UKAWA WATANGAZA MAJIMBO WALIYOGAWANA KATIKA UCHAGUZI MKUU
Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Nderakindo Kessy (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho, Ilala Dar es Salaam jana, wakati akitangaza majimbo yaliyochini ya vyama vinavyounda Ukawa ambayo vyama hivyo vitasimamisha wagombea wao katika uchaguzi mkuu. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha NLD, Masudi Makunjunga.
Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Shaweji Mketo (wa pili kulia), akizungumza katika mkutano huo na waandishi wa habari. Kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha NLD, Masudi Makunjunga, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Nderakindo Kessy na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, akizungumza katika mkutano huo.
Viongozi wa vyama hivyo wakiwa meza kuu.
Mkutano na wanahabari ukiendelea.
Na Mwandishi Wetu
Na Mwandishi Wetu
UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umetangaza
mgawanyo wa majimbo yake 253 huku majimbo mengi yakienda Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema).
Taarifa ya mgawanyo wa majimbo ilitolewa na Kaimu
Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Dk. Nderakindo Kessy jana katika ofisi
kuu za chama hicho Ilala jijini Dar es Salaam.
Kessy alisema baada ya majadiliano ya muda mrefu
kuhusu kuachiana majimbo ya ubunge, vyama vinavyounda Ukawa vimefanikiwa
kuachiana majimbo ili kuhakikisha wanakiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
madarakani.
Alisema mgawanyo wa majimbo hautahusiana na
mgawanyo wa kata za kugombea udiwani na mwongozo wa kuachiana kata ndiyo
utatumika katika kuamua namna ya kugombea kata.
“Tunapenda kuchukua nafasi hii kuwatangazia
Watanzania majimbo ambayo hadi leo (jana), tumekubaliana kuachiana kuwa ni
majimbo 253 na majimbo 12 tutawaambia Jumatano au Alhamis kwani kuna mambo
hayajakaa vizuri,” alisema.
Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Mkoa wa Mara majimbo
yote wameachiwa Chadema ambayo ni Rorya, Tarime Mjini, Tarime Vijijini, Musoma
Vijijini, Butiama, Bunda Mjini, Mwibara, Musoma Mjini na Bunda Vijijini.
Kessy alisema Mkoa wa Simiyu ambao una majimbo
saba, majimbo sita wamepewa Chadema ambayo ni Bariadi, Maswa Magharibi, Maswa
Mashariki, Kisesa, Meatu, Itilima na Jimbo la Busega atasimama mgombea wa Chama
cha Wananchi (CUF).
“Mkoa wa
Shinyanga majimbo yote sita wameachiwa Chadema na sababu ya msingi ni wao kuwa
na mizizi ambapo ni majimbo ya Msalala, Kahama Mjini, Kahama Vijijini,
Shinyanga Mjini, Kishapu na Ushetu na Mkoa wa Mwanza ni Ukerewe, Magu,
Nyamagana, Buchosa, Sengerema, Ilemela, Misungwi yameenda Chadema na Kwimba na
Sumve CUF,” alisema.
Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema Mkoa wa Geita
majimbo yote yaliachiwa Chadema, ambayo ni Bukombe, Busanda, Nyang’wale, Chato
na Mbogwe, Mkoa wa Kagera katika majimbo tisa Chadema imeachiwa majimbo sita
ambayo ni Karagwe, Kyerwa, Bukoba Mjini, Muleba Kaskazini, Muleba Kusini na
Biharamulo na Nkenge, Ngara yakiachwa kwa NCCR-Mageuzi na Jimbo la Bukoba
Vijiji likiachwa kwa CUF.
Mkoa wa Mbeya Jimbo la Lupa, Songwe, Mbeya Mjini,
Kyela, Rungwe, Busekolo, Mbozi Mashariki, Momba, Mbeya Vijijini, Vwawa na
Tunduma yote yameachiwa Chadema na Jimbo la Ileje NCCR-Mageuzi.
“Iringa, Jimbo la Ismani, Kalenga, Mufindi Kaskazini,
Iringa Mjini, Kilolo, Mufindi Mjini Chadema itasimamisha wagombea na Mufundi
Kusini NCCR-Mageuzi, ambapo Mkoa wa Njombe majimbo yote yameachwa Chadema
ambayo ni Njombe Kaskazini, Lupembe, Wanging’ombe, Makete, Ludewa na Makambako,”
alisema Kessy.
Kessy alisema Mkoa wa Rukwa wamekubaliana
kuwaachia Chadema, ambapo ni majimbo ya Nkasi Kusini, Kwela, Nkasi Kaskazini,
Sumbawanga Mjini na Kalambo, huku Mkoa wa Tanga CUF wameachiwa majimbo nane
ambayo ni Handeni Mjini, Handeni Vijijini, Pangani, Tanga Mjini, Bumbuli,
Mlalo, Lushoto na Mkinga. Chadema wameachiwa majimbo manne ambayo ni Kilindi,
Muheza, Korogwe Mjini na Korogwe Vijijini.
Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema Mkoa wa Kilimanjaro
majimbo saba imeachiwa Chadema ambayo ni Rombo, Same Magharibi, Same Mashariki,
Moshi Vijijini, Moshi Mjini, Hai na Siha ambapo Vunjo NCCR-Mageuzi wameachiwa
na Jimbo la Mwanga likibakia hadi Alhamis.
Mkoa wa Arusha alisema Chadema wameachiwa majimbo
yote ambayo ni Arumeru Mashariki, Arumeru Magharibi, Arusha Mjini, Longido,
Monduli, Karatu na Ngorongoro halikadhalika Mkoa Manyara Jimbo la Simanjiro,
Mbulu Vijijini, Hanang, Babati Mjini, Babati Vijijini, Kiteto na Mbulu Mjini.
Aidha, Kessy alisema Mkoa wa Dar es Salaam, Jimbo la
Ubungo, Kawe, Ukonga, Ilala na Kibamba Chadema itasimamisha wagombea na
Kinondoni, Jimbo la Temeke na Mbagala CUF itasimamisha wagombea huku majimbo ya
Segerea na Kigamboni yakibakia kiporo hadi Alhamisi wiki hii.
Alisema Mkoa wa Pwani majimbo ya Bagamoyo,
Kisarawe, Mkuranga, Mafia, Rufiji Utete na Rufiji Kibiti majimbo hayo
yameachiwa CUF na Majimbo ya Chalinze, Kibaha Mjini, Kibaha Vijijini yakiachiwa
Chadema.
Mkoa wa Morogoro Jimbo la Kilosa na Morogoro
Kusini Mashariki CUF watasimamisha wagombea huku majimbo ya Mikumi, Morogoro
Kusini, Kilombero, Mlimba, Mvomero, Ulanga Magharibi, Ulanga Mashariki na
Morogoro Mjini yatakuwa chini ya Chadema.
“Mkoa wa Dodoma Jimbo la Kondoa Mjini, Kondoa
Vijijini, Chemba yameachwa kwa CUF, Jimbo la Kibakwe na Mtera wameachiwa
NCCR-Mageuzi na Dodoma Mjini, Kongwa, Bahi na Chilonwa Chadema itasimamisha
wagombea.
Kessy alisema Mkoa wa Singida majimbo yote saba
yameenda Chadema ambayo ni Iramba Magharibi, Iramba Mashariki, Singida
Kaskazini, Singida Mashariki, Singida Magharibi, Manyoni Magharibi na Manyoni
Mashariki.
Kwa Mkoa wa Tabora Jimbo la Bukene, Nzega Vijijini, Igalula, Kaliua
Tabora Kaskazini na Tabora Mjini watagombea CUF na Nzega Mjini, Igunga, Urambo,
Ulyankulu, Manonga na Sikonge Chadema watasimamisha wagombea.
Alisema Mkoa wa Katavi majimbo yote sita ya Mpanda
Mjini, Mpanda Vijijini, Katavi, Nsimbo na Kavuu. Mkoa wa Kigoma Jimbo la Buyungu,
Mhambwe, Kasulu Mjini, Kasulu Vijijini, Kigoma Kusini na Manyovu NCCR-Mageuzi
itasimamisha wagombea na Kigoma Kaskazini na Kigoma Mjini Chadema
itasisimamisha wagombea wa ubunge.
Mkoa wa Ruvuma Jimbo la Tunduru Kaskazini,
Namtumbo na Tunduru Kusini Chama cha CUF watasimamisha wagombea na majimbo ya
Peramiho, Mbinga Magharibi/Nyasa, Mbinga Mashariki/Mbinga, Songea Mjini na
Madaba, na Mbinga Mjini NCCR-Mageuzi itasimamisha mgombea.
“Mtwara Jimbo la Newala Mjini, Newala Vijijini,
Tandahimba, Mtwara Vijijini, Nanyamba na Nanyumbu CUF itasimamisha wagombea
huku majimbo ya Lulindi, Masasi na Ndanda wakiachiwa Chama cha National League
Democratic (NLD),” alisema Kessy.
Kessy alisema Mkoa wa Lindi Ukawa kwa ujumla wao
wamekubaliana kuwaachiwa CUF katika majimbo yote ambayo ni Mtama, Kilwa
Kaskazini, Kilwa Kusini, Lindi Mjini, Ruangwa, Nachingwea, Liwale na Mchinga.
Mketo
Akizungumzia uamuzi huo, Kaimu Naibu Katibu Mkuu
CUF, Shaweji Mketo alisema mgawanyo huo umezingatia mambo makuu matano ambao ni
kuhusu mbunge aliyeko tangu waka 2010, nafasi ya chama katika uchaguzi huo wa
2010, nafasi ya udiwani, uchaguzi wa Serikali za Mitaa na nguvu na mtandao wa
chama hadi sasa.
Mketo alisema lengo la Ukawa si kugawana majimbo
kama inavyotafsiriwa ila ni kugawana kwa vigezo ili kuhakikisha wanapata
ushindi wa jumla na kushinda uchaguzi ujao.
Makujunga
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa NLD, Masudi
Makujunga alisema chama chao kipo pamoja kuhakikisha kuwa mabadiliko ya
kisiasa, kijamii yanatokea ndani ya nchi wakati huu.
“Lengo si ufahari katika kugawana majimbo, lengo
letu ni kuhakikisha kuwa mabadiliko yanapatikana na sisi NLD tupo tayari
kushiriki katika mabadiliko hayo kwenye sehemu husika,” alisema.
Mnyika
Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema
jitihada za Ukawa zipo katika hali nzuri hivyo wao watahakikisha kuwa wanakuwa
wamoja hadi kufikia hatima yao ambayo ni kushinda uchaguzi na kuongoza nchi.
Alisema kilichofanyika ndio makubaliono ya
viongozi wao hivyo wana Ukawa wote wanapaswa kukubaliana na hali hiyo ili Taifa
liweze kusonga mbele kwa maslahi ya wananchi na wapenda mabadiliko.
Aidha, Mnyika aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), kutoa ufafanuzi kuhusu kuwepo kwa maelekezo ya kuvitaka na wagombea wao kurejesha
fomu Agosti 19, mwaka huu huku ikiamini kuwa sheria inataka mchakato huo
kukamilika Agosti 21.
Mnyika aliitaka NEC kutoa ufafanuzi kuhusu kuwepo
kwa wanajeshi watatu ambao wanahusika na mfumo wa teknolojia ya habari katika
tume hiyo jambo ambalo ni kinyume cha taratibu za tume hiyo.
Mnyika alisema iwapo tume itakuwa kimya itakuwa
imethibitisha taarifa hizo ambazo kimsingi zinachochea vurugu na hofu kwa
washiriki wa uchaguzi huo.
Ukawa uliasisiwa wakati wa Bunge Maalumu la Katiba
mwaka 2014, lengo likiwa kuunganisha nguvu kwa ajili ya kusimamia na kutetea
maoni ya wananchi yaliyowasilishwa kupitia rasimu ya pili ya Katiba
iliyotayarishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Umoja huo ulihusisha wabunge kutoka vyama
mbalimbali vya upinzani na baadhi ya wabunge kutoka kundi lililojulikana kama
la 201ambapo baadaye, ulibaki na wabunge na viongozi kutoka vyama vya NLD, NCCR
– Mageuzi, CUF na Chadema.
Lowassa
Wakati huo huo, Mgombea urais wa Chadema, Edward
Lowasa amelakiwa na maelfu ya watu mjini hapa na kusema yeye ni muumini wa
muungano wa serikali tatu na si mbili, ikiwa ni kuhitimisha mchakato wake wa
kutafuta wadhamini Zanzibar.
Akihutubia maelfu ya wanachama wa vyama
vinavyounda umoja huo na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja
vya Demokrasia Kibanda Maiti mjini Unguja, alisema wanaosema yeye si muumini wa
serikali tatu ni wazushi na wapuuzwe.
Lowassa alisema alikuwa muumini wa mfumo huo tangu
alipokuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu katika miaka ya 90. Alisema wanaosema
yeye ni muumini wa serikali mbili na hawezi kubadilika hawamjui.
Alisema yeye na wenzake waliwahi kupendekeza jambo
hilo katika vikao vya chama na serikali kwa lengo la kuimarisha muungano,
lakini ilishindikana kutokana na viongozi wengi wa CCM kuwa na woga wa
mabadiliko.
“Hali hii ya uwoga wa viongozi wengi wa CCM
haikuja bure bali ni kutokana na mfumo wa chama hicho ila wanasahau mwalimu
aliwahimiza kuwa Watanzania wanahitaji mabadiliko, na kwa mujibu wa Baba wa
Taifa kama watayakosa ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM,” alisema.
Lowassa aliongeza, “fursa ya mabadiliko imekuja
kupitia Ukawa na ninawaomba Watanzania tuitumie vyema na kuionesha CCM kuwa
nchi hii inaweza kuwa na mabadiliko bila ya ubabe wala vitisho.”
Kabla ya mkutano huo alipokelewa na wafuasi wa
vyama hivyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume mjini
Zanzibar kisha msafara wake ulioongozwa na mgombea wa urais wa Zanzibar kwa
tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Alisema muungano kati ya iliyokuwa Tanganyika na
Zanzibar ni watu wa pande hizo mbili, hivyo kuna umuhimu wa kuwepo kwa
maridhiano yatakayoondoa manung'uniko miongoni mwa wananchi wa pande hizo jambo
ambalo atalisimamia kwa nguvu zake.
“Umaskini wa nchi hii una sababishwa na watu
kutojiamini kwa baadhi ya watendaji wa serikali na kutosimamiwa kikamilifu kwa
sheria za nchi, miongozo na maamuzi yanayofikiwa ktika vikao vya kitaifa jambo
ambalo tukiwa timu moja mimi, babu Duni (mgombea mwenza) na Maalim Seif
(mgombea urais wa Zanzibar) tutawapeleka mchaka mchaka ili kuleta maendeleo kwa
kasi kubwa na ya ajabu,” alisema.
Aidha, mgombea huyo alikosoa hatua ya Umoja wa
Vijana wa CCM (UVCCM) ya kumvua ukamanda wa vijana taifa, muasisi wa Tanu na
CCM, Kingunge Ngombare Mwiru na kuitaja hatua hiyo kuwa ni kukiuka haki ya
kikatiba ya kutoa maoni na kwamba laana za kiongozi huyo zitakishukia chama
hicho.
“Watu makini hamuwezi kukubali kumpoteza mtu kama
Kingunge eti kwa sababu alitoa maoni yake hadharani kuhusu jambo la kweli.
Wamesahau kuwa mzee huyu ndiye aliyekinusuru chama kisisambaratike wakati
Ujamaa ulipokuwa umesambaratika ulimwenguni na yeye kuwa ndiyo msemaji mkuu wa
chama. Jambo hili linaashiria mwisho wa zama za CCM na laana za kitendo hicho
ni lazima ziwashukie na hawatakuwa na wa kumlaumu,” alisema Lowassa.
Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu ajiunge na
Chadema katika ardhi ya Zanzibar, mgombe mwenza wa Lowassa, Juma Duni Haji
aliwaomba wananchi wa Zanzibar kuwaunga mkono na kuwapa ridhaa itakayowawezesha
kuwaunganisha wananchi wa Tanzania kuelekea katika umoja na maridhiano.
Maalim
Seif
Akihutubia hadhara hiyo, Maalim Seif alivitahadharisha vyombo vya dola
kusimamia ulinzi wa raia na mali zao kwa haki bila ya upendeleo kutokana na
kuwepo kwa taarifa za vitendo vinavyoashiria uvunjwaji wa sheria alivyodai
vinafanywa na CCM.
“Wenzetu
hawa wamekuwa mabingwa wa kuhubiri amani wanapokuwa majukwaani lakini
wanaposhuka huwa ndiyo wavunjaji wakubwa wa amani kwani kuna taarifa kuwa
wagombea wetu wa ubunge na udiwani katika Jimbo la Shauri Moyo na Wadi ya
Kidatu wamevamiwa na kunyang'anywa fomu zao za kusaka wadhamini. Hali hii
haiashirii kuwa kuna nia njema,” alisema.
Mapema aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa
Shinyanga ambaye alijiunga na Chadema, Khamis Mgeja aliwataka wananchi wa
Zanzibar kuendelea kuiunga mkono Ukawa kwa kuwa ndiyo yenye uwezo wa kukidhi
matakwa ya Wazanzibar na Watanzania.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe aliwashukuru wananchi wa Zanzibar na CUF kwa kumridhia
aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho na Waziri wa Miundombinu, Duni Haji
kujiunga na Chadema hatua iliyomuwezesha kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa
Lowassa.
“Kumekuwa na vitisho dhidi ya watumishi wa vyombo
vya dola kuwa mtaachwa pindi mkiwaunga mkono wagombea wa Ukawa, ninawatoa hofu
kuwa mtaendelea kuwepo hata baada ya CCM kuondoka kwa sababu nyinyi mpo kwa
mujibu wa sheria,” alisisitiza Mbowe na kuahidi kustawisha maslahi yao pindi
Ukawa ikishinda.
Mbatia
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa ambaye pia ni
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kupitia umoja wao wamewaagiza
wanasheria wa vyama vinavyounda Ukawa kunakili matukio yote ya ukiukwaji wa
haki binadamu vitakavyofanywa na watendaji au viongozi wa CCM ili waweze
kuwafungulia kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita-The Hague.
“Hatutavumilia aina yoyote ya uharamia ambayo
itafanywa na mtu au taasisi ili kuvuruga harakati za Ukawa kuleta mabadiliko
kupitia uchaguzi mkuu ujao, tumewaagiza wanasheria wetu kunakili kila tukio
linaloashiria hali hiyo na tutamfikisha kila aliyehusika au atakayehusika
kuhujumu matakwa ya demokrasia yasitekelezwe,” alisema.(Imeandaliwa na mtandao wa habari za jamii.com-simu namba 0712727062)