 alipoamua kujitosa kimya kimya, akachukua
fomu na kuondoka, bila mbwembwe wala madoido kama walivyofanya wengine.
Wanaomfahamu wanasema nguvu
yake kubwa iko kwenye elimu yake, lakini kukaa muda mrefu kwenye wizara zake na
mambo makubwa aliyoyafanya katika wizara alizopata kuziongoza, pamoja na uwezo
wake wa kutoa maamuzi magumu kila mara vinampa sifa ya kuwa rais anayefaa
katika kipindi hiki ambacho rushwa, ufisadi na ukosefu wa maadili vimetamalaki.
Udhaifu wake pekee unaotajwa
na walio karibu yake ni kufanya maamuzi ya haraka, jambo ambalo linaweza
kurekebishwa kwa kuwa ndani ya Taasisi ya Urais kuna washauri makini.
UJENZI WA BARABARA
Katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya
awamu ya nne, barabara zenye urefu wa jumla ya 6,276.82km zimejengwa kwa
gharama ya Dola 102,654.98 milioni, nyingi kati ya hizo zikiwa za lami na hivyo
kuutengeneza mtandao imara wa miundombinu ya barabara.
Kujengwa kwa barabara hizo kumerahisisha
hata usafiri ambapo leo hii magari ya abiria na mizigo kutoka Dar es Salaam
kwenda Musoma, Mwanza, Kagera na Kigoma hayahitaji kuzunguka Nairobi bali
yanakwenda moja kwa moja.
Hivi sasa usafiri wa kutoka Dar es Salaam
kwenda Sumbawanga ni wa siku moja badala ya siku mbili, kama ilivyo kwa usafiri
wa Dar es Salaam kwenda Mbinga, jambo ambalo miaka 10 iliyopita lilikuwa ndoto.
Asilimia 90 ya miradi hiyo imesimamiwa na
Dk. Magufuli akiwa Waziri wa Miundombinu katika kipindi cha mwaka 2010 hadi
2015na bado miradi mingine inaendelea kujengwa japo imesimama kidogo kutokana
na ufinyu wa bajeti.
Kampuni za Kichina zimepata mikataba mingi
ya ujenzi. Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS),
katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, kampuni 14 kutoka China zimeingia jumla
ya mikataba 58 ya ujenzi wa kilometa 3,140.85 yenye thamani ya Dola 1.75 bilioni.
Kampuni ya China Henan International
Cooperation Group Co., Ltd. (CHICO) ambayo ilipata mkataba wenye thamani ya
Dola 206 milioni kutoka Wakala wa Barabara Zambia kujenga barabara ya
Mansa-Luwingu yenye urefu wa kilometa 175, peke yake imeingia mikataba 13
nchini Tanzania ya barabara zenye urefu wa kilometa 705.2 zikiwa na thamani ya
Dola 490.26 milioni.
Hizi ni pamoja na barabara za
Singida-Iguguno (76km)
yenye thamani ya Dola 20.55 milioni;
Sekenke-Shelui (33km)
yenye thamani ya Dola 12.51 milioni;
Mwandiga-Manyovu (60km)
wenye thamani ya Dola 32.54 milioni;
Kigoma-Kidahwe (35.7km)
kwa Dola 19.56 milioni; Bonga-Babati (19.20km) kwa Dola 11.95
milioni; Tabora-Urambo (42km) kwa Dola 31.17
milioni; Kyaka-Bugene (59.1km) kwa Dola 51.6
milioni; Dareda-Minjingu (84.6km) kwa Dola 51.6
milioni); Kidahwe-Uvinza-Ilunde (76.6km) kwa Dola 47.5
milioni; Isaka-Ushirombo (132km) kwa Dola 88.223
milioni; Kilwa Road Phase III (1.5km) kwa Dola 3.4
milioni; Nyanguse-Musoma (85.5km) kwa Dola 3.3
milioni; na Kagoma-Lusahunga (154km ) kwa ubia na kampuni ya CRSG kwa gharama ya Dola 116.2 milioni.
China Sichuan International Cooperation
Co., Ltd (SIETCO) inajenga barabara zenye urefu wa 283.9km zenye thamani ya
Dola 123.03 milioni ambazo ni Isuna-Singida (63km) kwa Dola 18.5 milioni; Tarakea-Rongai-Kamwanga (32km) kwa Dola 8.8 milioni; Iringa-Migori (95.1km) kwa Dola 51.123 milioni; na Migori-Fufu Escarpment (93.8km) kwa Dola 44.7 milioni, wakati kampuni ya CICO inajenga barabara ya
Nangurukuru-Mbwemkuru yenye 95km kwa thamani ya Dola 23.82 milioni.
Kampuni ya China Geo-Engineering
Corporation International Ltd (CGC INT'L) inajenga barabara zenye urefu wa
525.9km zikiwa na thamani ya Dola 151.2 milioni. Barabara hizo ni Shelui-Nzega
(112km) kwa
Dola 12.6 milioni; Kyamorwa-Buzirayombo (120km) kwa Dola 29.822
milioni; Manyoni-Isuna (54km) kwa Dola 18.4
milioni; Arusha-Namanga (104.2km) kwa Dola 49.64
milioni; Chalinze-Tanga Phase I (125km ) kwa Dola 25.9
milioni na ndiyo kampuni iliyojenga Daraja la Mkapa
(Daraja la Umoja 10.7km) linalounganisha Tanzania na Msumbiji kwa gharama ya
Dola 14.9 milioni.
Katika orodha hiyo, ipo kampuni
inayomilikiwa na serikali ya China, Hydropower Engineering and Construction
Company (SINOHYDRO) ambayo ilipata mikataba 12 nchini Tanzania ya ujenzi wa
barabara zenye urefu wa jumla ya 779.95km zenye thamani ya Dola 434.36 milioni.
Barabara hizo ni Sengerema-Usagara (40km) kwa gharama ya Dola 21.724 milioni; Buzirayombo-Geita (100km) kwa Dola 25 milioni; Geita-Sengerema (50km) kwa Dola 24.034 milioni; Dodoma-Mayamaya (43.65km) kwa Dola 25 milioni; Manyoni-Itigi-Chaya (89.3km) kwa Dola 66.56 milioni; Puge-Tabora (56.1km) kwa Dola 35.085 milioni; Handeni-Mkata (54km) kwa Dola 34.81 milioni; Korogwe-Handeni (65km) kwa Dola 38.4 milioni; Katesh-Dareda (73.8km) kwa Dola 38.94 milioni; Singida-Katesh (65.1km) kwa Dola 31.34 milioni; Tanga-Horohoro (65km) kwa Dola 42.43 milioni; na Peramiho Junction-Mbinga (78km) kwa Dola 48.444 milioni.
CHIKO ilijenga barabara ya Sam Nujoma
jijini Dar es Salaam yenye urefu wa 4km kwa thamani ya Dola 7.9 milioni, China
Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) ilipata mikataba minne ya
kujenga barabara zenye urefu wa 145.6km kwa thamani ya Dola 95 milioni.
Barabara hizo ni Magole-Turiani (48.6km) kwa Dola 25.43 milioni; Tabora-Urambo (52km) kwa Dola 36.3 milioni; Dumila-Rudewa (45km) kwa Dola 25.5 milioni na Jangwani Depot kwa ajili ya mradi wa mabasi yaendayo kasi Dar
es Salaam (BRT) kwa Dola 7.81 milioni.
(Imeandaliwa na www.brotherdanny.com. Simu: 0656-331974)