VIONGOZI WA SERIKALI ZA MITAA WAONYWA KUTOCHAKACHUA ZOEZI LA UGWAJI WA VYANDARUA VYA BURE MKOANI KAGERA
Viongozi wa Serikali za Mitaa
waonywa kutochakachua zoezi la ugawaji wa vyandarua vyenye viatilifu vinavyoua
mbu waenezao malaria vinavyogawiwa na serikali kwa wananchi bure katika nchi nzima ukiwemo mkoa wa
Kagera ili kutokomeza maambukizi na ugonjwa wa malaria.
Viongozi hao walionywa na Mkuu wa
Mkoa wa Kagera Mhe. John Mongella wakati wa uzinduzi wa zoezi la kugawa
vyandarua kwa wananchi Mkoani Kagera katika
Kata ya Kemondo Wilayani Bukoba Jumatano 12 Agosti, 2015.
Mhe. Mongella aliwasistiza viongozi hao kusimamia zoezi la
ugawaji bila kufanya ujanja wa
kutowatoza wananchi fedha kiwango
chochote kwani serikali imetoa vyandarua hivyo bure kwa kila mwananchi
aliyejiandikisha hapo kabla na kupewa kadi ya kuchukulia chandarua.
Pia Mhe. Mongella aliwaeleza
wananchi kuwa kila mmoja anastahili kupata chandarua hata ambaye hakupata fursa
ya kujiandikisha hapo awali au alipoteza kadi yake atajiandikisha wakati wa
zoezi na kuhakikiwa na viongozi wake na
atapewa chandarua .
Wananchi nao walionywa kutotumia
zoezi hilo kufanya udanganyifu wa kujiandikisha zaidi ya mara moja kwa nia ya
kuchukua vyandarua zaidi na atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria ikiwa
ni pamoja na matumizi mabaya ya vyandarua hivyo kama kufugia kuku, kuvua na
kutengenezea vitalu vya miti.
Katika sensa iliyofanyika hapo
awali ilibainika kuwa mkoa wa Kagera una jumla ya kaya 509,710 ambazo zitagawiwa
jumla ya vyandarua 1,810,250 ambapo kaya moja inaweza kupata zaidi ya chandarua
moja kwa kutegemea wanankaya waliopo na walioandikishwa wakati wa sensa.
Mratibu wa Malaria Mkoani Kagera
Dk. Julian Mugengi akisoma taarifa katika uzinduzi huo alisema kuwa Mkoa wa
Kagera umekuwa na historia ya milipuko ya malaria hasa katika Wilaya ya Muleba
kwa miaka ya 1997, 1998, 2007, na mwaka 2013.
Dk. Juliani alisema kuwa
katika taarifa ya utafiti wa viashiria
vya UKIMWI na Malaria ya mwaka 2007 ilionyesha kuwa mkoa wa Kagera ulikuwa na maambukizi ya
malaria kwa asilimia 42% hadi 50% na
mwaka 2010 kiwango hicho kilishuka hadi asilimia 10% hiyo ilitokana na
mabadiliko ya hali ya hewa.
Kwa mwaka 2015 wagonjwa waliopima
katika vituo vya kutolea huduma maambukizi ya malaria yalikuwa juu kwa miezi ya
Januari na Februari kwa watoto juu ya miaka 5, na watoto chini ya miaka 5
maambukizi yalikuwa asilimia 59.1%.
Aidha maambukizi ya vimelea vya
malaria yalipungua kwa mwezi Marchi hadi Juni 2015 kutokana na unyunyiziaji
wadawa ya ukoko majumbani uliofanyika katika Wilaya za Biharamulo Ngara na
Muleba na kupunguza mambukizi hadi Julai 2015 watoto chini ya miaka 5 yalikuwa
asilimia 25.7% na wakubwa asilimia 4.6% kwa wagonjwa waliopima katika vituo vya
kutolea huduma.
Kauli mbiu ya mwaka huu 2015
inasema “Wekeza kwa Maisha ya Baadae, Tokomeza Malaria”