BALOZI WA VATICAN NA MWAKILISHI WA PAPA NCHINI TANZANIA AWASILI MKOANI KAGERA KUFANYA ZIARA YA SIKU SITA
Balozi wa Vatican na Mwakilishi wa Papa nchini Tanzania, Francisco
Montecillo Padilla atembelea mkoa wa Kagera katika ziara ya kujione shughuli
mbalimbali za Kanisa Katoliki mkoani zinavyotekelezwa pia na kutoa Baraka za
pamoja kwa wakristo wa kanisa hilo.
Balozi Padilla akiwa ofisini kwa
Mkuu wa Mkoa Kagera alipowasili kumsalimia aliishukuru serikali ya mkoa wa
Kagera kwa kuwaunganisha wananchi wa Kagera
bila kujali imani zao ambapo wanafanya shughuli zao kila mmoja kwa imani
yake bila usumbufu wowote.
Pia Balozi Padilla alisema kuwa
serikali inafanya kazi moja ya kuwaudumia wananchi pia na dini zinafanya kazi
ya kuwahudumia wananchi hao hao kiroho kwa hiyo hakuna haja ya serikali na dini
kugombana wala kukwaruzana kwasababu wote wanafanya kazi moja kwa wananchi.
“Ni bora kuendeleza ushirikiano
uliopo kati ya serikali na dini na nashukuru jambo hilo linatekelezwa mkoani
Kagera, nimekuja kukagua shughuli mbalimbali hapa na kupata baraka za pamoja na
wakristo wa mkoa wa Kagera ili kujenga jamii moja yenye familia moja katika
kumtukuza Mungu.” Alimalizia Balozi Padilla.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera John
Mongella akimkaribisha Balozi Padilla alimshukuru kwa kufanya ziara mkoani
Kagera na alimweleza kuwa serikali inatambua juhudi za kanisa Katoliki katika
kuleta maendeleo kwa wananchi hasa ujenzi wa shule na hospitali kama huduma za
jamii kwa wananch,i pia kutoa huduma za kiroho zinazosaidia kukuza maadili
katika jamii.
Balozi wa Vatican na Mwakilishi
wa Papa chini Tanzania, Francisco Montecillo Padilla ziara yake imeanza leo
Septemba 3, 2015 na anatarajia kuwepo mkoani hapa kwa takribani siku sita,
aidha Balozi Padilla anatarajiwa kuongoza ibada takatifu ya maombezi ya Bikra
Maria katika hija huko Nyakijooga Parokiani Mugana Wilayani Missenyi tarehe 6.09.2015 siku ya Jumapili.
Na Sylvester Raphael